Kiungo Ally Ng’anzi anacheza Marekani, akili yote ipo Lique1 Ufaransa

Muktasari:

Mpango wa kuja huku kwa mkopo ni kuendelea kutafuta njia ya kwenda Ufaransa, nahitaji kuendelea kukua kwenye soka la ushindani kabla ya kwenda kucheza Ligue 1.

Dar es Salaam. Kiungo wa timu Forward Madison, Ally Ng’anzi anayecheza kwa mkopo  Minnesota United FC, amesema hakuna matata kabisa Marekani ambako alitua Machi 5 akitokea Jamhuri ya Czech katika klabu ya MFK Vyskov.

Mambo yameanza kumnyookea Ng’anzi ambaye alizaliwa Septemba 3, 2000 mkoani Mwanza kwenye familia ya mzee Hamis na Bi. Mwajuma yenye watoto wanne.

Ng’anzi ambaye kiasili ni mtu wa Tanga aliyezaliwa na kukulia Mwanza, anasema pamoja na hali ya hewa nchini Marekani kuwa changamoto kwake anajisikia poa kuishi na Wamarekani.

“Nafanana nao najihisi kuwa Afrika hilo muda mwingi limekuwa likinipa faraja sina maana kuwa ningekuwa kwenye taifa lenye raia wengi wenye rangi tofauti na yangu ningesononeka hapa mimi ni mpambanaji.

“Nilianzia Czech ambako nilipambana na mwishowe nikapata nafasi ya kuja huku Marekani. Naishi nao vizuri na mapokezi yao kwangu yalikuwa mazuri, niliyafurahia.

“Mpango wa kuja huku kwa mkopo ni kuendelea kutafuta njia ya kwenda Ufaransa, nahitaji kuendelea kukua kwenye soka la ushindani kabla ya kwenda kucheza Ligue 1.

“Czech nilikuwa nacheza Ligi daraja la pili na huku timu ambayo nimejiunga nayo ni ya Ligi Kuu Marekani, Minnesota United FC nilikaa na kocha baada ya kujiunga na timu hiyo akaona nahitaji kupata kwanza muda mwingi wa kucheza madaraja ya chini kabla ya kuanza kunitumia.

“Kipindi hiki huku kuna baridi kali tofauti na Czech hivyo aliona mbali na kuimarika kutokana na muda ambao nitapata wa kucheza mara kwa mara pia itakuwa nafasi kwangu ya kuzoea maisha ya Marekani,” anasema.

Baada ya Ng’anzi kumaliza maongezi hayo na kocha wa Minnesota United FC, Adrian Heath pamoja na wawakilishi wake alitua Forward Madison ambayo ameanza kuichezea.

“Kocha akiona imetosha nitarejea Minnesota United FC kuanza patashika za kucheza Ligi Kuu Marekani, naamini ninauwezo wa kucheza MLS bila ya shida yoyote,” anasema kiungo huyo.

Akiyazungumzia maisha yake ya Jamhuri ya Czech yalivyokuwa Ng’anzi anasema hayana tofauti sana na Marekani, pindi akiwa huko alipelekwa kikosi cha vijana cha MFK Vyskov na baadae akaanza kutumika kwenye kikosi cha kwanza.

Kiungo huyo wa Kitanzania, anasema mchezo wake wa kwanza kuwa benchi ulikuwa dhidi ya Rymarov, Oktoba 20 mwaka jana ambapo hadi unamalizika ugenini hakupata nafasi ya kucheza.

“Tulifungwa mabao 2-1, mchezo wa pili pia sikupata nafasi ya kucheza safari hiyo tulishinda kwa mabao 2-1, mchezo wa tatu nao sikupata nafasi, lakini nashukuru mungu ilikuwa Novemba, 10 tukiwa nyumbani nilicheza kwa dakika 17 tu.

“Dakika zile zilitosha kocha kunikubali kwa sababu nilichokuwa nakifanya ni kuhakikisha natoa sapoti kwa mabeki wa kati pia nilikuwa nikiachia mipira kwa haraka, penye ulazima wa kukaa nao nilifanya hivyo na kupiga mashuti mawili,” anasema

Ng’anzi anasema waliibuka na ushindi wa mabao 4-1 na anadai kuwa alijisikia furaha na baada ya mchezo huo, yakafuata mapumziko marefu na aliporejea akatolewa kwa mkopo kwenda Marekani.

Kiungo huyo mwenye ndoto ya kucheza soka la kulipwa Ufaransa, anamalizia kwa kuwataka vijana wa timu ya taifa chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kutumia vema uwenyeji wa mashindano hayo ya Afcon U17 yatakayoanza kutimua vumbi nchini Aprili 14.

Wakati wa mataifa ya Afcon U17 nchini  Gabon, Ng’anzi anasema alipata Ulaji kutokana na kiwango chake kumvutia wakala wa Kikameroon, Alexandre Morfaw ambaye aliwahi kuzichezea klabu kadhaa kubwa barani Ulaya kama vile Leicester City na Nantes.

“Tatizo umri wangu ulikuwa chini ya miaka 17, ilikuwa ngumu kwangu kuchukuliwa, sikuelewa vizuri vipengele vyao lakini tuliendelea kuwasiliana kwa lengo la umri wangu ulisogea anisaidia kutimiza ndoto zangu,” anasema Ng’anzi na huo ndio ulikuwa mwanzo kwenye safari yake ya soka.

Morfaw ndiye mtu ambaye yupo nyuma ya kiungo huyo hivyo Ng’anzi anawasihi vijana hao kutochukulia poa mashindano hayo.