Dante afunguka sababu za kutoonekana Yanga

Muktasari:
Awali, Eymael alinukuliwa na gazeti hili akisema kumekuwa na mfululizo wa matukio ya nidhamu kwa wachezaji wake kuhudhuria mazoezi na hata kuchagua baadhi ya mechi hasa za mikoani kwa sababu ya viwanja
SAA chache tangu Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael kusema kuwa nyota wa timu hiyo wamekuwa na nidhamu mbovu na kuanika kwamba beki wake wa kati, Andrew Vincent ‘Dante’ ametoweka klabu kwa zaidi ya wiki mbili, beki huyo amefunguka na kutoa sababu ya kutojiunga na Yanga mazoezini akidai imetokana na kumaliza mkataba wake, kukosa namba na alitoa udhuru kwa kocha huyo.
Awali, Eymael alinukuliwa na gazeti hili akisema kumekuwa na mfululizo wa matukio ya nidhamu kwa wachezaji wake kuhudhuria mazoezi na hata kuchagua baadhi ya mechi hasa za mikoani kwa sababu ya viwanja, lakini Dante akizungumza na Mwanaspoti alisema kabla ya kuamua kukaa nyumbani, alitoa udhuru kwa kocha wake kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia na akaruhusiwa kwenda kuyashugulikia.
Dante aliendelea kueleza kuwa baada ya kumaliza matatizo yake zilibakia mechi nne, zilizomfanya ajitafakari nafasi yake ya kucheza alipogundua hayupo katika mpango wa kocha, akaamua kufanya mazoezi binafsi ili kuendelea kulinda kipaji chake.
“Tangu nirejee kikosini baada ya mgogoro uliokuwepo baina yangu na viongozi nimecheza kama dakika 30 tu dhidi ya Simba ambapo niliingia kipindi cha pili, sasa katika mechi hizo nne ningefanya nini?” Alihoji beki huyo aliyesajiliwa misimu mitatu iliyopita kutoka Mtibwa Sugar na kuongeza;
“Ukiachana na hilo sikuwa kwenye mpango wa kocha sasa nashangaa anaposema nakosa nidhamu kutofika mazoezini, sijui nifanyaje hapo, ili nidhamu yangu ionekane.”
Ukiachana na hilo Dante alisema mkataba wake umemalizika ndani ya kikosi hicho na hakuna kiongozi ambaye amemfuata ili kuzungumza naye, hivyo akaona bora aendelee na kupambana na mazoezi binafsi.
“Natamani mtu ajaribu kukivaa kiatu changu ndio atanielewa namaanisha nini ila kwa sasa naacha yaendelee kuzungumzwa yanayozungumzwa,” alisema Dante.
Kocha wa Yanga aliiambia Mwanaspoti hivi karibuni kwamba mchezaji huyo hatakuwa kwenye kikosi hicho msimu ujao kwavile mkataba wake unamalizika na hajaonyesha kiwango kizuri, tangu aliporejeshwa baada ya mgogoro wake wa kususia kambi enzi za Kocha Mwinyi Zahera, ili kushinikiza alipwe fedha zake za usajili na malimbikizo ya mishahara.
Kesi hiyo ya Yanga na Dante ilitolewa uamuzi ya Kamati ya TFF na pande mbili kuafikiana na beki huyo kujiunga na timu, lakini hajaaminika chini ya Eymael wakati Ligi Kuu ikimalizika Jumapili ya wiki hii.