Prime
Ni aibu! Madudu ya waamuzi yachefua wengi Ligi Kuu

Muktasari:
- Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Hamduni alinukuliwa jana na Mwanaspoti wameanza uchunguzi wa waamuzi waliochezesha mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, kutokana na kuzagaa wa tuhuma mmoja wao ni mwanachama wa Simba.
WAKATI Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka nchini, ikisema imeanza uchunguzi kwa waamuzi waliochezesha mechi ya Simba na Mashujaa, iliyogeuka gumzo, wadau mbalimbali wa soka wakiwamo wachezaji wa zamani wameibuka na kusema kinachofanyika sasa ni aibu kwa soka la Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Hamduni alinukuliwa jana na Mwanaspoti wameanza uchunguzi wa waamuzi waliochezesha mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, kutokana na kuzagaa wa tuhuma mmoja wao ni mwanachama wa Simba.
Mechi hiyo ya kiporo cha Ligi Kuu lilipigwa Ijumaa na Simba kushinda mabao 2-1, yote kwa penalti yakifungwa na Leonel Ateba, lakini muda wa nyongeza wa dakika 15 ulioongezwa na waamuzi na utata wa penalti iliyowapa ushindi wenyeji, ndiyo limekuwa gumzo mtaani na mitandao ya kijamii.
Mwamuzi wa kati, Kefa Kayombo aliongeza dakika hizo, huku akimlima kadi ya pili ya njano kipa Patrick Munthary wa Mashujaa iliyozaa nyekundu akitoa pia penalti dk ya 90+19 iliyoonekana ya utata imezua kelele kwa mashabiki, huku baadhi ya wadau wakishindwa kujizuia na kutoa misimamo yao.

Wadau hao wamesema kilichofanyika katika mechi ya Simba na Mashujaa si tukio la kwanza kwa Ligi Kuu ya msimu huu, kwani kuna pambano yaliyopigwa siku za nyuma yalikuwa na uamuzi ya utata, lakini kinachoshangaza ni mara zote kuzihusisha timu chache, huku mamlaka zinazosimamia ligi hiyo zikinyamazia aibu hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wadau walisema, licha ya Ligi Kuu Bara kutajwa inashika nafasi ya nne kwa ubora Afrika, lakini matukio yanayoendelea ya maamuzi yenye utata hasa kwa timu moja yanaleta taswira mbaya haistahili kuwepo hapo.
Mmoja wa nyota wa zamani wa soka nchini aliyewahi kukipiga Simba, Yanga na Mtibwa Sugar pamoja na Taifa Stars, aliyeomba kuhifadhiwa jina, alisema hajui ubora wa Ligi Kuu Bara kushika nafasi nne Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS), lilitumia vigezo gani.
“Haiwezi kuwa Ligi Bora wakati waamuzi wanachezesha kwa upendeleo na hakuna kiongozi yeyote wa mamlaka ya soka anayekemea. Kuna matukio mengi ya aibu kwa ligi yetu, lakini ni kama wahusika wanaosimamia ligi wameridhika. Hawakemei na hata wanaovurunda hawaadhibiwi kukomesha vitendo hivyo. Hii inaharibu sifa ya soka la Tanzania ambalo limetoka katika shimo la sintofahamu,” alisema nyota huyo na kuongeza;
“Matokeo haya ya kubebwa kwa baadhi ya timu ndiyo yanayozifanya klabu zetu zinazowakilisha nchi kimataifa zimekuwa wasindikizaji tangu mwaka 1968 tulipoanza kushiriki michuano hiyo, zikipitwa na klabu changa zilizobeba mataji ya michuano ya CAF. Tusikubali aibu hii.”

Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema kwa hatua iliyofikia ni wazi TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), wanapaswa kujitokeza hadharani kulaani vitendo hivi vinavyoturudisha kimaendeleo zaidi.
“Ukiangalia tunasema ligi yetu inashika nafasi ya nne kwa ubora Afrika, ila ninachokiona sisi tumevaa suti lakini nguo zetu za ndani ni chafu. Kitu kibaya kinachoniumiza ni kuona wahusika wenyewe wamejifungia na wala hawawajibiki,” alisema Angetile.
Angetile alisema kinachopaswa kufanyika ni Rais wa TFF, Wallace Karia na viongozi wa Bodi ya Ligi (TPLB) kujitokeza ili kukomesha matukio tata yanayotuharibia, ikiwezekana wachunguze na hatua kali kwa wababaishaji zichukulie kwa haraka sana.
“Hizi adhabu zinazotolewa na Kamati ya Ligi hazijitoshelezi, kwa sababu Rais amejiwekea mamlaka makubwa ya kiuongozi, basi ni vyema na huku akachukua uamuzi mgumu ili kwa pamoja tunusuru kasumba hii inayoendelea kila kukicha,” alisema Angetile.

WASIKIE WAKONGWE
Nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika na timu za Tumbaku, Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’, alisema kinachoendelea ni wazi vyombo vya usimamizi havikwepi lawama, hivyo ili kuondoa hali hii ni lazima wafanye uamuzi mgumu.
“Tatizo lililopo tunaangaliana sana usoni hasa zinapokuja suala la Yanga na Simba, kwa mfano tukio lao la kugomea mechi ingekuwa timu ndogo uamuzi ungeshatolewa mapema sana, ila angalia kinachoendelea hadi sasa ni kuogopana tu,” alisema Mogella.
Mogella aliongeza kinachoonekana ni wazi wasimamizi wa Ligi ni waoga wa kufanya uamuzi hasa linapokuja suala la Yanga na Simba, ingawa kama tunataka soka letu lipige hatua ni lazima tuondokane na jinamizi hilo ambalo ndilo linalotuangusha.

Nyota mwingine wa kimataifa aliyewika na Biashara Shinyanga, Yanga, Simba, Malindi na Taifa Stars, Edibily Lunyamila alisema Bodi ya Ligi (TPLB), inapaswa kufanya uamuzi mgumu kwa mechi zilizosalia kumalizia msimu huu, ili isionekana vigogo hao nchini ndio wenye haki tu ya kushinda.
“Shida ni kushindwa kwa viongozi kuwajibika, yaani mwamuzi unaona leo kakosea tena zaidi, kesho tena unamuona anachezesha timu hiyo hiyo, tumefikia hatua ya kuona Simba na Yanga zina haki ya kushinda ila wengine hawana jambo ambalo ni aibu kubwa kwa soka letu.”
Lunyamila alisema ifike wakati mechi zote apewa mwamuzi Ahmed Arajiga tu kama wengine wameshindwa kuonyesha weledi na kusababisha sintofahamu ambayo inazidi kuliweka soka letu katika taswira mbovu, licha ya hatua kubwa zinazoonekana wazi.
“Soka letu limepiga hatua sana lakini matukio madogo kama haya ya waamuzi ndio yanayoturudisha nyuma, ifike wakati tuone Arajiga akichezesha mechi zote kwa sababu kaamua kufuata weledi kuliko wenzake ambao kila kukicha wanasingizia makosa ya kibinadamu.”

Katika mitandao ya kijamii mashabiki na wapenzi wa soka wamekuwa wakishutumua ukimya wa viongozi wa Bodi ya Ligi na TFF kwa jumla, huku baadhi wakisema inaleta picha kuna timu inatengenezewa mazingira ya ubingwa wa msimu huu, kwa kuorodhesha matukio tata ya timu husika.
Hata hivyo, mashabiki wengine wamekuwa wakirejea matukio kadha ya utata yakihusisha zaidi ya timu moja, ikiwamo lile la bao la mkono la beki wa Yanga, Ibrahim Bacca dhidi ya Tanzania Prisons, penalti yenye utata ya mechi ya Namungo dhidi ya Dodoma Jiji, utata wa mechi ya Namungo dhidi ya Simba na mwamuzi Japhet Smart alitoa kadi nyekundu kwa beki Derrick Mukombozi wa Namungo kisha kuizawadia Simba penalti tatu wakati ikishinda 3-0 kabla ya kadi hiyo kwa beki huyo kufutwa.
Hakuna kiongozi wa TFF wala wa Bodi ya Ligi waliopatikana jana kutolea maelezo juu ya hali iliyopo kwa sasa katika ligi hiyo, lakini juzi Mwenyekiti wa Mwamuzi alisema sheria na kanuni zinawabana waamuzi kuwa wanachama wa klabu na wameanza uchunguzi kwa waamuzi wa mechi ya Ijumaa.