Prime
Belouizdad kumchomoa Kibu denis Libya
KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Kibu Denis, ameibuka kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na CR Belouizdad ya Algeria, kuelekea msimu wa 2026-2027, kufuatia kiwango anachoendelea kukionyesha akiwa na Al Nasr Benghazi ya Libya.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Algeria, kocha mkuu wa CR Belouizdad, Nabil Maaloul, ndiye anayesukuma kwa nguvu dili hilo baada ya kuvutiwa na kiwango cha Kibu tangu alipotua Al Nasr.
Kibu alijiunga na Al Nasr mwezi Januari 2026 akitokea Simba SC kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu. Tangu alipowasili, amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, akichangia mabao matano.
Katika kipindi chake cha miezi sita ya kwanza akiwa Al-Nasr, Kibu amefunga mabao mawili, huku pia akitoa pasi tatu za mabao.
Meneja wa Kibu Denis, Carlos Silvester maarufu kama Mastermind, amethibitisha kuwepo kwa mazungumzo ya uhamisho wa nyota huyo licha ya kwamba hakuweka wazi ni klabu gani inamuhitaji, lakini alieleza hatua ya kwanza ipo mikononi mwa klabu zinazohusika kabla ya mchezaji kuanza kujadiliana kuhusu maslahi binafsi.
“Kibu alikwenda kwa mwaka mmoja na nusu na anaendelea kufanya vizuri. Nakupa exclusive, kuna ofa zimewasilishwa Al-Nasr na kwa sasa klabu ndiyo inaendelea na mazungumzo. Wakifikia makubaliano, ndipo watatuita kwa ajili ya kujadili maslahi binafsi,” amesema Carlos.
Aliongeza kuwa, kuna uwezekano wa Kibu kubaki Al-Nasr kutokana na mkataba wake wa sasa uliobaki mwaka mmoja, lakini pia hakuficha uwezekano wa kuhamia katika klabu nyingine kubwa.
“Chochote kinaweza kutokea kati ya leo na Ijumaa. Anaweza akaendelea kucheza Al-Nasr kwa sababu bado ana mkataba, lakini pia msishangae kumuona akihamia nchi nyingine. Ni klabu kubwa kutoka nchi yenye ushi ndani mkubwa wa soka, hivyo bado tunasubiri mawasiliano rasmi kutoka klabuni,” alisisitiza.
Kabla ya kuhamia Libya, Kibu alikuwa mchezaji mwenye uhakika wa namba ndani ya kikosi cha Simba alichojiunga nacho msimu wa 2021-2022 akitokea Mbeya City. Kabla ya hapo, alikuwa akiitumikia Geita Gold.
Winga huyo anafahamika kwa uchezaji wake wa kasi, nguvu na uwezo wa kucheza katika nafasi mbalimbali za ushambuliaji, jambo lililomfanya kuwa mchezaji muhimu kwa makocha tofauti aliowahi kufanya nao kazi ndani ya Simba. Iwapo mazungumzo kati ya Al-Nasr na CR Belouizdad yatakamilika kwa mafanikio, kwa Kibu itakuwa mwendelezo wa safari yake ya soka la kimataifa, baada ya kuondoka Tanzania na kuthibitisha uwezo wake nchini Libya.
Uha misho huo unaweza kumpa nafasi ya kucheza tena mashindano ya CAF, huku akiendelea kuongeza thamani yake katika soko la usajili Afrika kwani hivi sasa kwa mujibu wa Transfermarket, thamani yake sokoni ni Euro 225,000 (Sh674.8 milioni).