Dante aonywa, hukumu leo

Muktasari:

Mwanaspoti ilipenyezewa kwamba uongozi wa Yanga ulimwandikia barua ya onyo, Dante ikimtaka asisaini mkataba na klabu yoyote kwa kuwa bado ni mali yao, huku wakipambana kulimaliza sakata hilo salama.

ILE filamu ya beki Andrew Vincent ‘Dante’ dhidi ya klabu yake ya Yanga inaendelea, huku beki huyo akionywa na mabosi wake wa Jangwani lakini leo Alhamisi Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji itakata mzizi wa fitina baada ya ukimya wa muda mrefu.

Si mnajua baada ya kesi kufika katika kamati hiyo, uongozi wa Yanga uliomba kumlipa Dante kiasi cha Sh 10 Milioni kila mwezi, ili kumaliza deni lake la zaidi ya Sh 50 milioni, lakini waligomewa na upande wa mchezaji na kufanya kesi hiyo kuendelea kuwepo katika kamati hiyo ya TFF.

Baada ya kutoafikiana upande wa mchezaji kupitia kwa Mwanasheria wake, Alfred Mtawa suala hilo alilirejesha katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji na leo imepangwa kusikilizwa na kutolewa maamuzi, huku ikielezwa mapema Yanga walimpa onyo Dante kwa kutosaini kokote.

Mwanaspoti ilipenyezewa kwamba uongozi wa Yanga ulimwandikia barua ya onyo, Dante ikimtaka asisaini mkataba na klabu yoyote kwa kuwa bado ni mali yao, huku wakipambana kulimaliza sakata hilo salama.

Mwanaspoti lilimsaka Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama wa Klabu ya Yanga, Simon Patrick na kusisitiza bado wanaamini Dante ni mali yao hata kama hajajiunga kambini tangu msimu huu uanze.

“Dante ni mchezaji wetu, lakini hakuamua kufuata taratibu ambazo tulimuomba azifuate, pia hakufuata mkataba wake unavyosema ili aweze kumaliza suala lake,” alisema Patrick.

Aliongeza kwa kusema kwamba barua ya kumuonya kutokusaini timu yoyote waliiandika kutokana na bado yupo katika mkataba.

Naye Mwanasheria wa Dante, Alfred Mtawa alipoulizwa juu ya msimamo wa Yanga, alisema asingeweza kuongea chochote kwani kwa sasa wanasubiri maamuzi ya kamati ya TFF.

“Kesho (leo) kamati (leo) itakaa na wao ndio watatupa mwanga, tunasubiri kwa sasa siwezi kusema lolote, tusubiri hiyo kesho (leo),” alisema.