Prime
Ikulu tuitwe kupongezwa, si kusuluhishwa

Muktasari:
- Yanga ilikuwa iikaribishe Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 8, lakini usiku wa kuamkia siku ya mechi Simba ilitangaza kutocheza mechi hiyo kwa madai kuwa ilizuiwa kutumia haki yake ya kikanuni ya kufanya mazoezi mepesi kwenye uwanja huo.
HATIMAYE Rais Samia Suluhu Hassan ametatua mgogoro uliokuwa na uwezekano wa kuvuruga msimu wa soka baada ya Yanga kushikilia msimamo wa kutocheza mechi iliyopangwa tarehe mpya baada ya ile ya awali kuahirishwa kiholela.
Yanga ilikuwa iikaribishe Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Machi 8, lakini usiku wa kuamkia siku ya mechi Simba ilitangaza kutocheza mechi hiyo kwa madai kuwa ilizuiwa kutumia haki yake ya kikanuni ya kufanya mazoezi mepesi kwenye uwanja huo.
Ilisema haitacheza mechi hiyo hadi hapo waliowazuia kuingia uwanjani watakapochukuliwa hatua. Hata hivyo, kanuni haziipi klabu ambayo imezuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi haki ya kugomea mchezo, badala yake wahusika hushughulikiwa kadiri watakavyoonekana wana hatia.
Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya saa 72) haikukubaliana na tishio hilo na badala yake ikasema mchezo utafanyika kama ulivyopangwa, lakini saa mbili kabla ya mchezo, ikatangaza kuuahirisha.
Yanga haikukubaliana na uamuzi wa kuuahirisha mchezo huo ikisema kamati ilikiuka kanuni. Yanga, ambayo timu yake huweka kambi Avic Town, Kigamboni ambako ni takribani kilomita 34.2 hadi Uwanja wa Mkapa, ikasema inapeleka timu uwanjani. Ilipeleka na baadaye ikadai ipewe ushindi, jambo ambalo Bodi ya Ligi (TPLB) haikulikubali na badala yake ikapanga tarehe mpya kuwa Juni 15.

Kuanzia hapo ikawa ni malumbano na kuonyeshana ubabe. Viongozi wawili, Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Wallace Karia na Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto walitoa matamko ambayo yalichochea zaidi sakata hilo.
Akihojiwa na waandishi Uwanja wa Ndege, Karia, ambaye wakati sakata hilo linaanza alikuwa nchini Morocco kuhudhuria mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), alidhihaki madai ya Yanga ya kutaka viongozi wa TPLB wajiuzulu, akihusisha mgogoro huo na njama za kutaka kuuvuruga mpira, akisema kama ‘wamezoea waende wakacheze sinema zao’, jambo lililotia petroli kwenye moto uliokuwa hafifu.
Walitumia kifungu kisemacho kamati inaweza kuahirisha mechi ‘pale itakapoona inafaa’, lakini wakakimbia wajibu wa kuhalilisha kufaa huko, huku wakitoa sababu hafifu ya viashiria vya vurugu na rushwa.
Juhudi za Bodi ya Ligi kumaliza tatizo kwa kukutana na viongozi wa Yanga ndio zilichochea zaidi mzozo huo, hasa baada ya kudokezewa kikaoni kuwa meneja aliwazuia Simba baada ya kupigiwa simu na kigogo wa serikali.

Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Yanga kupanua wigo wa vita kwa kudai ilipwe fedha za zawadi za mashindano ya mtoano ya Kombe la Shirikisho (FA) za miaka mitatu na kuahidi kuwa isingecheza mechi ya fainali dhidi ya Singida Big Stars na kutishia kutocheza mechi za Ligi Kuu ya NBC zilizokuwa zimebakia na kutocheza msimu ujao wa ligi pia.
Tangu mzozo ulipoanza si Kamati ya Utendaji ya TFF wala Shirikisho iliyojitokeza kujaribu kusuluhisha zaidi ya kauli ya Karia ya ‘sinema zao’. Hakuna kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kilichoitishwa kujadili suala hilo. TPLB ndiyo iliyochapisha picha inayoonyesha kamati ya uongozi ya bodi hiyo katika kikao chake cha kawaida bila ya kusema kilichojadiliwa.
Mijadala ilikuwa mingi kwenye vyombo vya habari ikijaribu kuonyesha tatizo lilipo na kushauri hatua ambazo zingefaa kuchukuliwa, lakini hakukuonekana jitihada zozote kutoka kwa mamlaka za kutuliza hali.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi aliita pande zote husika katika sakata hilo, yaani Yanga, Simba, TPLB na TFF, na kuzungumza nazo kwa nyakati tofauti, lakini hakueleza yeye na timu yake waliona nini na baadaye akasema sakata hilo ni ‘mtego’ na hawezi kujitumbukiza.
Hakukuwa na upande uliokubali kurudi chini kutafuta muafaka na ilikuwa kama Yanga inasema “tuone watafanyaje” huku TFF na TPLB wakisema “watakiona cha mtema kuni”.
Madai ya Yanga yalionekana kama yangeilazimisha Bodi ya Ligi kuahirisha mchezo wa Juni 15, hali iliyosababisha Simba nayo iibuke na kusema iwapo mamlaka zitahamisha mchezo kutoka Juni 15, nayo haitacheza tena mchezo huo namba 184, hali iliyozidisha ugumu kwa TPLB kufanya uamuzi.

Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Juni 15, ndipo Mheshimiwa Rais Samia akaona busara za kuokoa hali iliyokuwa inaelekea kuwa mbaya. Aliwaita viongozi wa pande zote na kuzungumza nao na baadaye ikatoka taarifa ya kuusogeza mbele mchezo huo hadi Juni 25.
Kama nilivyoeleza hapo awali, sakata kama hilo linapoibuka ni muhimu sana kwa viongozi kuchunga kauli zao na kujizuia kufanya mahojiano na vyombo vya habari kuhusu kinachoendelea. Kauli ya Karia kuhusu “sinema zao’ ilimaanisha kuwa shauri la Yanga haliwezi kupewa umuhimu wowote kwa kuwa alishaliona halina umuhimu. Hivyo hata watuhumiwa, yaani Mnguto na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo hawakuona umuhimu wa kukaa kando, na badala yake wakaendelea na kupanga tarehe nyingine.
Ilikuwa ni muhimu kwa Rais kutodokeza lolote kuhusu kinachodaiwa na Yanga kwa kusema kama wana hoja itafanyiwa kazi na wakionekana hawana hoja, itaachwa. Ni kauli ya katikati ambayo isingemtumbukiza Karia na shirikisho lake kwenye mzozo.
Wakati mwingine kauli yenye maoni kama hayo humaanisha ni maelekezo kwa vyombo vyake kufanya uamuzi kwa mtazamo wa rais na si kwa kuangalia ushahidi na tatizo lenyewe.

Lakini hoja ya Yanga tangu mwanzo, mbali na kudai ushindi, ilikuwa ni kutaka viongozi wawili wa Bodi ya Ligi wajiuzulu. Hicho kingefanyika mapema, mgogoro usingeenda Ikulu. Lakini TFF haikuona hilo na badala yake ikadhani mgogoro ungeisha kwa mazoea.
Kwa kuwa mgogoro ulishagusa pande zote, ilikuwa ni muhimu kwa Karia kuitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tatizo lililokuwa na uwezekano wa kuvuruga mpira wa miguu. Kitendo cha kukaa kimya kwa miezi mitatu tangu sakata lilipoibuka hadi rais anaingilia kati ni udhaifu mkubwa katika uongozi na ukosefu wa stadi za usuluhishaji migogoro (conflict resolution).
Ilikuwa na uwezo wa kuunda kamati ya kuchunguza suala hilo na kuwalazimisha Mnguto na Kasongo kukaa pembeni hadi uchunguzi ukamilike, lakini haikuona umuhimu huo wakati utashi wa Yanga ulitaka kuwajibishwa kwa wawili hao.
Hoja kwamba wawili hao wasingeweza kuondolewa kwa shinikizo la timu moja, wala ile nyingine kwamba kwanini Yanga iendelee kucheza mechi nyingine na kugomea moja tu, zilikuwa nyepesi sana. Yanga walilalamikia njama za kuahirisha mechi moja tu na nyingine za ligi na mechi hiyo ndiyo moja ya mechi mbili muhimu kwao katika msimu mmoja.

Kwa hiyo, kama walifanya kosa moja katika kuahirisha mechi hiyo walistahili kuingia kwenye lawama na kutolalamikiwa na klabu nyingine isingekuwa kinga ya kosa ambalo walituhumiwa kulifanya.
Kwa hiyo, hatua zilitakiwa zichukuliwe mapema kuunusuru mchezo badala ya kuachia hadi mkuu wa nchi anajitosa kuchukua hatua ambayo ingeweza kuchukuliwa na wahusika walioomba kura za wajumbe wapewe dhamana hiyo kubwa ya kuongoza mchezo unaofuatiliwa na mamilioni ya Watanzania na wengine walioko nje ya nchi.
Hata sekretarieti ya TFF haikufanya juhudi zozote kumaliza tatizo hilo. Wakati Kasongo anaita viongozi wa Yanga kujadili maandalizi ya mchezo wa Juni 15, sekretarieti ya TFF haikuona umuhimu wowote wa kulishughulikia tatizo hilo kwa kutumia kamati zake, ikiwemo ya sheria na katiba ambayo ingeweza kujadili uamuzi wa kuahirisha mchezo kama ulikuwa sahihi na kutoa mwongozo wa nini kifanyike.

Jitihada zingefanyika kwa njia nyingi badala ya kudhani klabu moja ingeadhibiwa kwa kutumia kanuni ambazo wanaozisimamia walizivunja.
Kwa kuwa mpira wa miguu hautaki walio nje washiriki kufanya maamuzi ya kila siku, ni muhimu viongozi wakaona umuhimu wa kuunda vyombo tofauti vya haki vinavyoweza kushughulikia migogoro inayoibuka.
Ni dhahiri kwamba Yanga isingeweza kupeleka malalamiko yake kwa Bodi ya Ligi, ambayo mwenyekiti wake, Mnguto ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Saa 72 iliyoahirisha mchezo. Asingeweza kujichunguza na kufanya uamuzi tofauti na ule alioufanya ndani ya Kamati.
Yanga isingeweza kupeleka shauri lake kwenye Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi, ambayo mwenyekiti wake ni yuleyule Mnguto. Katika hali ya kawaida, kamati hiyo ya uongozi ndiyo ingewawajibisha viongozi wa bodi, lakini Mnguto angewezaje kujiwajibisha.
Kauli ya Kasongo kwamba mashauri ya Yanga yatashughulikiwa na vyombo vya juu zaidi, inamaanisha kuwa Kamati ya Utendaji ndiyo chombo cha juu katika utendaji na hivyo ingeweza kuingilia kati mapema kunusuru mpira wa miguu.
Ni vizuri kwamba Rais Samia Suluhu ametatua mgogoro huo, lakini ni vibaya kwamba viongozi wa soka wanaitwa Ikulu kujadili mgogoro badala ya kuitwa Ikulu kupongezwa kwa mafanikio ya timu za soka.
Ikulu kunatakiwa kwenda kwa ajili ya kupongezwa baada ya kupata ushindi muhimu au kwenda na kombe, lakini si kuitwa kwa sababu mmeshindwa kukubaliana wenyewe jinsi ya kumaliza mgogoro.