Makomandoo Yanga, Simba mita mia kwa Mkapa

Muktasari:
- Yanga na Simba zitamalizana kesho kwenye uwanja huo kwenye mchezo wa kiporo namba 184 wa Ligi Kuu Bara, unaotarajiwa kupigwa kuanzia saa 11 jioni.
Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku makomandoo wa klabu za Yanga na Simba na wakilazimika kukaa umbali wa mita mia kutoka katika mageti ya uwanja huo.
Yanga na Simba zitamalizana kesho kwenye uwanja huo kwenye mchezo wa kiporo namba 184 wa Ligi Kuu Bara, unaotarajiwa kupigwa kuanzia saa 11 jioni.
Tofuati na michezo iliyopita ya timu hizo, makomandoo wakionekana kusimamia ulinzi wa timu zao, kabla ya mchezo huo wa kesho, wametakiwa kukaa mbali na uwanja huo.
Makomandoo hao wamejikusanya kwa makundi kulingana na timu zao wakiwa ng'ambo ya barabara kuu inayowatenganisha na uwanja huo, huku mageti yote yakiwa yamezingirwa na askari wa Jeshi la Polisi na hakuna mtu anayekaribia eneo hilo.
Mwanaspoti limefika uwanjani hapo usiku huu wakati mwenyeji Yanga inafanya mazoezi ya mwisho na ni timu pekee na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo ndio wameruhusiwa kuingia uwanjani hapo huku wengine wakirudishwa nyuma.
Yanga imefika uwanjani hapo huku wachezaji wakitangulia na mabasi mawili madogo aina ya Coaster na basi kubwa likiwa na viongozi.
Simba haikufika kufanya mazoezi hayo kuanzia saa 11 jioni kama ambavyo kanuni inawaruhusu wakiwa timu mgeni, lakini Yanga ikatumia nafasi yao ikienda uwanjani hapo saa 1:30 usiku.
Mchezo wa kesho ni wa mwisho kwa Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya timu nyingine 14 kumaliza mechi zao na bingwa atapatikana bada ya dakika 90.
Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa kinara kwenye msimamo na pointi 79 huku watani zao Simba ikiwa nafasi ya pili na pointi 78.