Prime
Ishu ya Ibenge, Azam haitanii

MAPEMA bila ya kuchelewa, taarifa zinabainisha kwamba Azam FC imeanza mchakato wa kumpata mrithi wa Kocha Rachid Taoussi ambaye inaelezwa mwisho wa msimu huu anaondoka klabuni hapo.
Katika kumsaka mrithi wake mapema, uongozi wa Azam FC, tayari umekutana na kocha Florent Ibenge jijini Dar es Salaam kwa ajili kufanya mazungumzo ya kuhitaji huduma yake ya kukinoa kikosi chao msimu ujao.
Azam inahitaji huduma ya Ibenge ambaye anainoa klabu ya Al-Hilal ili kuja kuziba nafasi ya Taoussi anayemaliza mkataba wake wa mwaka mmoja baada ya kujiunga nao msimu huu.
Chanzo cha ndani kilisema: "Mazungumzo ya awali yamefanyika hapa Tanzania kati ya Ibenge na uongozi wa Azam, yapo mapendekezo ambayo kocha kayatoa yanayotakiwa kufanyiwa kazi na uongozi ambayo kwa sasa siwezi kuyaweka wazi.
"Azam ina malengo makubwa kwa msimu ujao hasa katika michuano ya kimataifa, ndiyo maana inahitaji kocha mwenye CV kubwa, inasajili wachezaji wazoefu ambao watafanya tufike mbali mmoja wapo akiwa kipa Aishi Manula."
Azam ni klabu ya tatu kuhusishwa na Ibenge ambapo tetesi za huduma yake kuhitajika zilianza kwa Simba na Yanga, hata hivyo hazikufanikisha kumpata kwa kile kilichoelezwa ni kocha ghali.
SAFARI YAKE YA UKOCHA NA MAFANIKIO
Ibengé alianza kazi ya ukocha nchini Ufaransa, alizinoa timu za ES Wasquehal na SC Douai, mwaka 2012 alipata fursa ya kuwa kocha wa klabu ya Shanghai Shenhua nchini China alikokaa kwa kipindi kifupi, kisha 2014 alirudi Afrika kuifundisha AS Vita Club ya DR Congo.
Mwaka huohuo, Ibengé aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya DR Congo (Leopards), akafanikiwa kuipa ubingwa wa mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN) mwaka 2016. Hata hivyo mwaka 2017 alijiuzulu kuwa kocha wa taifa na 2019 akarudi AS Vita.
Ndani ya AS Vita, Ibenge ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya DR Congo maarufu Linafoot katika msimu wa 2014–15, 2017–18 na 2020–21. Pia ametwaa ubingwa wa DR Congo Super Cup mwaka 2015.
Mwaka 2021, Ibengé alienda Morocco kujiunga na RS Berkane kama kocha mkuu ambapo akashinda taji la Moroccan Throne Cup msimu wa 2020–21 sambamba na Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021–22.
Mwaka 2022 alikwenda Sudan kuifundisha Al-Hilal akiisaidia timu hiyo kutwaa Kombe la Sudan kwa ushindi wa penalti dhidi ya Al Ahli Khartoum, lakini kazi yake iliingia dosari baada ya kuzuka kwa vita nchini Sudan mwaka 2023, hali iliyomlazimu timu hiyo kuhamia Cairo, Misri kuweka kambi.
Baadaye Al Hilal ikaenda kuweka makazi Mauritania na kushiriki Ligi Kuu nchini humo ambapo msimu huu imekuwa bingwa huku mkataba wa Ibenge kikosini hapo ukitarajiwa kumalizika Juni 30 mwaka huu.