Prime
Simba yatembea na rekodi 7

Muktasari:
- Wakati hali ikiwa hivyo, kuna rekodi inaifukuzia ambayo inaonekana ni pasua kichwa. Katika mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ngazi ya klabu, rekodi zinaonyesha kuna timu saba pekee zilizopindua matokeo baada ya kupoteza fainali ya kwanza ugenini kwa mabao kuanzia mawili.
SIMBA inapiga hesabu kuhakikisha inapindua matokeo ya kufungwa mabao 2-0 ugenini katika fainali ya mkondo wa kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ili kubeba ubingwa Jumapili, wiki hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Wakati hali ikiwa hivyo, kuna rekodi inaifukuzia ambayo inaonekana ni pasua kichwa. Katika mashindano yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ngazi ya klabu, rekodi zinaonyesha kuna timu saba pekee zilizopindua matokeo baada ya kupoteza fainali ya kwanza ugenini kwa mabao kuanzia mawili.
Mwaka 1966 katika fainali ya African Cup of Champions Clubs ambayo kwa sasa ni Ligi ya Mabingwa Afrika, Stade d’Abidjan ya Ivory Coast ilipoteza mchezo wa kwanza ugenini kwa mabao 3-1 dhidi ya Real Bamako kutoka Mali, nyumbani ikaenda kushinda 4–1 na kubeba ubingwa kwa mara ya kwanza matokeo ya jumla yakiwa 5-4.
Katika michuano hiyo pia mwaka 1971, Asante Kotoko ya Ghana iliichapa Canon Yaoundé kutoka Cameroon mabao 3–0, marudiano Canon Yaoundé ikashinda 2–0.
Kwa wakati huo, ilikuwa ikiangaliwa matokeo ya ushindi yapoje bila ya kujali idadi ya mabao, hivyo licha ya Canon Yaoundé kufungwa 3-0 kisha ikashinda 2-0 na matokeo ya jumla kuonekana kupoteza kwa 3-2, lakini ilibebwa na kanuni hiyo kwamba matokeo yalikuwa sare, ikalazimika kuchezwa mechi ya tatu kumsaka mshindi ambapo dakika ya 82, mashabiki wa Asante Kotoko walivamia uwanja wakati Canon Yaoundé ikiwa mbele kwa bao 1-0. Kutokana na vurugu hizo, mechi ikavunjika na Canon Yaoundé ikatwaa ubingwa ukiwa ni wa kwanza kwao katika mashindano hayo. Baadaye kanuni hiyo ikaondolewa na kuwekwa bao la ugenini pindi timu zikilingana idadi ya mabao.
MC Alger ya Algeria nayo ilipindua meza mwaka 1976 katika michuano hiyohiyo. Mchezo wa kwanza ilipoteza ugenini kwa mabao 3-0 dhidi ya Hafia FC kutoka Guinea, marudiano ikapata ushindi kama huo, mikwaju ya penalti ikaibeba MC Alger ikishinda 3-1. Katika michuano ya Kombe la CAF mwaka 1996, Étoile Sportive du Sahel ya Tunisia ilishinda nyumbani 3–1 dhidi ya Kawkab Marrakech, lakini ikaenda kupoteza ugenini kwa mabao 2-0 na Kawkab Marrakech ya Morocco kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza.
Mwaka 2003 katika fainali ya Kombe la Washindi ambalo 2004 lilikuja kuunganishwa na Kombe la CAF ikazaliwa Kombe la Shirikisho Afrika, Julius Berger ya Nigeria iliichapa Étoile Sportive du Sahel ya Tunisia mabao 2–0, ikaenda ugenini kuchapika 3-0 na Étoile du Sahel ikatwaa ubingwa kwa matokeo ya jumla 3-2.
Stade Malien ya Mali ilishinda ubingwa wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2009 baada ya kupindua meza mbele ya ES Sétif ya Algeria kufuatia mechi ya kwanza ugenini kufungwa 2–0, kisha nyumbani ikapata ushindi kama huo, ikaenda kushinda kwa penalti 3–2.
Espérance de Tunis ya Tunisia ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018 mbele ya Al Ahly baada ya mchezo wa kwanza ugenini kupoteza kwa mabao 3-1. Wakati ikionekana Al Ahly imemaliza kazi huku rekodi yake ya kuwa bingwa wa kihistoria wa michuano hiyo ikimbeba, ikashangazwa ilipoenda Tunisia kwani ilikubali kichapo cha mabao 3-0. Espérance de Tunis ikatwaa ubingwa kwa ushindi wa jumla 4-3.
Ukiweka kando hilo, Simba imewahi kupita kwenye nyakati ngumu kama hizi kwa kupoteza mechi ya kwanza iliyofanya baadhi ya watu kuikatia tamaa, lakini ikarekebisha mechi ya pili na kuvuka hatua inayofuata.
Mwaka 1979 katika hatua ya kwanza ya African Cup of Champions Clubs, sasa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilifungwa nyumbani 4-0 na Mufulira Wanderers ya Zambia, ikaenda ugenini ikaibuka na ushindi wa mabao 5-0, ikatinga hatua ya pili kwa mabao 5-4.
Msimu wa 2018–19 katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya mtoano, Simba ilipoteza kwa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Nkana ya Zambia, nyumbani ikashinda 3-1 na kufuzu makundi kwa jumla ya mabao 4-3.
Msimu huu kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0 dhidi ya Al Masry ya Misri, nyumbani ikashinda 2-0 matokeo ya jumla yakawa 2-2, kwenye penalti, Simba ikashinda 4-1 na kufuzu nusu fainali.
NINI KIFANYIKE?
Kocha Julien Chevalier anayeifundisha ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambayo msimu huu iling’olewa na RS Berkane kwenye hatua ya robo fainali kwa mabao 2-0, alisema Fadlu anatakiwa kuimarisha ulinzi na kuuanza mchezo kwa kasi akiwapa nafasi wachezaji ambao wanaweza kushambulia kwa haraka.
Kocha huyo alimtaja mshambuliaji Steven Mukwala ambaye hakucheza mchezo wa kwanza Morocco akisema anatakiwa kupewa nafasi kutokana na kasi na nguvu.
Naye kocha Kheireddine Madoui wa CS Constantine ya Algeria timu pekee iliyoifunga RS Berkane kwenye michuano hiyo msimu huu zilipokutana katika hatua ya nusu fainali, alisema Simba haitakiwi kurudia makosa ya safu ya ulinzi kuruhusu mabao mapema kipindi cha kwanza.
“Tulifanya makosa (Constantine) kwenye ulinzi tukaruhusu mabao mengi mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Berkane, Simba haikufanya makosa hayo, mabao mawili wanaweza kuyarudisha,” alisema Madoui ambaye alishuhudia Constantine ikifungwa 4-0 ugenini na nyumbani ikaenda kushinda 1-0.