Aussems asifu kiwango Simba SC, Mwambusi alia uchanga Mbeya City

Muktasari:
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 21, katika michezo nane wakiwa wamepoteza mechi moja tu hadi sasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Dar es Salaam. Kocha wa Simba SC, Patrick Aussems amewapongeza wachezaji wake kwa kiwango walichokionyesha katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, uwanja wa Uhuru.
Simba imeibuka na ushindi wa mabao 4-0, yaliyofungwa na Meddie Kagere, Clatous Chama, Shaaraf Shiboub na Deo Kanda.
Aussems alisema nimefurahishwa na kiwango cha wachezaji wangu kwa sababu tumefanikiwa kupata pointi tatu.
"Tulicheza vizuri pamoja na kuwepo kwa makosa madogo madogo ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi. Kilichopo mbele ni kuendelea kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo ujao," alisema kocha huyo.
Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi alisema uchanga wa kikosi chake ndicho kilichowaangusha katika mchezo huo dhidi ya Simba.
"Kikosi changu kina vijana wengi ambao hawana uzoefu, tulikuja na lengo la kupata walau pointi moja, lakini mambo yalienda tofauti, bao la pili, liliwaondoa kabisa katika mchezo," alisema Mwambusi.
Mwambusi alisema licha ya kupoteza dhidi ya Simba, anaimani vijana wake watakaa sawa katika michezo inayokuja mbele.