Failuna apiga hesabu kali mashindano ya dunia

Muktasari:

Msimu uliopita Failuna alifuzu kushiriki mashindano ya dunia ambako alichuana katika mbio za mita 10,000 lakini hakufanya vizuri sanjari na Sarah Ramadhan akimaliza wa 56 katika marathoni na Magdalena Shauri akiishia njia huku Simbu akishinda medali ya shaba.

Dar es Salaam.Mwanariadha nyota wa kike nchini, Failuna Abdi ameanza kupiga hesabu ya kutwaa ubingwa wa dunia msimu huu mjini Doha, Qatar.

Failuna ni mwanariadha pekee wa kike nchini aliyefuzu kushiriki mashindano ya mwaka huu ambapo atachuana katika mbio za marathoni (kilomita 42) Septemba 27.

Katika mbio hizo, bingwa mtetezi ni Rose Chelimo raia wa Bahraini mwenye asili ya Kenya ambaye alitwaa medali ya dhahabu akikimbia kwa saa 2:27:11 ikiwa ni sekunde 44 mbele ya muda anaokimbia Failuna wa 2:27:55 aliouweka nchini Ujerumani.

"Najua ugumu wa mashindano ya dunia, lakini naamini Mungu atakuwa upande wangu," alisema Failuna ambaye ataondoka nchini Septemba 23 sanjari na rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka ambaye atakwenda kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Kimataifa (IAAF) sanjari na uchaguzi mkuu ambao rais anayemaliza muda wake, Sebastian Coe anatetea nafasi yake.

Alisema amejiandaa vizuri na amefanya mazoezi kuhakikisha anpunguza zaidi muda wake ili aweze kushinda medali katika mbio hizo zinazoshindanisha wanariadha nyota wa dunia.

Wanariadha, Alphonce Simbu, Agostino Sulle, Stephano Huche na Ezekiel Ngimba pia wamefuzu upande wa wanaume huku mmoja kati ya Huche au Ngimba akitakiwa kuondolewa kutokana na kanuni za IAAF ambazo haziruhusu wanariadha zaidi ya watatu kutoka nchi moja kuchuana katika mbio ya aiana moja.