Prime
Maswali saba mapya Dabi ya Kariakoo, hiki kitaikuta Yanga ikigoma

Muktasari:
- Ratiba hiyo imeanikwa saa kadhaa baada ya uongozi wa Yanga kutangaza kutokuwa tayari kucheza mchezo huo ambao awali ulikuwa ufanyike Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
WAKATI wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakicharuka Bungeni kuhusu Dabi ya Kariakoo, kuna maswali yanayohitaji majibu juu ya kile kinachoendelea baada ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) kupanga mechi ya marudiano ya Yanga na Simba iliyokwama Machi 8 itapigwa upya Juni 15, 2025.
Ratiba hiyo imeanikwa saa kadhaa baada ya uongozi wa Yanga kutangaza kutokuwa tayari kucheza mchezo huo ambao awali ulikuwa ufanyike Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mechi ya Machi 8 haikuchezwa baada ya kuahirishwa na Bodi kufuatia vurugu zilizojitokeza Kwa Mkapa siku moja kabla ya mchezo baada ya Simba kuzuiwa na waliotambulika kuwa ni makomandoo wa Yanga kufanya mazoezi uwanjani hapo.
Ratiba mpya iliyotolewa na Bodi imeonyesha kuwa mechi hiyo ya watani wa jadi itachezwa Juni 15, saa 11:00 jioni.
Mei 5, 2025 ambayo ni siku moja kabla ya kutolewa kwa ratiba hiyo, Yanga ilitangaza kuwa haitacheza mechi hiyo licha ya shauri ambalo ilifungua katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kurudishwa katika mamlaka za ndani ili lipitie utaratibu sahihi kabla ya kufikishwa huko Uswisi.

“Msimamo wa klabu yetu juu ya mchezo namba 184 wa Ligi Kuu Msimu huu uko pale pale kuwa hatutashiriki kwenye mchezo huo kwa namna yoyote ile,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilihitimisha kwa kuwataka wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa tayari kupambana kwa njia zote kuhakikisha haki inapatikana na kulaani kile walichokiita dhulma na uvunjwaji mkubwa wa kanuni unaofanywa na mamlaka za soka.
Yanga iliiomba CAS mechi ya marudiano ya Ligi Kuu baina yao na Simba isipangiwe tarehe na pia ipewe pointi za mezani, lakini barua ya CAS ya Mei mosi iliitaka Yanga irudi kufuata utaratibu, ambao awali klabu hiyo iliulalamikia kucheleweshwa.
NINI KITATOKEA?
Kufuatia Yanga kushikilia msimamo wa kutocheza mechi hiyo ya dabi, inaweza kuwa nafasi kubwa kwa Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, licha ya hivi sasa kuachwa pointi saba na vinara hao ambao pia ni watetezi wa ligi hiyo wakilishikilia kwa misimu mitatu mfululizo.
Yanga inabanwa na Kanuni ya 31 ya Ligi Kuu Bara Toleo la 2024 kifungu cha 1 (1.3) inayoelezea adhabu kwa timu itakayoshindwa kufika uwanjani itapokwa pointi 15.
Kwa sasa Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 70 baada ya kucheza mechi 26, ukiondoa mchezo huo wa Kariakoo Dabi, Yanga imebakiza mechi tatu kumaliza msimu huu. Katika mechi hizo tatu ikishinda zote, itafikisha pointi 79 lakini zikikatwa 15 zitabaki 64.
Simba ambayo ina pointi 63 katika mechi 24, ikipewa pointi tatu za mezani kutoka kwenye mchezo huo dhidi ya Yanga, itafikisha 66, huku mechi tano zitakazobaki ikishinda zote, itakusanya pointi 81 na kubeba ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo.
Lakini mgomo huo wa Yanga kuna hatari kwao kupoteza nafasi ya pili itakayowapa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao endapo itateleza katika mechi tatu zilizobaki kisha Azam ikafanya vizuri.
Azam kwa sasa inashika nafasi ya tatu na pointi 54, ina mechi tatu zimebaki ambazo ikishinda zote itamaliza ligi na pointi 63.
Yanga ikipokwa pointi 15 kwa kushindwa kucheza dhidi ya Simba, kisha katika mechi tatu zilizobaki ikapoteza moja tu, maana yake itamaliza ligi na pointi 61, ikiiacha Azam ikishika nafasi ya pili na hapo kupoteza nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika.

KANUNI HII HAPA
Kanuni ya 31 ya Ligi Kuu Bara Toleo la 2024, kipengele (1) kinasema: “Timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila ya sababu za msingi zinazokubalika kwa TFF/TPLB na/au kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu zifuatazo: 1.1 Kutozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000/-) ambapo shilingi milioni mbili na laki tano (2,500,000/-) itachukuliwa na Bodi ya Ligi Kuu na shilingi milioni mbili laki tano (2,500,000/-) italipwa kwa timu pinzani.
“1.2 Kulipa fidia ya maandalizi/uharibifu wowote unaoweza kujitokeza. 1.3 Kupokwa alama 15 (kumi na tano) katika msimamo wa Ligi na viongozi waliosababisha jambo hilo watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu. 1.3.1 Endapo timu itakuwa na alama pungufu ya 15, itakuwa na alama hasi kwa kiasi kinachopungua kwenye msimamo wa Ligi.
“1.3.2 Endapo timu itamaliza msimu wa Ligi ikiwa na alama hasi, itaanza na alama hizo hasi katika msimamo wa Ligi kwenye msimu unaofuata wa Ligi ya hadhi yake. 1.4 Itapoteza haki ya kuchukua gawio lake la mapato ya mchezo huo.
“1.5 Kiongozi yeyote atakayebainika kushiriki, alishawishi au alikuwa chanzo au sababu ya timu kutotokea uwanjani bila ya sababu za msingi atafungiwa kwa kipindi cha miezi kumi na miwili (12).
“1.6 Inaweza kukabiliwa na adhabu zaidi kama ambavyo TFF/TPLB itahitaji kuchukua hatua zaidi kadiri itavyoona inafaa. 1.7 Timu yoyote iliyopewa adhabu ya faini chini ya kanuni 31:1(1.1, 1.2 na 1.3) haitaruhusiwa kucheza hadi itakapotekeleza adhabu hiyo kwa daraja ambalo itakuwa ipo.”
ILIVYOKUWA
Machi 8, 2025 majira ya saa 7:52, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Bara (TPLB) ilitangaza kuahirisha mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya Yanga na Simba uliopangwa kuchezwa siku hiyo saa 1:15 usiku.
Kabla ya Bodi kutoa taarifa ya kuahirishwa kwa mchezo huo, tayari Simba ilitoa tamko la uamuzi wa kugomea kucheza ikidai imenyimwa haki ya kikanuni ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla.
TAMKO LA SIMBA
Taarifa iliyotolewa na Simba usiku wa Machi 8, 2025, ilifafanua kuwa uamuzi wa kugomea mechi umechukuliwa kwa vile kanuni zimekiukwa.
“Simba Sports Club imesikitishwa na vitendo visivyo vya kiungwana dhidi ya timu yetu kuelekea Mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Yanga, Simba ikiwa timu mgeni.
“Kwa mujibu wa Kanuni 17(45) ya Kanuni za Ligi Kuu Bara, Timu Mgeni ina haki ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Kwa makusudi Simba imenyimwa haki hiyo licha ya kufika uwanjani katika muda husika.

“Katika sintofahamu hiyo, Simba iliarifiwa na Meneja wa Uwanja kuwa hana maelekezo ya kuruhusu mazoezi kufanyika bila maelekezo ya kamishna wa mchezo. Pamoja na kamishna wa mchezo husika kufika, mabaunsa wa klabu ya Yanga walivamia msafara wa Simba huku wakiendelea na vurugu na wakizua msafara wa Simba kuingia uwanjani kufanya mazoezi.
“Jitihada za Simba kupata fumbuzi wa changamoto hiyo hazikuzaa matunda kwa zaidi ya masaa mawili kabla ya Simba kuondoka eneo la nje ya uwanja kwa sababu za kiusalama ambazo zimerekodiwa kwa ajili ya ushahidi.
“Kufuatia ukiukwaji huo wa Taratibu za Mchezo, Simba haitoshiriki mchezo husika na haki zote zimehifadhiwa. Simba inahimiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki dhidi ya wahusika wote wa sakata hili,” ilifafanua taarifa hiyo ya Simba.
Kanuni hiyo ya 17(45) inafafanua hivi: “Timu ngeni itafanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi angalau mara moja kabla ya siku ya mechi katika muda tarajiwa wa mchezo husika. Sababu zozote za kukwamisha timu mgeni kukidhi ipasavyo au kupata haki hii zitathibitishwa kwanza na kamishna wa mchezo.”
Simba ilienda uwanjani hapo saa 1 usiku muda ambao mchezo huo ulipangwa kuchezwa kwa ajili ya kufanya mazoezi, lakini ilizuiwa na wanaosemekana kuwa makomandoo wa Yanga na hivyo kulazimika kuondoka.
Wakati Simba ikitoa tamko hilo, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Crescentius Magori, alikazia kwa kusema: “Siyo mechi ya kesho (Machi 8, 2025) tu, hatuchezi ligi mpaka hawa walioshiriki kwenye huu upuuzi waadhibiwe.”
YANGA YAJIBU
Saa chache baada ya Simba kutoa taarifa ya kugomea mechi hiyo, uongozi wa Yanga ukajibu kwa kusema wangepeleka timu uwanjani na kweli walifanya hivyo.
Taarifa yao ya mapema kabla ya kuahirishwa kwa mchezo huo ilisema: “Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutaarifu Umma kuwa, mchezo wetu wa Ligi Kuu ya NBC, uliopangwa kuchezwa leo tarehe 8/3/2025, dhidi ya Simba SC, saa 1:15 usiku upo palepale na hakuna mabadiliko yoyote.
“Young Africans SC kama wenyeji wa mchezo, tunaamini taratibu zote za mchezo kama inavyoelekezwa kwenye kanuni za Ligi Kuu ya NBC, ziko sawa na maandalizi yote yako tayari.
“Uongozi wa Young Africans SC utapeleka timu uwanja wa Benjamin Mkapa kama inavyoelekezwa kwenye kanuni, na hatutakuwa tayari kucheza mchezo huu siku nyingine tofauti na leo.
“Tunawaalika uwanjani wanachama, mashabiki, wapenzi wa klabu yetu na wadau wengine waliosafiri kutoka mikoani, nchi za jirani na sehemu mbalimbali duniani kote kuja kushuhudia mchezo huu mkubwa barani Afrika.”

Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, aliandika hivi: “Nitakuwa wa mwisho kuamini kuwa kwa msimu wa 2024/25 Yanga SC itacheza mchezo mwingine wa Derby zaidi ya uliokuwa umepangwa tarehe 8/03/2025.”
Msafara wa kikosi cha Yanga uliwasili uwanjani hapo saa 10:30 jioni ukisindikizwa na ving’ora vya polisi, huku mashabiki wa timu hiyo waliokuwa ndani na nje ya uwanja walionekana kuwa na furaha kuwashangilia mastaa wao.
ILICHOSEMA BODI
Wakati hayo yote yakiendelea, taarifa ya Bodi ya Ligi ilisema imeahirisha mechi hiyo ili kupata fursa ya kuchunguza zaidi undani wa tukio hilo.
“Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha leo (jana) Machi 8, 2025 ilipitia shauri la klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC) uliopanga kufanyika kwenye uwanja huo leo (jana) kuanzia saa 1:15 usiku.
“Katika shauri hilo, klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajwa hapo juu, huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
“Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo (ambao walishuhudia tukio hilo), kutuma taarifa ya tukio haraka ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa, ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi. Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwamo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, Kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba, wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu, haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo, timu mwenyeji wala mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika uwanja huo ili maandalizi ya kikanuni yafanyike.
“Katika taarifa hizo, Kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa klabu ya Yanga, walishiriki tukio la kuzuia basi la klabu ya Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
“Kwa sababu pia Bodi ilipokea taarifa ya Ofisa Usalama wa mchezo ambayo imeainisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi, na kwamba baadhi ya matukio yanahitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati, Bodi ya Ligi kupitia Kamati yake ya Undeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1 (1.3) ya Ligi Kuu kuhusu Kuahirisha Mchezo, ili kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya uamuzi wa haki. Bodi itatoa taarifa kamili,” ilisema TPLB.

Ikiwa itabainika maofisa wa usalama wa Yanga walihusika kuizuia Simba kufanya mazoezi, kanuni ya 47 (1) inafafanua adhabu ambayo inaweza kupata.
“Klabu ina wajibu na jukumu la kuhakikisha kuwa wachezaji, viongozi, wanachama na wapenzi wake wanajiheshimu na hawajihusishi na vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu kama vile matusi, vitisho, vurugu, vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina na vitendo vyovyote vingine visivyokuwa vya kimichezo kwenye viwanja vya michezo. “Klabu ambayo mashabiki/wachezaji/viongozi wake watafanya vitendo hivyo itatozwa faini ya Sh5 milioni na kwa makosa ya kujirudia, faini itatozwa kati ya Sh10 milioni na Sh20 milioni,” inafafanua kanuni hiyo.
MASWALI SABA
1. Waliozuia Simba isifanye mazoezi wamechukuliwa hatua gani baada ya taarifa ya Bodi kubainisha walitambuliwa kwa sura, kwanini haijatangazwa kokote kilichoendelea baada ya hapo?
2. Simba ilitoa taarifa isingecheza mechi yoyote ya ligi hadi waliohusika na tukio hilo waadhibiwe, nini kimetokea hadi kuifanya ikacheza dhidi ya Dodoma Jiji, Mashujaa na JKT Tanzania?
3. Nini kitajiri endapo Yanga ikiendelea kushikilia msimamo wa kutocheza Kariakoo Dabi ijayo, huku ikidai haina imani na wasimamizi wa ligi kwa ujumla?
4. Kikao cha Waziri Kabudi alichofanya na viongozi wa Simba, Yanga, Bodi ya Ligi na TFF kilikuwa na muafaka gani wakati ratiba ya mechi imepangwa kabla ya majibu ya kikao hicho hayajatoka?
5. Uchunguzi juu ya viashiria vya rushwa na usalama, vitu vilivyotajwa kuchangia dabi kuahirishwa Machi 8, umefikia wapi, na je, Bodi imejihakikishia havitakuwapo tena katika mechi ijayo?
6. Wale wafanyabiashara walioingia hasara kutokana na dabi ya kwanza kuahirishwa, wameshafidiwa?
7. Gharama za mchezo ujao zitabebwa na nani, Yanga kama wenyeji, TFF au Bodi walioahirisha awali?