Kipa KenGold: Mpanzu? Tunajuana huko huko!

Muktasari:
- Mhagama ameliambia Mwanaspoti kwamba, anajua Simba itakuwa na uchu mkubwa wa kupata ushindi ili kujiweka pazuri katika mazingira ya kuunasa ubingwa wa msimu huu inaouwania na Yanga, lakini wachezaji wamejipanga kukabiliana na kina Ellie Mpanzu na Jean Ahoua ambao ndio wanaoonekana tishio kwa Wekundu.
KIPA wa KenGold, Castor Mhagama amesema mechi ya kesho ya kukamilisha ratiba ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba itakayopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora anatarajia itakuwa ngumu kwao kutokana na kutofanya maandalizi ya kutosha, lakini watapambana.
Mhagama ameliambia Mwanaspoti kwamba, anajua Simba itakuwa na uchu mkubwa wa kupata ushindi ili kujiweka pazuri katika mazingira ya kuunasa ubingwa wa msimu huu inaouwania na Yanga, lakini wachezaji wamejipanga kukabiliana na kina Ellie Mpanzu na Jean Ahoua ambao ndio wanaoonekana tishio kwa Wekundu.
Mhagama alisema kwa namna safu ya ushambuliaji ya Simba ilivyo na mabao mengi, anajua watakuwa na kazi ngumu ya kupambana nayo kuhakikisha wanashinda mchezo huo licha ya kushuka daraja.
“Hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu hatujafanya maandalizi ya kutosha na muda mwingi tulikuwa mapumziko ambayo mazoezi yake huwezi kuyafananisha na ya timu,” alisema Mhagama na kuongeza:
“Japo nasi tuna wachezaji wazoefu kama Zawadi Mauya, Kelvin Yondani, Bernard Morrison ambao wamecheza Simba na Yanga, lakini wenzetu walikuwa na maandalizi ya muda mrefu na morali zipo tofauti. Wao wanapambania ubingwa sisi kuonekana na timu nyingine za kuzichezea msimu ujao.”
Timu hiyo imecheza mechi 28, imeshinda tatu, sare saba, imekusanya 18 ikiwa na pointi 16 na iwapo itashinda mechi mbili zilizosalia dhidi ya Simba na Namungo itafikisha alama 22.
Rekodi zinaonyesha kwamba washambuliaji wa Simba, Jean Ahoua mabao ana mabao 15 na asisti nane katika mashindano hayo, huku Steven Mukwala na Leonel Ateba kila mmoja akiwa na mabao 12 ilhali Elie Mpanzu ana mabao matatu na asisti tano.
Kwa upande wa KenGold kuna Mashamo Daudi na Seleman Bwenzi ambao kila mmoja amefunga mabao matano.
Mbali na hilo, Mhagama alimtaja kipa wa JKT Tanzania, Yakoub Ali aliye na ‘clean sheet’ nane kwamba upande wake ndiye aliyemvutia zaidi kwa kazi aliyoifanya msimu huu.
KenGold imecheza msimu mmoja pekee katika Ligi Kuu Bara.