Prime
TFF na Bodi waitwa mahakamani Dar

Muktasari:
- Na wito wa kuitwa Mahakamani umetolewa leo Jumatatu, Juni 16,2025 na Jaji Butamo Phillip anayesikiliza shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
KUNA kitu kinaendelea Mahakamani kikilihusu Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) na Bodi yake ya Wadhamini.
Na wito wa kuitwa Mahakamani umetolewa leo Jumatatu, Juni 16,2025 na Jaji Butamo Phillip anayesikiliza shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Iko hivi; TFF, kupitia Bodi ya Wadhamini, wametakiwa kufika mahakamani Agosti 4, 2025 kwa ajili ya hukumu ya rufaa iliyokatiwa dhidi yake na Kocha Liston Katabazi.
Wito huo umetolewa leo Jumatatu, Juni 16,2025 na Jaji Butamo Phillip anayesikiliza rufaa hiyo, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Rufaa hiyo iliyosikilizwa kwa njia ya maandishi imetajwa leo kwa ajili ya kuangalia kama pande zote zimetekeleza amri za mahakama kuhusiana na uwasilishaji wa hoja za rufaa hiyo na kisha kupanga tarehe ya hukumu.
Wakati rufaa hiyo inatajwa TFF haikuwepo, yaani si ofisa wake yeyote wala wakili wao, huku Kocha Katabazi akihudhuria mwenyewe binafsi pamoja na Wakili wake, Rozalia Rutagwela.
Jaji Phillip baada ya kujiridhisha kuwa tayari pande zote zimeshawasilisha hoja zake za maandishi kuhusiana na rufaa hiyo, amepanga kutoa hukumu Agosti 4, saa 2:30 asubuhi.
Hivyo Jaji Phillip ameelekeza wajibu rufaa hao, TFF, wapelekewe hati ya wito wa kufika mahakamani (summons), siku hiyo kusikiliza hukumu hiyo.
Katika rufaa hiyo Katabazi anapinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, Kisutu, iliyotupilia kesi yake aliyokuwa anapinga uamuzi wa Kamati ya Maadili ya TFF kumfungia maisha yake yote kujishughulisha na masuala ya soka.
Katabazi ambaye anajitambulisha kuwa ni mdau wa mchezo wa soka na kocha wa mchezo huo mwenye Leseni Daraja C, iliyotolewa na TFF, alifungiwa na TFF kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi maisha yake yote, mwaka 2021.
Alifungiwa baada ya kuliandikia BMT barua Juni 15, 2021 akilishtaki TFF kuwa limeshindwa kusimamia mchezo huo kulingana na Sheria, Kanuni na miongozo yake.
Kufuatia barua hiyo, aliitwa katika Kamati ya Maadili, lakini hakuhudhuria badala yake alijibu kuwa yeye si mwanachama wa Chama cha Makocha Tanzania (Tafca) ambacho kiko chini ya usimamizi wa TFF, hivyo yeye si mwanachama wa TFF.
Juni 24, 2021 TFF ilichapisha katika tovuti yao uamuzi wa kumfungia Katabazi maisha kujishughulisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, mwaka 2024 alifungua kesi Mahakama ya Kisutu dhidi ya TFF na wadhamini wake akipinga uamuzi huo wa kufungiwa. Katika kesi hiyo ya madai namba 14708/2024, pamoja na mambo mengine alidai Kamati ya Maadili ya TFF haikuwa na mamlaka ya kutoa uamuzi huo dhidi yake kwa kuwa Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la Mwaka 2021, zilizotumika kumfungia si halali.
Alidai kuwa kanuni hizo hazijasajiliwa na BMT kwa mujibu wa matakwa ya Sheria namba 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake, na hivyo kuzifanya kuwa batili kutumika dhidi ya wanachama wake na mtu mwingine yeyote.
Katabazi alidai amri hiyo iliingilia haki yake ya kufanya kazi katika nyanja ya soka na hivyo kumkosesha fursa ya kupata mshahara na kipato kwa ajili ya kuendeleza maisha yake ya kila siku na familia yake, na kumsababishia maumivu ya kisaikolojia.
Hivyo aliiomba mahakama iiamuru TFF imlipe Sh 600 milioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata kutokana na uamuzi huo wa kumfungia maisha uliotolewa kwa makusudi, kimakosa na kwa nia ovu.
Pia aliomba alipwe Sh100 milioni kama fidia ya adhabu kwa kitendo cha wadaiwa kutoa uamuzi huo wakijua kuwa hawana mamlaka ya kisheria kuchukua hatua hiyo dhidi yake, riba ya kiwango cha Mahakama kwa cha tuzo (fedha ambazo ingeamuriwa alipwe) na gharama za kesi.
Vilevile aliiomba mahakama itoe zuio la matumizi ya Sheria (Katiba) na Kanuni za Maadili za TFF, kwa madai kuwa si vyombo halali kwa kutokusajiliwa kwa utaratibu na unaofaa.
Miongoni mwa vielelezo alivyoviwasilisha mahakamani ni barua ya BMT ya Juni 13, 2022 iliyothibitisha kuwa yeye si mwanachama wa TFF.
Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu iliitupilia mbali kesi hiyo, kufuatia pingamizi la awali lililoibuliwa na TFF.
Katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga ilikubaliana na sababu ya pingamizi la TFF kuwa haikuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
Hakimu Kiswaga alisema hakuna ubishi kwamba Katabazi ni mwanachama wa TFF.
Hivyo alikubaliana na wakili wa TFF, Rahim Shaban kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF, mwanachama asiyeridhika na uamuzi wa Kamati ya Maadili anapaswa kukata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya Maadili, lakini haukufuata utaratibu huo.
Hakimu Kiswaga alisema kuwa kwa Katiba ya TFF, TFF itakuwa na mamlaka kushughulikia migogoro yote ya soka ndani na mwanachama asiyeridhika, anaweza kupeleka shauri lake katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) baada ya kumaliza hatua zote ndani ya FFF.
Hivyo alisema mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani mlalamikaji, Katabazi alipaswa kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Maadili na kama asingeridhika angekata rufaa CAS kama Katiba ya TFF inavyoelekeza.
Katabazi pamoja na sababu nyingine, akidai Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria kushughulikia pingamizi la wajibu rufani ambalo halikuwa na msingi wa kisheria na kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa wakati wa usikilizwaji wa pingamizi.