Mbao yasisitiza haki uwanjani

Muktasari:

Khaji alisema kwa sasa hali si shwari kikosini kutokana na matokeo yao, hivyo wanaenda kupambana kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.

BAADA ya kupata sare mchezo uliopita dhidi ya Alliance FC, Kocha wa Mbao, Abdulmutiki Khaji amesema wanaenda kupambana kufa na kupona kusaka pointi tatu dhidi ya Biashara United ili kujinasua nafasi za chini.

Mbao ambayo inashika nafasi ya 16 ikiwa na pointi 19, itakuwa ugenini Uwanja wa Karume mjini Musoma ukiwa ni mchezo wake wa 21 utakaopigwa leo Jumanne.

Biashara yenyewe inashika nafasi ya 16 kwa kukusanya pointi 25 inatamba kubakiza pointi tatu uwanja wake wa nyumba ambapo timu zote zimecheza mechi 20.

Khaji alisema kwa sasa hali si shwari kikosini kutokana na matokeo yao, hivyo wanaenda kupambana kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.

Alisema licha ya kwamba ratiba imekuwa ngumu, lakini hawana la kufanya isipokuwa kila mchezo kwao ni fainali ili kujinasua katika nafasi za chini.

“Ni mchezo ambao utakuwa mgumu kwa sababu tunawafahamu wapinzani walivyo, hivyo tunaenda kwa umakini na tahadhari ili kufikia malengo yetu,” alisema Mutiki.

Kocha huyo aliongeza kuwa kutokana na hali ilivyo, waamuzi wanapaswa kutenda haki ili timu ipate matokeo kwa uwezo wake na kwamba vinginevyo mambo yatakuwa mabaya.

“Kwa mfano mechi yetu na Alliance, tunafunga bao halali lakini mwamuzi analikataa kwa matakwa yake, kwahiyo hali hii inapoteza morali kwa wachezaji wakati tunapambana kutoshuka daraja,” alisema kocha huyo alipokuwa akiuzungumzia mchezo wa Jumamosi.