Shiboub ndio basi tena Msimbazi

WAKATI straika Meddie Kagere ‘MK 14’ akiwa na wakati mgumu kwa sasa mbele ya Kocha Sven Vandanbroeck akikalishwa benchi katika mechi mfululizo licha ya kuwa kinara wa mabao, hatima ya kiungo fundi wa mpira Msudan Shiboub Sharafeldin ni kama saa zinahesabika Msimbazi.

Shiboub amerejea nchini wiki iliyopita baada ya kukwama kutokana na janga la corona, lakini sharti la kama anataka kuongezewa mkataba mpya klabuni hapo ni lazima afanye vyema kwenye mechi zilizobaki za timu zinatoa picha kiungo huyo nd’o basi tena.

Hatima ya kubaki katika kikosi hicho ipo katika mechi sita za Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho (FA) ambazo wamebaki nazo, lakini sintofahamu yake na Kocha Sven inatia shaka kama anaweza kutumika kwenye mechi hizo ili apewe mkataba mpya.

Habari kutoka ndani ya Simba zilizothibitishwa na mmoja wa viongozi ni kwamba, Shiboub alisaini mkataba wa mwaka mmoja unaomalizika mwisho wa msimu huu na ili asalie anatakiwa kufanya vizuri katika mechi zilizobaki za timu hiyo iliyotetea taji la Ligi Kuu mara ya tatu mfululizo.

“Unajua Shiboub mkataba wake umeshamalizika ila kilichopo wakati huu ni kuitumikia kutokana na kile kipengele cha (CAF) kuongeza mwezi mmoja wachezaji ambao mikataba yao inamalizika na hili limetokea kutokana na janga hili la virusi vya corona,” alisema kigogo huyo aliyekataa kutajwa jina.

“Tunachotaka ni kumuona akicheza mechi zilizobaki ili tuamue kumuongezea mkataba mpya wa mwaka mmoja, ila thamani haitakuwa kubwa kama ilivyokuwa pale awali.”

Shiboub aliyesajiliwa msimu huu akitokea El Hilal ya kwao Sudan, alisema amefurahi kuona uongozi wa Simba ukimtafutia njia ya kurudi Tanzania katika kituo chake cha kazi licha ya kukuta timu imeshatangaza ubingwa, na angependa kuonyesha kile alichonacho kama atapata nafasi ya kucheza. “Kikubwa ambacho naendelea kufanya wakati huu ni mazoezi na wenzangu, nikiwa na kiu ya kupata nafasi ya kucheza katika mechi chache zilizobaki, nikiamini zinatosha kuonyesha uwezo nilionao hadi mwisho kuipigania timu kabla ya mapumziko ya janga la virusi vya corona,” alisema Shiboub.

Kiungo wa zamani wa kimataifa aliyekipiga Simba na Yanga, Amri Kiemba alisema Shiboub katika mechi walizobakiza si sahihi kutaka kumuongezea mkataba kwa shinikizo. “Viongozi wakubali jamaa anajua soka na kama ni mkataba wampe bila shinikizo,” alisema Kiemba.