Watanzania wawili kukiwasha Qatar

NYOTA wawili wenye asili ya Tanzania, Akram Afif na Yussuf Poulsen wamebeba matumaini ya mwenyeji (Qatar) na Denmark kwenye Fainali za Kombe Kombe la Dunia 2022 ambazo pazia lake linatarajiwa kufunguliwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa Al Bayt, Al Khor, Qatar.

Msimu uliopita wa Kombe la Dunia Russia 2018, Watanzania walimshuhudia mshambuliaji wa RB Leipzig ya Ujerumani, Poulsen akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Tanzania kufunga bao kwenye fainali hizo huku akiwa na taifa la upande wa mama yake, Denmark.

Safari hii, chuma kingine, Akram ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Simba, Hassan Afif kitakuwa kikisaka rekodi nyingine tamu kwenye fainali hizo ambazo zinafanyika kwa mara ya kwanza kwenye taifa la Kiarabu huku ikiwa ni mara ya pili kwa Bara la Asia.

Akiwa na wenyeji wa fainali hizo ambao ni Qatar, Akram atakuwa akisaka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Tanzania kufunga bao kwenye mchezo wa ufunguzi ambao watacheza dhidi ya Ecuador.

“Hisia ni nyingi, ilikuwa ni ndoto ambayo nilikuwa nikiiota kwa kipindi kirefu hatimaye inatimia, tutakuwa mbele ya mashabiki zetu, wakiimba na kutuunga mkono, hakika tuna kila sababu ya kuwapa furaha,” alisema.

Kocha wa Qatar, Felix Sanchez amemtwisha jukumu zito mshambuliaji huyo hatari huko Asia ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Ulaya akiwa na Villarreal ya Hispania; “Naamini tutafanya vizuri,” alisema wiki chache zilizopita kutokana na kijiti cha wenyeji wa michuano walichonacho.

Mbali na Akram mchezaji mwingine hatari kwenye kikosi cha Qatar ambaye anategemewa kwenye kikosi hicho ni pamoja na Almoez Ali.

Akram ambaye anaichezea Al Sadd aliwahi kumwagiwa sifa na kocha wake wa zamani, Xavi ambaye kwa sasa anainoa Barcelona kuwa ni mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa, msimu huo alitwaa tuzo ya mchezaji bora Asia.

Denmark ya Poulsen yenyewe itatupa karata yake ya kwanza kwenye fainali hizo, Novemba 22 kwa kucheza dhidi ya Tunisia.