Mtibwa: Yanga wanapigika tu

KOCHA wa Mtibwa, Zubery Katwila amesisitiza kutowahofia Yanga hata kidogo kwenye mechi ya kesho Jumapili ndani ya Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Mtibwa licha ya msimu uliopita kumaliza ligi ikiwa katika nafasi mbaya ya kunusurika kushuka daraja, msimu huu imejipanga kufanya vizuri zaidi na sio kusubiri hadi mwisho wa ligi ndio waanze kujipapatua kupata matokeo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Katwila amesema; “Sawa Yanga wana wachezaji wa kigeni lakini tumekuwa tukikutana nao na wanapata wakati mgumu kupata matokeo, mimi nawaamini sana wachezaji wangu kwani uwezo wa kufanya vizuri wanao. Hata Simba wana wachezaji wa Kimataifa, lakini tulitoka nao sare katika mchezo uliopita na Simba ndio mabingwa watetezi lakini kazi waliiona, hivyo hata Yanga wajiandae tu mpira dakika 90.”
Mtibwa imecheza mara tatu katika Ligi Kuu Bara msimu huu sawa na Yanga ikishinda mechi moja dhidi ya Ihefu waliyoifunga bao 1-0, ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba na suluhu dhidi ya Ruvu Shooting.
Huku wapinzani wao Yanga wakitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, ikiwafunga Mbeya City bao 1-0 na kuwafunga pia Kagera Sugar ba 1-0.