Mbao FC watajilaumu wenyewe

Muktasari:

Kwa sasa mpira ni mapumziko,ambapo Azam anaongoza bao 1-0 dhidi ya Mbao FC ambapo ambapo dakika 90 zikimalizika hivyo,Mbao atakuwa amepoteza  mchezo wa nne kati ya saba kwa Azam tangu apande Ligi Kuu.

TIMU ya Mbao itajilaumu yenyewe kipindi cha kwanza kwa kukosa penalti iliyopigwa na straika wao Waziri Junior dakika ya 25 baada ya kuangushwa eneo la hatari na beki wa Azam, Agrey Moris na kusababisha timu yao kwenda mapumziko ikiwa nyumba bao 1-0.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara inachezwa uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa ambapo hadi mapumziko Azam walikuwa wanaongoza kwa bao hilo lililofungwa na beki wao Yakub Mohammed.
Azam walionekana kuanzia mapema kuhitaji mabao ya haraka kutokana na mashambulizi waliyoyafanya lakini walishindwa kutulia katika kutimiza malengo yao.
Mbao ambao ni wenyeji wa mchezo huo walionekana kukosa mawasiliano hasa eneo la ulinzi jambo ambalo liliipa Azam nafasi ya kulisakama zaidi lango la wapinzani na kufanikiwa kupata bao dakika ya 15 kupitia beki huyo.
Azam licha ya kupata bao hilo iliendelea kufanya mashambulizi zaidi ya wapinzani wao lakini kipa wa Mbao, Abdalah Makangana alilazimika kufanya kazi ya ziada ya kuokoa mikwaju mingi langoni mwake na kuifanya timu yake kupumzika ikiwa nyuma kwa bao moja.
Iwapo mpambano huo utanalizika kwa matokeo hayo, itakuwa ni mwendelezo mbaya kwa Mbao kwenye mechi za nyumbani kutopata matokeo mazuri tofauti na wanavyokuwa ugenini.