Mkenya afichua siri za Kaze Yanga

YANGA ipo uwanjani leo katika mchezo wa kwanza wa kocha wa timu hiyo Cedric Kaze tangu apewe kibarua hicho lakini kipa wake mmoja akamsoma kisha akagundua kwamba kuna safari ngumu timu pinzani zitaianza muda si mrefu juu ya Yanga.

Kipa aliyefunguka hayo ni Farouk Shikhalo ameiambia Mwanaspoti, Kaze katika siku takribani tano alizokaa na kikosi hicho amegundua jamaa amekuja na mbinu za soka la kisasa zaidi.

Shikhalo alisema alichomsoma Kaze ni kwamba jamaa anataka kuingiza mifumo ya kisasa kwa timu kukaba kisasa lakini pia kushambulia kwa mbinu hatua ambayo zitaziumiza timu nyingi pinzani.

“Huyu (Kaze) ni kocha bora sana sasa naelewa kwanini alikuwa nje kwa muda mrefu, kuna vitu ambavyo anataka tufanye, naona wazi Yanga itakuwa inacheza soka la kisasa zaidi kushinda timu zote hapa Tanzania,” alisema Shikhalo.

“Ukiangalia haraka anataka kuona timu inakaba kwa nidhamu ya kisasa zaidi na sio zile mbinu za kutegemea viungo wakabaji pekee, anataka kuona ukabaji ukianzia juu kule kwa washambuliaji lakini kwa mbinu sana,” alisema kipa huyo Mkenya na kuongeza;

“Muda mwingi anataka kuona timu yake ndio inamiliki mpira na ikitokea wapinzani wana mpira basi haraka anataka wapokonywe umiliki. Hizi ni mbinu zinazotumiwa na klabu kubwa sana Ulaya.”

Aidha, Shikhalo alisema kazi kubwa iliyobaki sasa ni wao kama wachezaji kushika haraka mifumo na kile anachotaka kocha huyo ambapo kama hilo litakamilika kwa haraka basi kuna hatari Yanga ikawa hatari zaidi.

“Kitu muhimu sasa ni kwetu kama wachezaji kushika kwa haraka kile ambacho kocha anataka tufanye, kama tukifanikiwa hilo naona kuna timu nyingi zitakuwa katika wakati mgumu zitakazokutana na Yanga,” alisema Shikhalo.