Makocha Warundi wanavyobamba TPL

Tuesday October 15 2019

 

By Mwandishi wetu

KATI ya mambo yanachoshangaza kwenye Soka la Bongo ni uwepo wa makocha wengi kutoka nchi za Burundi na Rwanda.

Ligi Kuu Bara ndio inaongoza kusheheni makocha tofauti kutoka mataifa hayo ya Afrika na hivyo kuwaacha mbali wazawa.

Simba iliwahi kuwa na kocha Mrundi Masoud Djuma ambaye kwa sasa amepata dili la kuinoa timu ya Bukavu Dawa ya DR Congo, Mwadui ilikuwa na mnyarandwa Ally Bizimungu ambaye alitimka baada ya msimu uliopita wa Ligi Kuu kumalizika.

Mbeya City ilikuwa na Mrundi Ramadhan Nsanzurwimo ambaye kwa sasa wameachana naye na ametua Singida United wakati Stand United iliwahi kunolewa na Mrundi Niyongabo Amas ambaye kwa sasa hayupo na kikosi hicho.

Makocha ambao wameendelea kusalia kwenye Ligi Kuu Bara ni Mrundi Ettienne Ndayiragije wa Azam na timu ya Taifa ya Tanzania’Taifa Stars’, Mnyarwanda Hitimana Thierry wa Namungo FC na Mrundi Haerman Huruma ambaye amejiunga na Lipuli hivi karibuni.

Makocha hao wote wameonyesha uwezo mkubwa wa kuzinoa timu zao lakini jambo la kuvutia wanazungumza kiswahili hivyo wachezaji wengi kuwaelewa.

Advertisement

Uwepo wa makocha hao umeibua maswali kuwa kwa nini wengi wanakuja kufundisha hapa na si pengine, au ni rahisi zaidi kwao kupata kazi Tanzania kuliko sehemu nyingine?.

Kocha wa zamani wa Simba, Masoud Djuma anasema kuna mambo matatu yanayochangia makocha kutoka Burundi na Rwanda kuja wengi kufundisha Tanzania.

“Jambo la kwanza ni lugha kwani wote tunazungumza kiswahili vizuri hivyo inakuwa rahisi kuwasiliana na wachezaji uwanjani na hata hata watu wengine.

“Pili Elimu.Makocha wengi wa Burundi wanapenda kusoma hivyo mnajikuta mnakuwa wengi katika nchi yenu na kazi hakuna na ndio maana wengi wanatoka nje ya nchi yao kusaka kazi sehemu nyingine.

“Jambo la tatu ni kipato kwani ukiangalia vipato vya Burundi, Rwanda na Tanzania havitofautini sana hivyo ni rahisi mkocha kutoka Burundi kwenda kufanya kazi Tanzania kwani anajua anapata kipato kile kile,” anasema Djuma.

Djuma amesema tatizo kubwa linalowakwamisha makocha wazawa wa Tanzania kushindwa kupata nafasi nje ya nchi yao ni kukosa elimu.

“Lazima wajitahidi kusoma kwani huwezi kutoka kwenda nchi nyingine kufundisha kama huna ujuzi hasa wa elemu ili ikisaidie kupata leseni ambayo itakuwezesha kufanya kazi kokote Duniani.

“Maana unaweza ukamuona kocha Tanzania ni mzuri na kuna timu labda nje inamtaka lakini anashindwa kwenda kwa sababu hana elimu ya kutosha inayomuwezesha kwenda huko.

“Lakini pia Watanzania wengi hawana roho ngumu wanapenda sana kwao tofauti na sisi Waburundi yaani ni kama tunajilipia, tunatoka kwenda kusaka kazi nchi yoyote na wala hatujali litakalotukuta mbele ndio maana tunafanikiwa,” anasema Djuma.

Djuma anasema kama mtu hautoki huwezi kujua kama nje kuna jua au mvua hivyo kuwataka makocha wa Tanzania kuchangamka kuhakikisha wanatoka na kwenda kufundisha nchi za wenzao kama makocha wageni wanavyomiminika katika nchi yao.

Naye kocha wa Namungo FC, Hitimana Thierry anasema elimu na uwezo walio nao unawavutia timu nyingi kuhitaji huduma yao ndio maana wanakuja Tanzania kufanya kazi.

“Zamani makocha walikuwa wanafanya kazi hata bila uzoefu lakini sasa hivi hadi uwe na elimu ya darasani na ya ukocha ya kiwango fulani ndipo unakuwa na vigezo vya kufundisha ligi mbalimbali.

Mawakala wanatusaidia kututafutia kazi sehemu tofauti na ndio maana unaona hata mimi niko hapa Tanzania nafundisha lakini pia kocha mwenyewe unatakiwa kujiongeza kusaka kazi sehemu mbalimbali.

“Pia makocha inatakiwa kusoma sana,ili kufuzu vigezo vya kufundisha timu sehemu tofauti. Mfano ligi ya Rwanda kwa sasa ina makocha watano tu wanaotoka katika nchi hiyo lakini wengine wote ni wageni na hiyo inatokana na kwamba makocha wengi wana hawataki kujiendeleza kielimu,” anasema Hitimana.

Kocha wa zamani wa Mwadui, Ally Bizimungu anasema makocha wengi wa Burundi na Rwanda hawana tabia ya kujibana katika nchi zao bali wanapenda kutoka na kwenda kufundisha nchi nyingine.

“Tabia ya kujibana na kukaa nyumbani tu hatuna, huwa tunapenda kutoka na kusaka maisha sehemu nyingine. Makocha wa nchi hizo hawana hofu na kitakachotokea mbele popote wanapokwenda.

“Pia kama mimi vigezo ninavyo vya kufundisha kokote hivyo jambo kubwa linalotubeba ni elimu tuliyonayo, wengi tunapenda kusoma na kujiendeleza katika fani yetu ya ukocha,” anasema Bizimungu.

Kocha wa Azam,Etienne Ndayiragije anasema elimu na vigezo ndiyo sababu kubwa ya makocha wengi kutoka nchi hizo kupata kazi ya kufundisha soka Tanzania.

“Hakuna kitu kingine zaidi ya kwamba tuna elimu ya kutosha na vigezo ndio maana timu nyingi zinatupa kazi,” anasema kwa ufupi Ndayiragije.

Advertisement