Kiungo mpya Jangwani afunguka mazito

Muktasari:

Asimulia alivyoshuhudia mwenzake akichomwa kisu na wahuni hadi kupoteza maisha walipokwenda kucheza ndondo.

KIUNGO mpya wa Yanga, Zawadi Mauya (27), anatambua wazi ametua kwenye timu yenye ushindani na maono makubwa anayoamini yatamfanya ajitume na kiwango chake kuonekana ndani na nje ya nchi.

Ni wazi atakaumbana na changamoto ya nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutoka kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Abdulaziz Makame na kukiri alishawasoma tangu akiwa Kagera Sugar.

Mauya ni kati ya wachezaji saba waliosajiliwa ndani ya kikosi hicho, wengine ni Waziri Junior (Mbao FC), Bakari Mwamnyeto (Coastal Union), Kibwana Shomary (Mtibwa Sugar), Mustapha Yassin (Polisi Tanzania), Farid Mussa (CD Tenerife B) na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (MFK ya Jamhuri ya Czech).

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Mauya na amefunguka mambo mengi kuhusu soka lake ikiwamo la kusikitisha linalohusu mauaji aliposhuhudia mwenzake akichomwa kisu hadi kufa wakati wa mechi za ndondo.

AANZIA MCHANGANI

Anasema katika safari yake ya soka, alianzia mchangani na huko amejifunza mengi na kukiri huko ni noma sana.

“Ujue nimeanzia mchangani, siwezi kutaja timu zote nilizocheza huko chini, lakini nimejifunza na kuumizwa na mengi. Hata hivyo, safari bado inaendelea kwani soka ndio maisha yangu.”

AKUMBUKA TUKIO LA MAUAJI

Huku akionyesha huzuni, anasimulia alivyoshuhudia mwenzake akichomwa kisu na wahuni hadi kupoteza maisha walipokwenda kucheza ndondo.

“Ilikuwa mwaka 2016, nilienda kucheza ndondo katika mkoa mmoja hivi (Anashindwa kuutaja ili kuepusha kukumbusha maumivu kwa wanafamilia wa ndugu yao).”

Anaendelea, “Sehemu hiyo haikuwa salama kutokana na wahuni walikuwa wengi kama unavyojua mechi za mchangani. Kila anajiona mjuaji, vurugu za hapa na pale na mambo mengine. Siku hiyo kulizuka vurugu na mwenzangu alichomwa kisu na kufariki dunia pale pale.”

Anasema tukio hilo lilivunja mechi huku wachezaji na mashabiki wakibaki na mshangao na hofu kubwa kwa kutoamini kilichotokea.

Anasema alishuhudia mhusika akikamatwa na polisi lakini hakufuatilia kilichoendelea kwani alikuwa kwenye masikitiko makubwa ya kifo cha mwenzake na kukiri hadi sasa hawezi kwenda sehemu yenye wahuni.

ALIVYOTUA YANGA

Amefunguka Yanga ilianza kuwinda saini yake baada ya kuifunga 3-0 kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar aliyokuwa akiichezea kutokana na mabao ya Yusuph Mhilu, Ally Ramadhani na Peter Mwalyanzi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Anasema kwenye mchezo huo alionyesha kiwango bora na kuisumbua sana Yanga na baada ya hapo ikaanza kumfukuzia.

“Injinia Hersi Said ndiye alinipigia simu na baadaye nikakutana naye na kufanya makubaliano kisha kusaini,” anasema na kuongeza anajua kunachangamoto kubwa Yanga kutokana na presha ya mashabiki, hivyo atahakikisha anayasoma mazingira ili kuendana na timu hiyo.

“Changamoto zitakuwa mbili kubwa, kuikabili presha ya mashabiki na kuonyesha kiwango kwenye nafasi yangu ya kiungo kuhakikisha napata nafasi ya kucheza,” anasema.

AMPA TANO LUHENDE

Beki huwa hasifiwi, lakini Mauya hasiti kufanya hivyo na kukiri msimu ulioisha beki wa Kagera Sugar, David Luhende alionyesha kiwango bora na licha yakutofanikiwa kupata tuzo za Ligi Kuu Bara (VPL), uwezo aliuonyesha ulikuwa na mchango mkubwa ndani ya timu.

Anafunguka, “Luhende alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu, achilia mbali kuibeba timu pia alikuwa mwiba kwa washambuliaji wa timu pinzani, anajitambua yeye ni nani katika kazi yake,” anasema.

BOBAN NAYE

Katika nafasi ya kiungo, Mauya hafichi hisia zake kwa kiungo fundi wa mpira, Anamtaja Haruna Moshi ‘Boban’ anamkosha zaidi kutokana na kipaji chake.

“Niwe mkweli kiungo ambaye namkubali mpaka kesho kwa aina yake ya uchezaji na kuna wakati natamani nikae pembeni nimwangalie kipaji chake, ni Boban. Ana madini mengi ambayo wengi wao hawana kwenye Ligi Kuu Bara,” anasema Mauya na kuongeza;

“Boban hana papara, anajua kumiliki mpira, anajiamini, mpambanaji, kifupi ana kila kitu kiungo anachostahili kuwa nacho. Binafasi natamani kumwona anacheza ligi kuu, ana heshima na amekuwa kioo cha watu wengi, kupenda kucheza nafasi hiyo.”

NAFASI YAKE YANGA

Anakiri haitakuwa rahisi kupata namba ndani ya kikosi cha kwanza, akiamini nafasi yake ina wachezaji wenye ushindani anaoupenda kuona utaisaidia timu kuwa imara.

“Kuna Feisal Salum ‘Fei Toto, Abdulaziz Makame ambao ni wenyeji wetu. Yanga pia imesajili wengine. Hata hivyo, jambo zuri ni kwenye nafasi moja ukiwapambanisha wachezaji wanaojua maana yake una uhakika wa mmoja akiumia kuna mbadala. Hivyo kikosi kinakuwa imara,” anasema na kuongeza;

“Kabla sijajiunga na Yanga, nilikuwa napenda muunganiko wa viungo licha ya wengine kuondoka, ila waliopo bado wanafanya vizuri na naamini wote tupo kwa ajili ya kutimiza malengo ya klabu,” alisema na kukiri mkwanja mnene katika soka ameupata kupitia Yanga.

“Siwezi kusema nimepewa kiasi gani, ila ndio mara yangu ya kwanza kuchukua pesa ndefu tangu niaanze kucheza soka. Nitazifanyia mambo ya maana na nitakapokamilisha ndio nitaweka wazi,” anasema.

ELIMU

Anasema taaluma yake nje na soka amesomea mambo ya kiutalawa katika chuo cha Serikali za Mtaa, hivyo anaweza akafanya kazi ya utendaji, ila kwa sasa amejikita na soka.

“Kama nisingekuwa na kipaji cha soka, basi taaluma yangu nimesomea mambo ya utawala, hata ikija kutokea nikastaafu huko mbeleni, basi nitaweza kuifanya kazi niliyoisomea,” anasema.

SAFARI YAKE LIGI KUU

Huu ni msimu wake wa tatu kucheza ligi ya VPL, Lipuli ya Iringa alicheza misimu miwili, Kagera Sugar mmoja na sasa katua Yanga, ndani ya muda huo anaeleza hajawahi kupata kadi nyekundu.

“Nimeanzia mchangani, nikacheza timu za daraja la tatu sla pili, siwezi kuzimaliza zote kuzitaja, sikukata tamaa kwani niliamini nina uwezo mpaka leo hii nimefanikiwa kutua Yanga,” anasema.