Wakanyaga pedeli tajiri zaidi muda wote duniani
Muktasari:
- Kama ilivyo katika ngumi, soka, kikapu na michezo mingine kwenye baiskeli kuna mastaa wanaotesa kwa kukanyaga pedeli ambao pia wanamiliki ukwasi wa maana waliouvuna kutokana na jasho wanalovuja katika uwanja wa mashindano ya mbio za baiskeli.
MILAN, ITALIA: KATIKA kila ulimwengu wa mchezo husika kuna wababe wake uwanjani ambao ndiyo walioukamata na majina yao hutajwa kwa mengi hasa namna wanaocheza. Lakini, kila mchezo una kipato chake.
Kama ilivyo katika ngumi, soka, kikapu na michezo mingine kwenye baiskeli kuna mastaa wanaotesa kwa kukanyaga pedeli ambao pia wanamiliki ukwasi wa maana waliouvuna kutokana na jasho wanalovuja katika uwanja wa mashindano ya mbio za baiskeli.
Mashindano ya baiskeli ya kulipwa duniani ni mchezo wenye malipo mazuri, ingawa zawadi zake hazifikii kiwango cha tenisi au gofu. Lakini, haijalishi waendesha baiskeli bora duniani wana utajiri unaofikia mamilioni ya dola, hususan wanaoshiriki mbio za Giro d’Italia, Tour de France na UCI Road World Championships zinazomalizika Septemba, 2025.
Mwaka 2024, zawadi za Giro d’Italia zilikuwa Euro 1.6 milioni zikigawanywa kwa washindi wote katika kipindi cha wiki tatu. Mshindi wa jumla alipata takriban Euro 265,000 ilhali aliyechukua nafasi ya pili akipata Euro 133,400 na nafasi ya tatu akaondoka na Euro 68,800.
Vivyo hivyo, Tour de France ilikuwa na zawadi ya Euro 2.31 milioni iliyogawanywa kati ya washindi wa hatua mbalimbali ikiwamo washindi wa jumla, waendesha baiskeli wa masafa mafupi, waendesha baiskeli bora wa kila hatua na mwendesha baiskeli aliyevunja rekodi bora zaidi.
Kwa kuzingatia zawadi hizo hawa hapa ni waendesha baiskeli tisa tajiri zaidi duniani kwa mujibu wa The Scotsman:
9. Mark Cavendish
Mwingereza huyo aliyestaafu kuendesha baiskeli anatajwa kuwa na utajiri wa Pauni 7.48 milioni. Mark Cavendish aliyejulikana kiutani kama Manx Missile anachukuliwa kuwa mwendesha baiskeli bora wa mwendo kasi katika mbio za umbali mfupi. Cavendish ndiye anayetajwa kuwa bora zaidi katika historia ya mchezo kwenye umbali mfupi wa mashindano. Mwaka jana aliweka rekodi ya ushindi wa haraka zaidi kwenye Tour de France.
8. Chris Froome
Chris Froome ni mwingereza mwingine katika mashindano ya baiskeli, lakini akiwa ni mshindi wa Grand Tours mara saba ikihusisha Tour de France mara nne, Vuelta a Espana mara mbili na Giro d’Italia moja. Utajiri wake unakadiriwa kuwa Pauni 8.98 milioni.
7. Alberto Contador
Huyu ni Mhispania na mmoja wa waendesha baiskeli bora zaidi wa kizazi chake. Amewahi kushinda Grand Tours zote tatu angalau mara moja na ni wa pili katika historia kushinda mashindano yote hayo makubwa mara mbili. Utajiri wake ni takriban Pauni 12.7 milioni.
6. Eddy Merckx
Eddy Merckx ni Mbelgiji anayechukuliwa kuwa mwendesha baiskeli aliyefanikiwa zaidi katika historia ya mchezo huo akiwa amebeba ubingwa wa Tours de France mara tano, Giros d’Italia mara tano, Vuelta moja, ubingwa wa dunia mara tatu na
Monuments yaani mbio tano kubwa zaidi za heshima na kihistoria kwenye kalenda ya mbio za siku moja. Haya ni mashindano yenye urefu mkubwa (karibu kilomita 250+). Utajiri wake unakadiriwa kuwa Pauni 14.98 milioni.
5. Jan Ullrich
Ullrich ni Mjerumani, bingwa wa zamani aliyekuwa katika kilele cha mafanikio mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa 2000. Alishinda dhahabu na fedha kwenye Olimpiki za Sydney 2000. Hata hivyo, mwaka 2012 alipatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli. Utajiri wake ni takribani Pauni 14.98 milioni.
4. Greg LeMond
Mmarekani huyu alishiriki mbio za dunia za baiskeli kati ya 1981 hadi 1994, akishinda Tour de France mara tatu na ubingwa wa dunia wa mbio za barabarani mara mbili. Alikuwa wa kwanza kusaini mkataba wa thamani ya Dola 1 milioni katika mchezo huu. Utajiri wake ni takriban Pauni 29.96 milioni.
3. George Hincapie
George Hincapie ni Mmarekani aliyeendesha baiskeli kati ya 1994 na 2012. Alishinda Tour de France mara 17 ikiwa ni rekodi ya pekee. Alikiri kutumia dawa za kusisimua misuli 2012 na akafutiwa matokeo ya mbio za 2004, 2005 na 2006.
Baadaye alikuwa mmiliki na meneja wa timu ya mbio za baiskeli, lakini ilivunjika 2020. Utajiri wake ni takribani Pauni 29.96 milioni.
2. Peter Sagan
Mslovakia huyo ni bingwa wa dunia mara tatu mfululizo na bingwa wa Ulaya mara moja. Utajiri wake unakadiriwa kuwa Pauni 37.45 milioni.
1. Lance Armstrong
Mwamba huyo Mmarekani aliwahi kushinda mataji saba ya Tour de France, lakini yote yalifutwa baada ya kugundulika kuwa sehemu ya njama ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu michezoni. Mwaka 2012, alipigwa marufuku kushiriki mbio na kupoteza wadhamini wakuu aliokuwa nao yaani Nike, Oakley, Trek na Anheuser Busch). Licha ya kashfa hiyo ana utajiri wa takriban Pauni 37.45. Wakati wa kilele chake katika mashindano ya baiskeli utajiri wake ulikadiriwa kufikia Pauni 100 milioni.