Ronaldo, Mastaa wengine wamlilia Diogo Jota

Muktasari:
- Alijiunga na Liverpool kutoka Wolverhampton mwaka 2020 na kushinda makombe matatu makubwa akiwa na klabu hiyo ya Merseyside. Jota ameacha mke na watoto watatu.
Baada ya kutokea taarifa ya majonzi kufuatia kifo cha mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Ureno, Diogo Jota aliyeaga dunia akiwa na miaka 28 baada ya kupata ajali ya gari akiwa na mdogo wake, Andre Silva, nchini Hispania mastaa kibao wamemlilia.
Wakati taifa la Ureno na klabu ya Liverpool zikiomboleza msiba huo mzito, mastaa wa zamani na wa sasa wametuma salamu za rambirambi wakieleza kushtushwa kwao na kifo hicho cha ghafla cha mchezaji huyo.
Mshambuliaji wa Al-Nassr na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, ameandika kupitia mitandao ya kijamii baada ya kifo cha Diogo Jota na mdogo wake Andre Silva.
“Haiingii akilini. Hadi muda mfupi tu ulikuwa nasi kwenye timu ya taifa na hata ndoa yako ulikuwa umefunga hivi karibuni. Kwa familia yako, mkeo na watoto wako, natuma salamu za rambirambi na nawatakia nguvu kubwa mno katika kipindi hiki. Najua utakuwa nao daima. Pumzikeni kwa amani, Diogo na André. Tutawakosa sana.”
Mwanasoka wa zamani wa Manchester United na mchambuzi wa soka, Gary Neville, ameandika ujumbe mfupi unaosema:
“Hii ni habari ya kuhuzunisha sana. Mapenzi yangu kwa familia ya Diogo Jota.”
Naye beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher, ambaye pia ni mchambuzi wa soka nchini Uingereza, ameonekana kushikwa na majonzi akisema:
“Nimehuzunika sana. Mawazo yangu yako kwa mkewe Rute na watoto wao watatu.”
Mshambuliaji nguli wa zamani wa England, Alan Shearer, ameeleza mshtuko wake kwa maneno machache:
“Inasikitisha sana.”
Naye beki mkongwe wa Ureno, Pepe, ambaye alikuwa mchezaji mwenzake kwenye kikosi cha taifa, hakuficha uchungu wake akisema:
“Kupoteza mtu wa kipekee kama Jota ni pengo lisilozibika. Tulimpenda kama rafiki, mchezaji na binadamu.”
Kipa wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Hispania, David De Gea, naye amechapisha ujumbe wenye hisia nzito, akionyesha namna tukio hilo lilivyomgusa:
“Wakati mwingine maisha yanakuwa ya kikatili sana.”
Beki wa zamani wa Manchester United na England, Rio Ferdinand, ameeleza majonzi yake kwa kutumia maneno ya huzuni kubwa:
“Nimevunjika moyo. Mawazo yangu ni kwa familia ya Jota.”
Klabu ya Liverpool nayo imetoa taarifa rasmi ikisema: "Tuna huzuni kubwa kwa taarifa za kifo cha Diogo Jota. Tumepoteza siyo tu mchezaji wa kiwango cha juu, bali pia binadamu wa kipekee." Klabu hiyo imesisitiza kuwa itatoa msaada wote kwa familia ya marehemu.
Klabu ya zamani ya Jota, FC Porto, imetoa taarifa ya maombolezo, ikisema:
“Tunaomboleza. Tumepoteza mmoja wetu.”
Shirikisho la Soka la Ureno (FPF) kupitia kwa Rais wake, Pedro Proença, pia limethibitisha vifo hivyo na kueleza kuwa Ureno imepoteza mchezaji mahiri, mtu wa watu na kielelezo katika jamii. FPF pia imeomba dakika moja ya ukimya kabla ya mechi ya timu ya taifa ya wanawake dhidi ya Uhispania katika michuano ya Ulaya.
Ajali hiyo ilitokea kwenye barabara ya A-52, eneo la Cernadilla karibu na Zamora, kaskazini magharibi mwa Hispania, jirani na mpaka wa Ureno, gari aina ya Lamborghini aliyokuwa akiendesha Jota iliteleza, kupinduka na kulipuka moto, na kusababisha vifo vya Jota na mdogo wake, Andre Silva, mwenye umri wa miaka 26, ambaye naye ni mchezaji wa soka.
Shirika la dharura la Castilla y León lilithibitisha tukio hilo saa 12:35 asubuhi na kueleza kuwa walipokea simu kadhaa kuhusu ajali hiyo mbaya na kutuma vikosi vya uokoaji, lakini miili ya wawili hao ilikutwa ikiwa tayari imepoteza uhai.
Diogo Jota alikuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kilichotwaa taji la Ligi Kuu England msimu wa 2024/25, akifunga mabao sita katika mechi 26. Aidha, alikuwa mhimili katika kikosi cha timu ya taifa ya Ureno kilichotwaa UEFA Nations League mwezi uliopita kwa ushindi dhidi ya Hispania kwa mikwaju ya penalti.
Alijiunga na Liverpool kutoka Wolverhampton mwaka 2020 na kushinda makombe matatu makubwa akiwa na klabu hiyo ya Merseyside. Jota ameacha mke na watoto watatu.