Yamal kufungwa kitanzi Camp Nou

BARCELONA, HISPANIA. KIUNGO wa Barcelona, Lamine Yamal, anatazamiwa kuzuia nia za timu za Ligi Kuu ya England kwa ajili yake kwa kusaini mkataba mpya wenye kipengele chenye masharti makubwa.
Kinda huyo machachari mwenye umri wa miaka 15 ndiye mwanasoka mwenye umri mdogo zaidi kuichezea Barcelona, baada ya kuingia akitokea benchi katika ushindi wao waliopata Aprili mwaka huu dhidi ya Real Betis.
Yamal pia aliweka rekodi kuwa mfungaji bora kinda zaidi wa timu ya taifa ya Hispania kuwahi kufunga alipofiisha umri wa miaka 16, alipofunga katika ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Georgia katika mechi ya kimataifa.
Kuongezeka kwa kasi kwa kijana huyo kulimfanya aingie kwenye orodha fupi ya timu kadhaa za Ligi Kuu England ambazo zinawania saini yake ikiwemo Manchester City.
kwa mujibu wa taarifa Yamal yuko tayari kuongeza mkataba mrefu na Barcelona kwa mujibu wa mkali wa masuala ya usajili Fabrizio Romano. Inaaminika kwamba kinda huyo atasaini mkataba mrefu na kifungu cha kipendele chenye thamani ya Pauni Bilioni 1.
Xavi Hernandez ana nia ya kuhakikisha kuwa Yamal haendi popote kufuatia kiwango bora alichoonyesha katika mechi tisa alizocheza.
Licha ya umri wake mdogo Yamal anaweza kuwa na uwezo wa kumrithi Lionel Messi ambaye anakipiga Inter Miami kwa sasa.
Lakini yeye sio kinda wa kwanza kuandaliwa mkataba mrefu wenye thamani ya Bilioni 1 wapo makinda wengine kama Pedri, Gavi na Ansu Fati anyekipiga Brighton kwa mkopo.