Papy arudisha mamilioni ya Yanga, apelekwa Simba

Friday July 31 2020
papy pic

YANGA wamempa nahodha wao, Papy Tshishimbi hadi Jumatano afanye uamuzi kama anataka kuendelea kuwepo au vinginevyo aende zake kokote hata Simba.

Simba wamekuwa wakihusishwa na Tshishimbi kwenye miezi ya hivi karibuni ingawa habari za ndani zinadai kwamba baadhi ya viongozi wameshauri kuachana naye kwavile amekita mizizi ndani ya Yanga ambao huenda ikawaathiri baadaye kimkakati.

Lakini habari za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Tshishimbi amewarudishia Yanga dola 30,000 (Sh.69 milioni) walizompa kama gharama ya mkataba wa miaka miwili ingawa yeye amezigomea akitaka kuongezwa nyingine dola 20,000.

Katibu Mkuu wa Yanga, wakili Simon Patrick ameithibitishia Mwanaspoti kwamba kama watashindwa kufikia muafaka na Tshishimbi hadi Jumatano basi wataachana naye na hiyo inaweza kuwa nafasi kwa kiungo huyo kutua Simba au Azam ambazo zinatajwa kuwinda huduma yake.

Kauli ya Simon imekuja siku chache baada ya mchezaji huyo kutoafikiana na klabu hiyo juu ya usajili mpya kwenye dirisha kubwa baada ya kumaliza mkataba na klabu hiyo huku klabu ikitaka asaini miaka miwili na yeye akisisitiza kuwa dau walilompa ni la thamani yake kwa mwaka mmoja tu.

Habari zaidi zimelidokeza gazeti hili kuwa Yanga ilimpa mchezaji huyo dola elfu 30 kwa ajili ya usajili huo na baada ya kutoafiki ikamtaka azirudishe na tayari amezirudisha fedha hizo klabuni.

Advertisement

Ingawa Tshishimbi mwenyewe alipotafutwa jana hakutaka kuzungumzia lolote kuhusu usajili wake mpya, Katibu wa Yanga alidai kwamba bado klabu haijampa pesa mchezaji huyo.

“Tulichompa ni ofa yetu, ni kweli tumemtaka asaini miaka miwili, akikubali kusaini ndipo tutamuingizia fedha, lakini klabu bado hatujampa pesa yoyote,” alisema Simon bila kueleza kiasi cha fedha ambacho Yanga imemuwekea mezani mchezaji huyo akisisitiza hiyo ni siri ya klabu.

Alisema baada ya kumpa Tshishimbi ofa yao, klabu imempa mchezaji huyo siku 14 za kuamua kama atakubali kusaini mkataba mpya au la ili waangalie maisha mengine.

“Siku 14 zinakwisha Jumatano ijayo, bado tunamsubiri, kama zitakwisha na hajasaini maana yake hataki, hatuwezi kumlazimisha wakati mwenyewe hataki, hivyo ikifika Alhamisi ijayo tutaendelea na vitu vingine, tutaachana naye,” alisema.

Alisema kama atakubali kusaini miaka miwili kama ambavyo klabu imempa ofa hiyo, ndipo watamuingizia kwenye akaunti fedha yake ya usajili ambayo walishaizungumza.

“Tunachosubiri ni muda wa siku 14 umalizike, ukipita na hajasaini maana yake hajakubali hivyo hatuwezi kumlazimisha,” alisema.

Tathmini ya Mwanaspoti inaonyesha kuwa Yanga wamekomaa kushusha dau la Tshishimbi kwavile tayari wameshanasa saini ya mido wa AS Vita ya DR Congo, Mukoko Tonombe ambaye naye wachambuzi wanasema ni moto wa kuotea mbali kwenye nafasi zote za kati.

 

Advertisement