Yule aliyewaibua Saka, Nwaneri kusepa Arsenal
Muktasari:
- Mertesacker amekuwa meneja wa akademi ya Arsenal tangu mwaka 2018, baada ya kustaafu soka mwaka huo huo.
LONDON, ENGLAND: MKUU wa akademi ya Arsenal, Per Mertesacker, ameripotiwa kuwa na mpango wa kuondoka kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Mertesacker amekuwa meneja wa akademi ya Arsenal tangu mwaka 2018, baada ya kustaafu soka mwaka huo huo.
Beki wa kati huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 41 ameibua idadi kubwa ya vipaji vya akademi katika kipindi chake cha uongozi.
Nyota kama Bukayo Saka, Ethan Nwaneri, Max Dowman na Myles Lewis-Skelly wote walicheza mechi zao za kwanza timu ya wakubwa wakati Mertesacker alipokuwa akiongoza akademi ya Arsenal.
Mjerumani huyo ataondoka Arsenal majira ya kiangazi akiwa kwenye mahusiano mazuri na klabu, na ameashiria kuwa anatafuta nafasi ya juu zaidi katika uongozi wa soka. Mertesacker aliwahi kutajwa kama mrithi anayeweza kuchukua nafasi ya Edu alipong’atuka kama mkurugenzi wa michezo wa Arsenal, Novemba 2024.
Hata hivyo, Arsenal iliamua kumteua Andrea Berta, Machi mwaka jana. Na Mertesacker amesema: “Arsenal daima itakuwa klabu ya kipekee sana kwangu, hivyo huu ulikuwa uamuzi mgumu. Nashukuru sana kwa imani ambayo klabu ilinipa nilipobadilika kutoka kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza moja kwa moja hadi kuwa mkuu wa akademi. Sasa ni wakati wa mimi kusonga mbele, kujaribu jambo jipya na kujisukuma zaidi.
Nitaendelea kujikita kumaliza msimu kwa nguvu, kuendelea kukuza na kuendeleza vipaji vyetu chipukizi na kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko laini hadi siku yangu ya mwisho kwenye klabu.”
Mertesacker atapewa sifa kubwa kwa kusaidia kukuza vipaji vya vijana Arsenal. Lakini, Arsenal imekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika ngazi za vijana.
Ilimaliza nafasi ya 33 katika Ligi ya Vijana ya UEFA msimu huu baada ya kushinda mechi moja tu kati ya sita walizocheza.
Arsenal inapitia mabadiliko makubwa katika akademi yao, hasa katika mfumo wa kuajiri na kusajili vipaji vipya. Klabu imeanzisha mpango mkubwa wa usajili wa vijana ili kushindana na vinara wa akademi kama Chelsea na Manchester City.