Indiana Pacers mabingwa wa comeback NBA

Muktasari:
- Hicho ndicho kinachoifanya Indiana Pacers kuwa timu pekee katika historia ya NBA, hasa inapofikia hatua ya mtoano (playoffs).
NEWYORK, MAREKANI: KATIKA ulimwengu wa mpira wa kikapu ushindi mkubwa haupimwi tu kwa pointi zilizopatikana, lakini mara nyingi hutokana na moyo, uvumilivu na uwezo wa kurudi mchezoni licha ya kupigwa bao.
Hicho ndicho kinachoifanya Indiana Pacers kuwa timu pekee katika historia ya NBA, hasa inapofikia hatua ya mtoano (playoffs).
Katika msimu wa mtoano wa NBA 2025, Pacers imejijengea heshima kuwa timu ya comeback ikitoka nyuma dhidi ya wapinzani wakubwa kama Milwaukee Bucks, Cleveland Cavaliers na sasa New York Knicks kwenye fainali za Kanda ya Mashariki.
1. Game 1 dhidi ya New York Knicks (Fainali ya Mashariki 2025)
Katika mchezo wa kwanza wa fainali za Mashariki, Pacers walikuwa nyuma kwa alama 14 (116-102) zikiwa zimesalia dakika 3 na sekunde 25. Lakini kama ilivyo ada walirejea kwa kishindo. Aaron Nesmith alitua mfululizo three-pointers, Haliburton alifunga kwa ustadi dhidi ya Mitchell Robinson sekunde chache kabla ya muda kumalizika na kusawazisha 126-126.
Katika muda wa ziada (overtime), Pacers ilitawala na kuishangaza Knicks kwa ushindi wa 138-135, ushindi ambao umeongeza presha kwa Knicks.
2. Vs Cavaliers (nusu fainali Mashariki, Game 2)
Cleveland Cavaliers ilikuwa mbele kwa alama 14 hadi kipindi cha tatu na bado iliongoza 119-112 ikiwa na sekunde 57.
Hapo ndipo Indiana ilipoonyesha ujasiri wa kipekee na Nesmith alidaka mpira uliopotea na kufunga, Donovan Mitchell alikosea kwa faulo ya ajabu na Haliburton akamalizia kwa 3-pointer ya kusisimua na kubeba ushindi 120-119. Huo ulikuwa mwanzo wa anguko la Cavaliers kwenye msimu huu wa mtoano.
3. Vs Milwaukee Bucks (raundi ya kwanza, Game 5)
Bucks ilikuwa inakaribia kuisogeza hadi Game 6 ilipokuwa mbele kwa pointi 118-111 ikiwa na sekunde 40 tu kwenye overtime. Lakini Pacers ilifanya yake, Andrew Nembhard alitupia 3-pointer, akachukua tena mpira baada ya kuiba pasi na Haliburton kufunga. Hatimaye, Haliburton alimzunguka Giannis Antetokounmpo na kufunga kwa sekunde moja kabla ya filimbi ya mwisho, wakashinda kwa kishindo.
4. Vs New York Knicks (mwaka 2000, Game 6)
Katika mechi iliyokuwa ya kufuzu kwa fainali za NBA, Pacers ilikuwa nyuma mwanzoni mwa robo ya mwisho. Reggie Miller alifunga pointi 17 kati ya 34 katika robo hiyo na kuipeleka Pacers kwenye fainali za NBA kwa mara ya kwanza katika historia. Hiyo ilikuwa pia mechi ya mwisho kwa Patrick Ewing akiwa na Knicks.
5. Vs. Milwaukee Bucks (2000, Game 5)
Mchezo huo haukuwa comeback ya kustaajabisha kwa alama, lakini ulikuwa na mwisho wa kuvutia. Pacers ilikuwa nyuma kwa 94-93, lakini Travis Best alitupia 3-pointer muhimu sekunde 16 kabla ya mwisho na kuiwezesha kushinda. Ray Allen alikosa nafasi ya kuipa ushindi Bucks.
6. Vs. Chicago Bulls (1998, Game 4)
Reggie Miller tena akisukuma mashambulizi kwa ustadi dhidi ya Michael Jordan na kutupia 3-pointer sekunde 0.7 kabla ya mwisho, Pacers iliiwasawazishia Bulls 2-2 kwenye mfululizo wa michezo. Jordan alijibu kwa kuiongoza Chicago kushinda Game 7, lakini Indiana ilionyesha kuwa ilikuwa wapinzani wa kweli.
7. Vs. New York Knicks (1995, Game 1)
Hii ndiyo comeback ya kihistoria inayokumbukwa zaidi maarufu kama Eight Points in Nine Seconds. Reggie Miller alifunga pointi nane ndani ya sekunde 8.9 na kuifanya Pacers kuibuka na ushindi wa 107-105 baada ya kuwa nyuma kwa 105-99. Hilo limebaki kuwa tukio la kusisimua zaidi kwenye historia ya NBA playoff.
SIO POA
Pacers imejijengea sifa ya kuwa timu isiyokata tamaa. Katika miaka 30 ya mwisho iliyopita imeonyesha uwezo wa kupindua matokeo yasiyotarajiwa na kuwapa mashabiki wake sababu ya kuamini hadi sekunde ya mwisho lolote linawezekana. Msimu huu inaendelea kuandika historia kwa kurejea kwenye michezo ambayo wengi walihisi imepoteza. Kama msemo wa michezo unavyosema 'mpira ni dakika 90' na kwa Pacers kila sekunde inahesabika.