Prime
Dau la Aziz KI laipa jeuri Yanga SC

Muktasari:
- Aziz KI ambaye aliitumikia Yanga kwa misimu mitatu mfululizo anakwenda Wydad akianzia katika mashindano ya Klabu Bingwa Dunia ambapo itacheza dhidi ya Manchester City ya England, Juventus (Italia) na Al Ain (United Arab Emirates).
STEPHANE Aziz KI ameipa jeuri kubwa Yanga na hiyo ni baada ya dili la kujiunga na Wydad Athletic Club ya Morocco kuhusisha kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimeingia Jangwani.
Aziz KI ambaye aliitumikia Yanga kwa misimu mitatu mfululizo anakwenda Wydad akianzia katika mashindano ya Klabu Bingwa Dunia ambapo itacheza dhidi ya Manchester City ya England, Juventus (Italia) na Al Ain (United Arab Emirates).
YANGA BILIONI 2
Yanga imekubali yaishe baada ya kuibana Wydad iliyokubali kutoa kiasi cha Sh2 bilioni kunasa saini ya kiungo huyo raia wa Burkina Faso ikiipiku FAR Rabat iliyokuwa tayari kutoa Sh1.6 bilioni.
Waarabu hao (Wydad) walitumia ushiriki wao wa kucheza mashindano ya Klabu Bingwa Dunia kama akili ya kurahisisha na kupata saini ya kiungo huyo kwa haraka. Wydad imelazimika kutoa kiasi hicho cha fedha kama sehemu ya kununua mkataba wa Aziz KI na Yanga uliobaki mwaka mmoja.
DAU LA USAJILI
Bado fedha itaingia kwa Aziz KI kwani hatua ya kukubali kusaini dili hilo ataweka kwenye akaunti yake kiasi cha dola 360,000 (Sh965 milioni) kama dau la usajili ambalo litaingia kwa makundi mawili.
Mwaka wa kwanza kiungo huyo atapewa dola 250,000 Sh670 milioni) wakati huu anakwenda kujiunga na kikosi hicho mara tu atakapomaliza kupimwa afya na kusaini mkataba.
Kiungo huyo kabla ya kuanza mwaka wa pili wa mkataba wake, ataingizwa sehemu ya mwisho ya malipo hayo ambayo ni dola 110,000 (Sh295 milioni).
Ukichukua Sh2 bilioni za kununua mkataba na Sh965 milioni za dau la usajili, jumla mauzo ya Aziz KI yanafika Sh 2.9 bilioni.
Fedha hizo zinaweza kuifanya Yanga kuwa klabu iliyoingiza mkwanja mrefu zaidi katika kuuza staa wake kwa hapa nchini.
Rekodi zinaonyesha Agosti 2021, Simba ilimuuza Luis Miquissone kwenda Al Ahly ya Misri kwa euro 850 (Sh2.6 bilioni). Julai 2023, Fiston Mayele alijiunga na Pyramids ya Misri kwa euro 733,000 (Sh2.2 bilioni), wakati Julai 2024, Azam ilimuuza Kipre Junior kwenda MC Algiers ya Algeria kwa euro 276,000 (Sh831 milioni).
Kwa kuingiza fedha hizo, Yanga sasa ina jeuri ya kumrudisha Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka Azam ambapo amebakiza mkataba wa mwaka mmoja baada ya kujiunga na timu hiyo Julai 2023 akitokea Yanga.
Hivi karibuni, Mwanaspoti liliripoti kuwa Yanga imemwambia Fei Toto, atakapokubali kurejea, imemuwekea ofa ya Sh800 milioni, ikimwambia pia itampa mshahara anaoutaka wa Sh40 milioni.
MSHAHARA WAKE
Mshahara wa Aziz KI akiwa Wydad nao ni kufuru nyingine ukiwa ni mara mbili ya ule aliokuwa anachukua Yanga.
Kitendo cha kukubali kutua Wydad, Aziz KI amewekewa mshahara wa Dola 27,000 sawa na Sh72.3 milioni kwa mwezi, katika kikosi cha Yanga, kwa mwezi alikuwa akilipa Dola 13,000 sawa na Sh34.9 milioni.
Kiungo huyo kwa hesabu hizo zitamfanya kwa mkataba wa miaka miwili atakaosaini wenye kipengele cha kuongeza mwaka zaidi atachukua jumla ya Sh1.7 Bilioni kwa miezi 24 atakayoichezea Wydad.
YANGA YAWABANA WAARABU
Kwenye mkataba huo, Yanga haijawaacha na uhuru Wydad kwani pia kama Aziz KI akiuzwa Ulaya ndani ya miaka hiyo miwili, itavuna fedha nyingine kwenye mauzo yake. Yanga pia imeweka masharti kwamba endapo Aziz KI atakutana na wakati mgumu Wydad na akatakiwa kuuzwa au kuondoka, basi mabingwa hao wa Tanzania watapewa nafasi ya kwanza kuzungumza naye.
Akili ya Yanga ni kuzuia kiungo huyo kutua kwa wapinzani wake Tanzania wakiwemo Simba na Azam ambazo ziliwahi kumuhitaji kiungo huyo.
Aziz KI ameondoka Yanga akiwa na rekodi ya kufunga mabao tisa kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, mechi yake ya mwisho akicheza dhidi ya JKT Tanzania katika nusu fainali ya Kombe la FA, Jumapili iliyopita.
Katika ishu nyingine, mauzo hayo ya Aziz KI umeifanya Yanga kumsubirisha Clement Mzize ambaye inataka kumuuza nje ya Afrika baada ya kuona hadi sasa hakuna timu iliyofikia dau lake.
Mwanaspoti liliwahi kuripoti Mzize alikuwa anatakiwa na Al Ittihad ya Libya na Wydad, huku ada yake binafsi ya kusaini mkataba (sign-on fee) ni zaidi ya Sh1.3 bilioni.