Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilio cha Jamal Bakhressa ni king’ora hatari

ZENGWE Pict


MWAKA 2013, Azam ilinyimwa haki ya kutwaa ubingwa wa soka wa Bara baada ya Kamati ya Mashindano kukiuka kanuni za Ligi Kuu kwa kuamuru mchezo wao na Mtibwa Sugar urudiwe baada ya kuvunjika kutokana na watu wa Morogoro kukataa penalti.


Kwa wakati huo, adhabu ya timu kugomea mchezo ilikuwa ni kushushwa madaraja mawili, adhabu iliyowekwa baada ya kukithiri kwa vitendo vya kugomea mechi na timu kutokwenda uwanjani kutimiza majukumu yao.


Kwa hiyo, Kamati ya Mashindano haikuwa na hata kazi ngumu ya kuamua shauri lililokuwa wazi. Kwamba Mtibwa Sugar walitoka uwanjani kugomea penalti na hivyo aliyesalia alikuwa Azam FC ambaye alistahili kupewa ushindi na mabao matatu.

Lakini ilikuwa ajabu kwamba wajumbe wa kamati hii walishindwa kufanya uamuzi wa haki uliokuwa wazi kabisa wa kuipa ushindi Azam na kuishusha Mtibwa Sugar hadi daraja la pili. Mjumbe mmoja kutoka Mtibwa Sugar alishauriwa ama atoke kikaoni au asishiriki katika mjadala wa kamati hiyo.

Aliamua kutotoka kikaoni na uamuzi ukawa kuipa Azam ushindi na kuishusha Mtibwa. Wakati wa kusubiri kumaliza kikao mwakilishi wa sekretarieti ya TFF akatoka kwa dharura kikaoni, mara hoja ikaendelea na yule mjumbe wa Mtibwa Sugar akashiriki.

Mwakilishi wa sekretarieti ya TFF aliporudi kikaoni akakuta ule uamuzi wa kuipa ushindi Azam na kuishusha Mtibwa umebadilishwa na badala yake kamati ikaamua ‘eti’ mchezo urudiwe.

Ulikuwa ni uamuzi uliokwenda kinyume kabisa na kanuni za ligi uliofanywa na wajumbe hao, huku mwakilishi wa Mtibwa akisema kuwa alizidiwa nguvu na wajumbe wanaoishabikia Simba. Alidai kuwa wajumbe hao waliona kuwa kuishusha Mtibwa kungeigharimu Simba pointi sita ilizopata dhidi ya timu hiyo ya Morogoro, lakini kwao suala la Azam kuwa ingenufaika na kutwaa ubingwa halikuwa jambo muhimu.

Ni kitu kibaya sana kwamba baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo leo wapo TFF na Bodi ya Ligi wakati ambao mmiliki wa Azam FC, Jamal Bakhressa ameamua kujitokeza na kutoa nyongo yake kuhusu uendeshaji na usimamizi wa ligi.

Jamal kutoka familia ya Said Salim Bakhresa inayomiliki kampuni ya habari ya Azam, anasema uongozi wa TFF na Bodi ya Ligi umepoteza dira, hautendi haki na unaendesha mchezo huo kwa kutaka timu fulani itwae ubingwa.

Jamal anasema kulikuwa na viongozi makini huko nyuma, lakini anaona sasa hakuna uongozi unaojali maendeleo ya mpira bali kutaka matamanio yao yatimie.

Kauli yake, ambayo si ya kawaida kutoka upande wa kampuni ya Azam na familia kwa ujumla, imetoka siku moja baada ya timu hiyo ya Chamazi kupoteza mchezo wa fainali ya Kombe la CRDB kwa bao 1-0 dhidi ya Simba, huku kukiwa na matukio yanayoweza kuwa yaliamua mchezo baada ya kutokea utata.

Ilikuwa kama ni dhambi kwa Azam kupewa haki yao katika baadhi ya matukio, hasa yale makubwa yanayoweza kuamua mchezo. Matukio kama ya uwezekano wa penati lililosababisha mshambuliaji wa Azam, Jephte Kitambala Bola kuonyeshwa kadi ya njano kwa madai kuwa alijirusha wakati picha za marudio zinaonyesha mguu wa Kitambala ulizuiwa kusogea na hivyo kusababisha aanguke.

Hakuna haja ya kurudia matukio yanayolalamikiwa kuwa yalikuwa na uamuzi mbovu. Cha muhimu ni hatua ambayo Jamal ameamua kuichukua baada ya kelele za muda mrefu kuhusu uamuzi mbovu ambazo hazishughulikiwi na badala yake walengwa wanakuwa wale wanaolalamika.

Mwaka jana, ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe alitozwa faini ya Sh miliomni 10 kwa kuziambia mamlaka zifanyie kazi mijadala iliyozagaa ya uamuzi mbovu. Adhabu hiyo ilitolewa lakini mamlaka hazikuwajibika kwa kile ilichoombwa ikishughulikie.

Badala yake kuwajibika kumekuwa ni kufungia waamuzi mizunguko mitatu hadi mitano halafu wanarejea uwanjani kurudia makosa yaleyale. Jamal anasema jambo hilo haliwezi kuondoa matatizo ya uamuzi kwa kuwa imekuwa ni kama mazoea kwamba mwamuzi akosee, afungiwee na halafu arejee tena kuchezesha.

TFF wala Bodi ya Ligi haichukui hatua zozote kuonyesha kuwa inawajibika kwa matatizo ya uamuzi zaidi ya kugungia waamuzi na wanaowalalamikia. Hakuna ubunifu wa jinsi ya kushughulikia matatizo hayo makubwa katika moja ya nguzo nne za mpira wa miguu.

Jamal anasema wadau wanaoingia kwenye mpira kwa kumiliki timu, wanakutana na matatizo ya uendeshaji na usimamizi na baadaye wanaondoka. Wa mwisho alikuwa Alexander Mnyeti na klabu yake ya Gwambina ambaye amesema yuko tayari kutumia uwanja wake kama malisho ya mifugo badala ya mpira wa miguu. Akaondoka na Gwambina yake.

Pia klabu ya Arusha FC iliamua kujiondoa kwenye ligi ikipingana na uamuzi mbovu. Pamoja na uongozi kutangaza kujiondoa, mamlaka zilihakikisha wachezaji wa timu hiyo wanahudhuria mechi zote ili kuepuka kuathiri matokeo ya timu walizotaka zifanye vizuri kama Arusha FC ingeshushwa daraja na kufuta pointi zote ilizotwaa au kupoteza.

Kauli ya Jamal ni king’ora cha pili cha kuashiria hatari iliyopo mbele. Waandishi na wachambuzi wameshajadili sana kuzitaka mamlaka zione soka linakoelekea na kuchukua hatua mapema, lakini king’ora hicho cha kwanza cha hatari kimepuuzwa.

King’ora hiki cha Jamal ni cha msisitizo kuwa hatari ni kubwa zaidi mbele na hatua zisipochukuliwa, hali inaweza kufikia pabaya. Jamal anasema yuko tayari kuihamishia Azam FC Zanzibar. Tutamnyamazia kama tulivyofanywa kwa Mnyeti?

Hatua hiyo ya kuhamishia timu Zanzibar itakuwa na maana gani kwa kampuni ya Azam Media iliyo na haki za matangazo ya ligi za juu nchini? Na kama Azam Media itachukua hatua zitakuwa ni zipi. Ni dhahiri hazitakuwa za kujiondoa kutangaza ligi, lakini zinaweza kuwa ngumu sana.

Ni muhimu kuchukua hatua mapema.