Ishu ya Mukoko kumbe ipo hivi

JANA kwenye sehemu ya kwanza, Mukoko Tonombe, staa mpya wa Yanga alizungumzia mambo kibao ikiwemo jinsi alivyopania kulipa kisasi watakapokutana na Simba, Oktoba 18.
Lakini pia aligusia kwamba awali alijua angetua Msimbazi kuichezea Simba, lakini wakala wake akamwambia kuwa dili limebadilika na Yanga wamepanda dau hivyo atatua Jangwani.
Fuatilia mahojiano yake maalumu na Mwanaspoti upate mengi aliyonayo.
KINACHOMPA CHANGAMOTO
Mukoko anakiri kitu kinachompa changamoto ni tatizo la lugha kwa sasa hapa nchini.
Anasema lugha anayoitumia ni Kilingala, huku Tanzania lugha inayotumika ikiwa ni Kiswahili na kwamba, afadhali angekuwa anajua Kingereza anaamini angeweza kurahisisha mawasiliano yake mengi hapa Bongo.
“Mimi ni mcheshi, napenda kila mchezaji ama mtu anayenizunguka awe na furaha, lakini kwa hapa Tanzania najikuta kwenye changamoto ya lugha kwani siwezi kuongea Kiswahili ingawa najifunza kwa bidii, angalau wachezaji wenzangu niweze kwenda nao sawa,” anasema Tonombe, mchezaji huyo wa zamani wa AS Vita ya DR Congo.
“Napenda utani, utani wa hapa na pale baada ya kumaliza mazoezi ama mechi, lakini lugha inanikwamisha ingawa wakati mwingine nawafuata na kuzungumza nao hivyohivyo, watacheka nitacheka siku zinaenda,” anasema.
MGUU WA KUSHOTO
Mchezaji huyo anasema anapokuwa uwanjani anapenda kucheza kwa kutumia mguu wa kushoto ambao anauelezea ndio hatari zaidi kuleta madhara kwa timu pinzani, na anakuwa na uwezo wa kumiliki mpira vizuri zaidi.
“Japokuwa naweza nikacheza kwa miguu yote miwili inapobidi kama tu vile ambavyo ninaweza nikacheza namba nyingine nje ya ile sita niliyozoea, basi nachezea mguu wa kushoto ilimradi tu timu ipate matokeo,” anasema Tonombe ambaye alikuja Yanga na mwenzake Tuisila Kisinda.
ANATAKA KUFUNGA
Tonombe ameshafunga mabao manne Ligi Kuu Bara - moja akifunga kwenye ligi na katika mechi za kirafiki ana mabao matatu. Jamaa anafichua kwamba suala la kufunga kwake wala sio kitu kipya na akipata nafasi ya kujaribu anajua kufunga na sasa anataka kuwa bora kati ya wafungaji watano wa juu dhamira ambayo aliiweka tangu alipotoka kwao DR Congo.
“Dhamira yangu kubwa niwe kwenye orodha ya wafungaji watano bora, natamani hata kuwa mfungaji bora, shida ni nafasi ninayocheza lakini uwezo wa kufunga kwangu ni mkubwa tu, hilo linawezekana kwa kutoa jasho, sina vitu vingi vya kunifanya nisilifanye hilo.
“Kadri muda unavyokwenda ndivyo ninavyozidi kuizoea ligi ya Tanzania, hivyo ninaamini nitafunga mabao ninayoyataka na Yanga ifurahie kunisajili.”
SHIKHALO AMFUNDISHA
Anasema anapenda kukaa karibu na golikipa wa Yanga, Mkenya Farouk Shikhalo kwa sababu anamfundisha Kiswahili, ambapo anaweza akasalimia “mambo” au kuitikia “poa” akisalimiwa.
“Nawapenda wachezaji wote, lakini najikuta nipo karibu zaidi na Shikhalo ambaye ananifundisha Kiswahili, pia anaongea kwa mbali Kilingala anapenda kujifunza,” anasema Tonombe.
“Hivyo naamini baada ya muda mfupi nitaweza kuzungumza kwa usahihi kabisa, ukiacha ukaribu wangu nimegundua ni mchezaji mzuri anayejua kujiheshimu, lakini zaidi ni kipa mzuri sana namuamini sana.
“Naamini hata wachezaji wengine watakuwa wanapenda stori na sisi lakini lugha ndio inafanya tusielewane, kwani sipendi ukimya utani ndio unafanya tuzipumzishe akili baada ya kazi kubwa tuliyoifanya uwanjani.”
STAILI YA KUSHANGILIA
Tonombe tangu atue Yanga amekuwa akiwaongoza wenzake staili mbili za kushangilia mabao, ambapo akifunga mwenzake huwachezesha muziki, lakini akifunga huwa na mtindo tofauti akiwaweka wenzake chini kisha huanza kusema nao, na hapa anaelezea:
“Wakati timu ya taifa ya Congo tunacheza michuano ya Chan, kuna timu ilitufunga halafu kuna mchezaji akawa anashangilia kwa staili hiyo ya kucheza muziki iliniuma sana, baadaye nikaona niige kwa kufanya kazi kwa bidii ili nikifunga na mimi niwaudhi wapinzani wetu.
“Kuhusu ile ninayoitumia nikifunga mimi huwa napenda niongee na wenzangu wajue nasema nini, pale ninapowaambia wakae chini kisha mimi nasimama huwa napenda kuwaambia ‘jamani tulieni hili bao ni moja tu tunatakiwa kupambana zaidi kushinda mabao mengi lakini na mabeki nao tuhakikishe tunazuia kwa nguvu’, sasa najikuta nasema Kilingala bila wao kuelewa ila siku nikijua Kiswahili nitawaambia wanielewe.”
SIO MTU WA STAREHE
Tonombe anasema hana mambo mengi ya starehe, hanywi pombe, havuti bangi wala sigara bali anapenda sana kutumia muda wake kumpumzika.
“Mimi sio mtu wa starehe kabisa kwanza sinywi pombe, sivuti sigara kama nikipumzika huwa napenda kucheza gemu nikiwa kwangu nimetulia au nitaangalia mpira au kulala kabisa, wakati mwingine nitasikiliza muziki kidogo, hayo ndio maisha yangu ya siku zote hakuna kinachoweza kunibadilisha hapo.”
MKEWE KUMBE MWANDISHI BUANA
Akizungumzia maisha yake ya familia na uhusiano, Tonombe anafichua kwamba ana mke mtarajiwa, Jose Kitoko na kitaaluma ni mwandishi wa habari, lakini ameshamuachisha kazi hiyo na atamuoa Jumamosi ijayo Oktoba 10 akiwa hapahapa nchini.
“Mimi sio mtu wa tamaa za kubadilisha wanawake, sio kitu ninachopenda, kuna wakati mchezaji unaweza kujikuta unaporomosha uwezo wako kwa tabia kama hii,” anasema.
“Sijaoa, ila nitaoa Oktoba 10 kwa harusi ya kimila sitaweza kwenda (DR Congo), lakini familia yangu itaniwakilisha kule kumaliza kila kitu halafu nitampokea mke wangu na tutaanza maisha.
Mpenzi wangu anaitwa Jose Kitoko na ni mwandishi wa habari nampenda sana na naamini ananipenda mpaka tumekubaliana kila kitu katika maisha yetu nafikiri atakuja hapa na nitakaa naye hapahapa Tanzania.”
Tonombe anasema mchumba wake walikutana akiwa mchezaji naye akiwa kazini kama ofisa habari wa klabu moja huko DR Congo.
“Basi tukapendana nakumbuka ilikuwa ni mwaka 2017 baadaye tulipokubaliana nilimuomba aache hiyo kazi na akakubali na sasa nataka nianze naye maisha ingawa baadaye kuna kazi tofauti atakuja kuifanya, huyu ndio atakuja kuwa mama wa watoto wangu, sina mtoto na sikutaka kuanza kuwa na watoto kabla sijaingia katika ndoa.”
UKARIBU NA KISINDA
Mchezaji huyo anaonekana muda wote yupo karibu na mchezaji mwenzake, Tuisila Kisinda ambaye ametoka naye klabu moja.
Anasema urafiki wao ulianza toka DRC Congo na timu alizopitia kabla ya kujiunga na AS Vita, rafiki yake naye alipita hukohuko.
“Kwanza meneja wetu ni mmoja, kuna timu nilicheza naye kabla ya kucheza pamoja tena AS Vita, tupo wote Yanga, tunashauriana jinsi tunavyotakiwa tupambane kuhakikisha tunafika mbali kwenye mpira wa miguu, ndio maana mnaona na yeye mwenyewe ana juhudi,” anasema Mukoko.