Man United yaweka sokoni mastaa wote wa kikosi cha kwanza

Muktasari:
- Kipigo kwenye fainali ya Europa League kutoka kwa Tottenham kimeifanya Man United kuwa njiapanda kwenye ishu ya kuwa na pesa za kutosha ili kusajili dirisha lijalo.
MANCHESTER, ENGLAND: HABARI ndo hiyo. Manchester United imeripotiwa kuwaweka sokoni mastaa wake wote kwenye kikosi kwamba hakuna ambaye hauzwi kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kipigo kwenye fainali ya Europa League kutoka kwa Tottenham kimeifanya Man United kuwa njiapanda kwenye ishu ya kuwa na pesa za kutosha ili kusajili dirisha lijalo.
Mabosi wa klabu hiyo ya Old Trafford waliweka matumaini ya kukamatia Pauni 100 milioni kutokana na kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya endapo kama ingebeba taji la Europa League.
Lakini, kushindwa kufanya hivyo, njia pekee ya kupata pesa kwa sasa ni kuuza mastaa wake.
Wachezaji kama Bruno Fernandes, Casemiro, Kobbie Mainoo, Luke Shaw, Harry Maguire, Andre Onana na Alejandro Garnacho wote wanaweza kuwekwa sokoni dirisha hili.
Kulikuwa na wasiwasi pia kocha Ruben Amorim naye anaweza kufungasha virago vyake na kuondoka kwenye timu hiyo endapo kama tajiri Sir Jim Ratcliffe ataamua kumfuta kazi.
Na baada ya kipigo hicho kwenye fainali ya Europa League, nahodha wa kikosi hicho, Fernandes alijitoa ofa mwenyewe kuondoka Old Trafford, endapo kama itaamua kumpiga bei ili kupata pesa za kufanya usajili wa wachezaji wa kuja kuboresha kikosi. Msimu ujao utakuwa ni mara ya pili kwa Man United katika kipindi cha miaka 35 kushindwa kufuzu kucheza michuano yoyote ya Ulaya. Kwenye ishu ya usajili, Man United tayari imeshaweka ubaoni majina ya mastraika inaowasaka, ambao ni mkali wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres, yule wa RB Leipzig, Benjamin Sesko na straika wa Ipswich Town, Liam Delap.
Lakini, kushindwa kufuzu kucheza michuano yoyote ya Ulaya msimu ujao linamfanya kocha Amorim kuwa na wakati mgumu wa kupata wale wachezaji aliowataka na hilo linaweza kumfanya kuhamia kwenye mpango mbadala. Na mpango mbadala unaweza kuwa wa kuwasajili wachezaji Lorenzo Lucca, Mateo Retegui, Moise Kean na straika wa Crystal Palace, Jean-Philippe Mateta. Man United itahitaji kuwafungulia mlango wa kutokea jumla wachezaji waliokuwa nje kwa mkopo ili kupunguza bili ya mishahara na kuwa na salio la kutosha kufanya usajili wa wakali wapya.
Wachezaji hao waliokuwa kwa mkopo ni mawinga Marcus Rashford, Jadon Sancho na Antony, ambao watapaswa kurudi Old Trafford mwisho wa msimu huu wakitokea Aston Villa, Chelsea na Real Betis, mtawalia. Kinachoelezwa, kocha Amorim ataendelea na kazi yake Old Trafford.