Suala la malipo; Yanga yamwacha njia panda Dante

Muktasari:

Wachezaji wengine ambao walikaa pembeni na kudai pesa zao za usajili ni Kelvin Yondani na Juma Abdul, lakini wawili hawa walirejea katika kambi ya timu hiyo.

Dar es Salaam. Kaimu Katibu Mkuu na Afisa habari wa Yanga, Dismas Ten ameweka wazi madai ya mchezaji Andrew Vincent ‘Dante’ anayedai Sh40 milioni.

Beki Dante anadai fedha za malimbikizo yake ya usajili baada ya kuongeza mkataba mpya wa kuitumikia klabu hiyo msimu uliopita.

Dismas alisema mchezaji huyo anapaswa kufuata taratibu za klabu hiyo kwani sio yeye tu ambaye anadai, bali wapo wachezaji wenzake wanaodai na wamefuata utaratibu.

Ten ameongeza kwa kusema uongozi wa klabu hiyo bado unaendelea kushughulikia suala hilo la kuwalipa wachezaji wote.

“Hatuwezi kuzungumza kupitia mtu mmoja mmoja ni mchezaji wetu na si yeye peke yake anayedai, wachezaji wengi wanadai, taratibu zao zinaendelea kushughulikiwa,” alisema.

Hata hivyo Mwanaspoti linafahamu mchezaji huyo alishawaandikia Uongozi wa Yanga barua na kuliacha suala lake kwa Mwanasheria wake lakini bado kumekuwa na ukimya wa kutatua jambo hilo.

Wachezaji wengine ambao walikaa pembeni na kudai pesa zao za usajili ni Kelvin Yondani na Juma Abdul, lakini wawili hawa walirejea katika kambi ya timu hiyo.

Awali ikumbukwe mchezaji Beno Kakolanya naye aliwahi kukumbana na mkasa kama huu baada ya kuidai Yanga pesa zake, lakini mchezaji huyo alijikuta akikaa nje bila kupata pesa hizo mpaka anasajiliwa na Simba.