Barbara: Chama Yanga? thubutuu

MTENDAJI Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amekiri hawajamalizana na staa wao, Clatous Chama kuhusu mkataba mpya lakini akasisitiza Mzambia huyo hawezi kucheza Yanga ng’o.

Barbara ambaye ni kiongozi wa kwanza mwanamke msomi kushikilia nafasi ya juu klabuni, alisema wanapambana kumalizana na mchezaji huyo muda si mrefu na wana malengo naye.

Aliwahakikishia wapenzi wa Simba nchini, kutulia na kuwa na amani na suala la Chama na uongozi wao ni makini kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kulingana na heshima na thamani ya klabu hiyo.

Alisisitiza kabla ya Chama kuanza kusaini kwenye mkataba mpya bado ni mali yao kwa sababu hajamaliza ule wa kwanza, pia mazungumzo yao na staa huyo yapo vizuri ingawa hawajafika mwisho.

“Simba ni brandi kubwa ambayo inajua ifanye nini kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa na wapenzi wake hawajuti kuishabikia, hilo suala la Chama tumekaa naye mezani na mazungumzo yanakwenda sawa ingawa bado hatujafika mwisho, ila habari njema kwao ni siku za usoni watapata majibu yao,” alisema Barbara maarufu kama Boss Lady.

VIPI CHAMA KWENDA YANGA?

Barbara alijibu Simba ni klabu kubwa kuliko hao Wanajangwani na Chama hawezi kwenda kwa namna yoyote ile kwa vile anaelewa anavyonufaika na Simba na wao hawako tayari kumwachia.

“Unapoizungumzia Simba kwa sasa ni klabu kubwa hapa nchini, huwezi kulinganisha brandi yake na Yanga, narudia tena Chama hawezi kwenda Yanga kwa namna yoyote ile, hivyo kama mashabiki wao walikuwa wanalisubiria hilo kwa hamu wajiandae kiakili kuendelea kumwona anavaa uzi mwekundu,” alisema.

Alifafanua habari za Chama kuhusishwa na Yanga wanazo, ila wanazipuuzia kulingana na nyakati zenyewe kuwa za usajili na vinaweza kuibuka vitu mbalimbali ili kukuza mambo.

“Hiki ni kipindi cha usajili, kinaweza kuongelewa chochote na kwa mchezaji yoyote, ila sisi tunajua nini tunafanya, tunataka kulifikisha wapi soka la Tanzania kwa kuwa mfano dhidi ya timu nyingine,” alisema.

“Tunafanya vitu kwa usahihi, kuhakikisha tunaendelea kulinda brandi yetu,” alisema na kuongeza kila kitu kipo kwenye mpangilio na kitafanyika kwa umakini mkubwa.

Alisema katika muda ambao Chama amekaa ndani ya Simba amefurahia maisha na amenufaika na mambo mengi ndio maana katika mazungumzo yao wana uhakika tu atamwaga wino.

HERSI ANASEMAJE?

Hersi Said ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ushindi Yanga, aliliambia Mwanaspoti kama wanamhitaji mchezaji huyo watafuata taratibu kwa vile wanatambua bado ni mchezaji wa Simba na wana mkataba naye.

Lakini akaenda mbali zaidi kwa kusema hata thamani za mchezaji huyo wanazoziona zikitajwa kwenye mitandao ya kijamii siyo sahihi kulingana na aina ya mkataba wake ambao unamalizika Simba na uhalisia wake sokoni.

Alisema wako makini na kama kuna jambo lolote litafahamika.

CHAMA MWENYEWE

Mchezaji mwenyewe alizungumza na Mwanaspoti juzi jijini Dar es Salaam na kusisitiza Yanga wamempa ofa nono lakini Simba nao pia wanaendelea na mazungumzo naye.

“Mazungumzo na Simba yanaendelea vizuri lakini kuna vitu ambavyo nimewapa ambavyo ni vya kimasilahi, ninaipa kipaumbele Simba kama itatekeleza kile ambacho nimewaambia.

“Ikishindikana kabisa Simba nitaangalia Afrika Kusini au Arabuni kuna ofa nimezipata, lakini si timu nyingine ya hapa,” alisema Chama na kuongeza Yanga hawapi nafasi kubwa sana ingawa dau lao linavutia na akakiri ni kubwa kuliko la Simba.

Chama ambaye aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu uliopita, alikosekana katika mechi mbili msimu huu dhidi ya Prison na Ruvu Shooting ambazo timu yake ilichezea vichapo viwili mfululizo.

Baadhi ya mashabiki wa Simba wanaamini ishu ya Chama kwenda nje, inaweza kufanana na ile ya staa wao Mrundi Ramadhan Wasso aliyeondoka akaibukia Yanga kirahisi.

Chama alijiunga na Simba mwaka 2018, akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia alisaini mkataba wa mwaka mmoja na baadae aliongeza mwingine wa miaka miwili ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu.

Akiwa ndani ya Simba katika miaka ya hivi karibuni, amewaingiza kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Robo Fainali ya michuano hiyo mikubwa.

USIKOSE MAHOJIANO MAALUM YA CLATOUS CHAMA NA MWANASPOTI KESHO ALHAMISI NOVEMBA 12, 2020 KUJUA UNDANI WA SAKATA HILI..