Jonas Mkude: Tulieni tu, mtaona wenyewe

KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude ameingiwa hofu kuwa wachezaji wanaweza kuumia pindi ligi itakaporejea kutokana mazoezi magumu ya binafsi waliyokuwa wakiyafanya hivyo, miili inakuwa haijafunguka vizuri.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mkude alisema wanapofanya mazoezi ya timu wanahitaji uangalifu kutoumia na ili kuandaa miili kuwa miyepesi kwa ajili ya kazi iliyombele yao.

“Ndio maana hata wakati msimu unaanza, makocha wanatoa programu tofauti hadi ligi inapoanza, yapo ya kujenga ufiti, stamina, mbinu na mengeneo

“Hatuwezi kucheza chini ya kiwango kwani, mapokeo ya ugonjwa wa covid 19 yalieleweka hivyo kila mchezaji alikuwa anajilinda kuhakikisha hatoki katika ari ya mchezo.

“Hatukujua hatma yetu ya kurejea uwanjani, iliongeza umakini wa kutozembea mazoezi ila changamoto ni pale ambapo kila mtu alikuwa anafanya mazoezi kivyake, sasa tunaingia kusaka nafasi ya kuingia kikosi cha kwanza,” alisema.

Kwa upande wake alisema licha yakujituma kufanya mazoezi bado anachukua tahadhari kubwa ili kujiepusha na majeraha.

“Binafsi nipo makini kujiepusha na majeraha, nafuata maelekezo ya kocha ili huduma yangu iwe msaada kuelekea kumaliza msimu na kutimiza lengo la kuchukua ubingwa kwa mara tatu mfululizo,” alisema.

Wakati Mkude anatazama uwezekano wa kutokea majeruhi, straika wa Kagera Sugar, Yusuf Mhilu amefichua kuwa kutengeneza kombinesheni ndio itakuwa tatizo.

Mhilu, ambaye ana mabao 11 alisema asilimia kubwa ya makocha watakuwa na kazi ya kuunda kombinesheni baada ya kila mchezaji kufanya mazoezi kivyake.

“Kuhusu ufiti tupo sawa kwa sababu hatukukaa bure, kila mchezaji alitafuta chaka la kufanya mazoezi hivyo katika hilo makocha hawatasumbuka, lakini kazi kubwa naiona kwenye kutengeneza kombinesheni. Timu bora ni ile yenye muunganiko mzuri kwa wachezaji iliona,” alisema.