Mwamnyeto:Yanga wazuri ila Morrison ni mchezaji hatari

Muktasari:

Beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto amesema ukitaka kukabana na winga wa Yanga, Benard Morrison lazima pumzi iwe yakutosha kwa namna alivyo na kasi.

Dar es Salaam. Beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto amesema pamoja na Yanga kupata sare mfululizo bado wanakikosi bora chakuendelea ushindani Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwamnyeto alisema Yanga ina kikosi bora, akimtolea mfano winga wao Benard Morrison kuwa ni hatari akicheza mtu na mtu.

"Kwanza ukimkaba Morrison lazima uwe na pumzi yakutosha kwa sababu ni msimbufu, unamkuta kila eneo la uwanja, nilimsoma kabla ndio maana hakuweza kufurukuta mbele yangu,"amesema.

Amesema sare wanazopata Yanga hazimanishi kikosi chao kibovu na kwamba timu watakazocheza nazo kwenye mechi zilizosalia zinatakiwa kujipanga.

"Timu ambazo zinacheza na Yanga zisije zikajidanganya kwamba ni mbovu, zisipojipanga zinaweza zikapigwa mabao mengi, ina kikosi cha ushindani, kupata sare ama kufungwa na kushinda ni matokeo ambayo lazima yatapatikana baada ya dakika 90," amesema Mwamnyeto.