Prime
Siri ya ajabu nyuma ya ushindi! Barker, Fei Toto watajwa
HATIMAYE Simba imehitimisha mateso ya miaka minne ya kukaa bila ya taji lolote kubwa baada ya mwishoni mwa wiki kutwaa bingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB kwa kuichapa Azam FC kwa bao 1-0, katika mchezo wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Wakati Simba ikipitia mateso hayo ya miaka minne, Yanga ilikuwa ikifurahia mafanikio ikibeba mataji ya Ligi Kuu ya NBC na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Msimu huu, watani hao wa jadi wamegawana mataji hayo. Yanga imebeba Ligi Kuu ya NBC, Simba ikichukua Kombe la Shirikisho la CRDB. Kilichobaki sasa Simba kubeba taji la Ligi Kuu ya NBC, mtihani ilionao msimu ujao.
Haikuwa rahisi kwa Simba kupata ushindi huo kwani ililazimika kusubiri kwa dakika 62 kupata bao hilo pekee ambalo nalo lilitokana na Azam wenyewe kujifunga kupitia kiungo wake Yahya Zayd.
Katika misimu 11 tangu kurejea kwa mashindano hayo 2015-2016, Simba sasa imebeba taji hilo mara nne, wakati Yanga ikiongoza kwa kuchukua mara tano. Azam na Mtibwa mara moja moja.
FAINALI ILIYOPOOZA
Mbinu nyingi za makocha pamoja na tahadhari ya kiuchezaji katika dakika zote ilifanya mchezo huo ulipoteza mvuto machoni mwa watazamaji uwanjani.
Azam ndio iliyokaa nyuma zaidi na mpango wao kufanikiwa kwani ilikuwa inajua wazi kwamba kama ingetoa nafasi kwa viungo wa Simba kucheza kwa uhuru ingepata madhara makubwa.
Mpango huo ukampa wakati mgumu zaidi mshambuliaji wa Azam, Jephte Kitambala, ambaye muda mrefu akajikuta anakabiliana na mabeki wawili wa Simba, huku akikosa msaada kutokana na wenzake kuwa nyuma.
DAKIKA 45 BILA SHUTI LA MAANA
Mpango huo ukaifanya mechi hiyo kukosa ufanisi ambapo timu zote zikaonyesha udhaifu kwa kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza bila kupiga shuti lililolenga lango huku mashuti mengi yakitoka nje.
FEI TOTO KAZINGUA
Azam ililazimika kucheza pungufu kwa dakika zaidi ya dakika 30 kutokana na kiungo wake Feisal Salum 'Fei Toto' kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja baada ya kuonekana kumpiga ngumi Libasse Gueye wa Simba na mwamuzi Sifuni Amoni kutoka Mbeya kumpa adhabu hiyo.
Ukiangalia picha za marudio utamsifu Amoni kwa uamuzi huo ulikuwa sahihi kwani Fei Toto hakuwa na sababu ya kufanya hivyo hatua ambayo iliibebesha mzigo wa pili Azam kwa kucheza pungufu wakati ambao ilikuwa inapambana na mzigo wa kwanza wa kuruhusu bao.
Fei Toto ni kama aliipulizia sumu Azam kwa kadi hiyo ambapo ilikuja wakati ambao ilikuwa inapambana kurudisha heshima yao na kuwarudisha nyakati za kucheza pungufu.
AMONI FRESH LAKINI BADO
Mwamuzi Amoni alifanikiwa kuimaliza mechi salama lakini kuna maeneo alikuwa ameshindwa kufanya kwa mkazo uliostahili.
Matukio mawili ya awali kabisa wakati Kitambala anakabiliana na mabeki wa Simba yalistahili kuwanufaisha Azam lakini bahati mbaya haikuwa hivyo, Amoni aliipa faida Simba huku Mkongomani huyo akionyeshwa kadi ya njano.
Simba nayo ikakosa haki yake kwa Amoni kupitia tukio la Himid Mao kumchezea vibaya Gueye dakika ya 33, mwamuzi huyo hakumpa kadi kiungo huyo mkongwe.
Simba tena ikanyimwa nafasi nzuri ya kukamilisha shambulizi lake dakika ya 78, Amoni aliona ni kama kiungo wa Azam alichezewa vibaya, wakati Elie Mpanzu anakwenda kufanya kitu kumalizia nafasi nzuri.
BARKER AKILI NYINGI
Kocha wa Simba, Steve Barker aliishinda mechi kwa uamuzi wake ambapo baada ya kupata bao akamtoa beki wa kushoto Nickson Kibabage, ambaye alikuwa mzuri wa kupandisha mashambulizi, nafasi yake ikachukuliwa Antony Mligo aliyekuwa mzuri wa kujilinda zaidi.
Hapa Barker alikuwa anawapa wakati mgumu Azam, wakati inatafuta bao la kusawazisha, kocha huyo pia akamtoa Clatous Chama nafasi yake ikachukuliwa na Alassane Kante ambaye alikuja kuongeza idadi kwenye eneo la kiungo cha ulinzi.
Mabadiliko hayo mawili yakaifanya Azam kuzidi kupata ugumu wakati inajenga mashambulizi yake kuelekea lango la Simba lakini idadi ya wachezaji wa ulinzi kwenye ukuta wa Wekundu hao ukawa ni shida.
Sasa Simba imeshinda fainali zote nne za mashindano hayo yaliyorejea msimu wa 2015-2016 ikizifunga Mbao mabao 2-1 (2016-2017), Namungo 2-1 (2019-2020), Yanga 1-0 (2020-2021) na Azam 1-0 (2025-2026).
Azam yenyewe katika fainali tano ilizocheza, imeshinda moja pekee msimu wa 2018-2019 ilipoifunga Lipuli bao 1-0. Fainali nne ilizopoteza tatu ni dhidi ya Yanga (2015-2016, 2022-2023 na 2023-2024), kisha mbele ya Simba (2025-2026).