Ndayiragije: Waliotupeleka CHAN2020 kazi yao imekwisha, nasaka nyota wapya Taifa Stars

Muktasari:

Tanzania ilifuzu michuano hiyo kwa kuwaondoa Sudan mabao 2-1 wakiwa ugenini na sasa wanajiandaa katika hatua ya makundi na tayari imepangwa kundi D.

Mwanza. Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Ettiene Ndayiragije amesema wachezaji waliosaidia timu hiyo kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN2020) kazi yao ilikwisha.

Tanzania itashiriki mashindano CHAN2020 yanayotarajia kuanza Aprili 4-25 mwaka huu nchini Cameroon huku Taifa Stars ikipangwa Kundi D pamoja na Namibia, Zambia na Guinea.

Akizungumza maandalizi yake Ndayiragije amesema kikosi chake kitakuwa na mabadiliko makubwa ya wachezaji kwa kuwa waliosaidia timu kufuzu, kazi yao iliisha.

"Ndio maana unaniona leo niko Mwanza kuangalia mchezo wa Mbao na Singida ili kuona kina nani naweza kuondoka naye, nitazunguka maeneo mbalimbali ili kusaka wachezaji, wale waliosaidia kufuzu tayari kazi yao iliisha" alisema Mrundi huyo.

Ndayiragije alisema anaamini Stars itafanya vizuri na muda upo wa kujiandaa na kufafanua kuwa hata wiki moja au mbili zinatosha.

Ameeleza kuwa kikubwa ni wachezaji wenyewe kuwa tayari na kwamba mkakati wanaoufanya timu hiyo itafanya vizuri na kubainisha kuwa wapinzani watakuwa na ushindani, lakini hawaogopi kitu.

"Bado hatujachelewa timu inaweza kuingia kambini hata wiki mbili tu ikafanya vizuri, kikubwa ni wachezaji wenyewe kuwa tayari na ninaamini Stars itafanya vizuri kwa sababu tulifuzu kwa uwezo wetu na tutajiandaa" amesema Kocha huyo.