Nahimana, Berahino kumbe wana siri nzito

MSIMU mpya umeanza, lakini unaambiwa Ligi Kuu Bara ina kama makipa wanne tu waliodaka kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 zilizofanyika kule Misri na Algeria kunyakua taji kwa kuinyoosha Senegal katika mechi ya fainali.

Makipa walioenda katika fainali hizo ni Aishi Manula aliyeidakia Tanzania akiichezea Simba, Farouk Shikhalo wa Kenya aliyepo Yanga, Jonathan Nahimana wa Burundi anayeichezea KMC na Metacha Mnata wa Yanga naye alikuwa kikosi cha Taifa Stars.

Uwepo wa makipa hao walioshiriki fainali hizo za Afrika ni kuthibitisha kuwa Ligi Kuu sio ya mchezo na kama hujui ni kwamba Nahimana ndiye aliyekuwa kipa nam,ba moja wa Burundi, huku Manula na Mnata wakipokezana kudaka na Farouk hakudaka kabisa.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Nahimana na kufunguka mambo mengi ikiwamo siri yake na nyota wa Burundi aliyekuwa akikipiga England, Saido Berahino sambamba na ushiriki wake wa Afcon 2019.

LIGI YA BONGO YAMKOMAZA

Nahimana alisajiliwa na KMC msimu uliopita akitokea Vital’O ya Burundi wakati huo timu hiyo iliyotolewa Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa chini ya Kocha Etienne Ndayiragije.

Wakati anaingia alikutana na changamoto ya majeraha kabla ya baadaye kuanza kudaka mfululizo katika kikosi cha kwanza.

Kipa huyo alisema Ligi ya Bongo ina ushindani wa hali ya juu ambayo ilimfanya afanye mazoezi muda wote kuhakikisha anakuwa fiti.

“Mechi za mwanzo nilishindwa kucheza kwasababu nilipata majeraha, lakini ilibidi nizoee mazingira na kujituma muda wote kwasababu najua mpira wa hapa unalipa sana,” alisema.

SIRI YA KUDAKA MBELE YA KASEJA HII HAPA

Katika kikosi cha KMC kuna makipa ambao wote ni chaguo la kwanza hivi sasa katika timu zao za Taifa -- Juma Kaseja wa Tanzania na Nahimana wa Burundi.

Lakini katika msimu uliopita kilichokuwa kinatokea wawili hawa walikuwa wakicheza mwa kupeana nafasi mpaka wakaisadia timu kumaliza katika nafasi ya nne na kufuzu kucheza Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa ni msimu wao wa kwanza katika Ligi Kuu.

Nahimana anasema amekuwa mwanafunzi mbele ya Kaseja na amejikuta akipata vitu vingi zaidi.

“Kaseja ana uzoefu wa kutosha kwahiyo ninapokuwa nipo naye mazoezini nachukua baadhi ya vitu katika uchezaji wake nachanganya na vyangu.

“Unajua kuna baadhi ya wachezaji mpaka wakawa wanashangaa kwamba tumewezaje kuelewana mimi na Kaseja lakini ukweli mimi najifunza kupitia kwake.”

AWA BURUNDI ONE

Nahimana anasimulia baada ya kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha KMC ilimuwekea wepesi wa kwenda mbele zaidi na kupata nafasi katika timu ya Taifa.

“Nashukuru Mungu nimeweza kuingia katika historia ya Burundi, juhudi zangu na kumuamini Mungu vimenisaidia kutimiza moja ya ndoto zangu.”

Nahimana anasema baadaya kufanikiwa kucheza Afcon 2019 hivi sasa ameanza kupiga hesabu za kucheza Kombe la Dunia.

“Nimeshacheza mechi nyingi kubwa zote, ile imenipa hali ya kujiamini sana na kunifanya niwe mpaka kipa tegemeo, lakini yote hii ni kutokana na nafasi niliyopewa KMC.

WAKALA ACHELEWESHA DILI

Baada ya kucheza mechi za Afcon, wengi waliamini kwamba Nahimana alikuwa mbioni kuondoka KMC na kwenda kukipiga nje ya Tanzania.

Akizungumzia ishu ya kucheza soka nje ya Tanzania, Nahimana sura yake inabadilika na kuingia sura ya upole flani hivi kisha anafunguka kuwa wakala wake ndiye aliyemfanya aendelee kubaki katika kikosi cha KMC.

Dili la Nahimana kama lingekuwa chini ya wakala wa kimataifa Jorge Mendez au Mino Raiola, lingekuwa jepesi sana na hili ni kutokana na namna ambavyo anamiliki wachezaji wengi.

Nahimana anasema alikuwa na ofa nyingi kutoka Zambia, Angola na sehemu nyingine lakini wakala wake alikuwa anataka pesa nyingi kuliko kuangalia nafasi ya kucheza.

“Nilikuwa na dili Builcorn, Gor Mahia, Athletic De Agosto na Nkana, lakini hizo zote zilishindikana kutokana na wakala wangu kutaka pesa nyingi sana,” anasema.

Anaongeza, licha ya kushindwa kuondoka, aliamua kurejea KMC katika dakika za lala salama kutokana na maelewano mazuri ambayo yupo nayo.

“Unajua KMC mimi siku zote nimekuwa nikiishi nao vizuri, kwahiyo nilizungumza nao vizuri na kuweza kurejea kuendelea na maisha mengine, nina furaha kuwa hapa kwasababu nilishawahi kuwa hapa,” anasema.

BERAHINO NOMA

Saido Berahino aliwashtua watu wengi alipoamua kuachana na ofa ya kuchezea timu ya Taifa England na kuchagua kuchezea taifa lake la Burundi.

Berahino alicheza timu za taifa za vijana za England chini ya miaka U-16, U-17, U-18, U-19, U-20 na U-21, lakini baadaye alijiweka pembeni na kuamua kurudi zake Afrika.

Nahimana anasimulia kwamba mchezaji huyo yuko tofauti kabisa na watu walivyokuwa wanamchukulia kwamba pengine ana mapozi mengi na kujisikia.

“Berahino alivyokuja mazoezini alijikuta akishangazwa na viwango vyetu, nakumbuka alisema kabisa kwamba wachezaji wengi wanaocheza Ulaya wanakuwa na bahati tu,” alisema.

Anaongeza kwa namna ambavyo Berahino alikuwa anaishi, alikuwa kawaida kabisa na akiwaheshimu wachezaji wenzake.

APEWA GLOVES

NA BERAHINO

Nahimana anaendelea kusimulia namna gani ambavyo mshambuliaji Berahino amekuwa akiishi nao vizuri katika timu ya taifa Burundi, anasema amekua pia mtu wa kutoa zawadi pindi mchezaji anapofanya vizuri.

Kipa huyo alisema yeye pia ni mmojawapo wa watu ambao wamepokea zawadi kwa Berahino baada ya kufanya vizuri alipokuwa golini.

“Mimi katika mchezo dhidi ya Gabon niliweza kuwa Man of the Match (Mchezaji bora wa mechi), baada ya hapo aliniletea Gloves kitu ambacho sikutarajia,” alisema.