Messi amwakia mwamuzi Pinheiro
Muktasari:
- Messi hakufunga bao katika mchezo huo, lakini alitoa pasi ya bao la mapema lililofungwa na Alexis Mac Allister ndani ya dakika 10 za mwanzo.
MIAMI, MAREKANI: NAHODHA wa Argentina, Lionel Messi, alinaswa akibishana kwa hasira na mwamuzi Joao Pinheiro wakati wa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Uswisi uliowapeleka mabingwa watetezi katika nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Messi hakufunga bao katika mchezo huo, lakini alitoa pasi ya bao la mapema lililofungwa na Alexis Mac Allister ndani ya dakika 10 za mwanzo.
Dakika chache kabla ya mapumziko, kamera zilimuonyesha staa huyo mwenye umri wa miaka 39 akizungumza kwa ukali na mwamuzi Pinheiro kufuatia maamuzi yaliyolalamikiwa na pande zote mbili.
‘’Ongea nami tafadhali ili uheshimiwe na wengi humu.’’ ni baadhi ya maneno ambayo aliyasema Messi
Mchezo huo uligeuka baada ya mshambuliaji wa Uswisi, Breel Embolo, kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia uamuzi wa VAR.
Mwanzoni mwamuzi alimpa kadi ya njano Leandro Paredes wa Argentina kwa kumchezea vibaya Embolo, lakini baada ya kupitia tukio hilo kwenye VAR ilibainika kuwa mshambuliaji huyo wa Uswisi alikuwa amejiangusha makusudi.
Kutokana na hilo, kadi ya Paredes ilifutwa huku Embolo akionyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje.
Baada ya Uswisi kubaki wachezaji 10, Argentina ilitawala mchezo na kufunga mabao mengine kupitia Julian Alvarez na Lautaro Martinez ili kuthibitisha nafasi yao ya kucheza nusu fainali.
Sasa Argentina itakutana na England katika pambano kubwa litakalochezwa Jumatano mjini Atlanta.
Messi amesema anakisubiri kwa hamu kikosi hicho cha England.
“Kucheza dhidi ya England ni jambo maalum kwa sababu ni moja ya mataifa makubwa ya soka duniani. Itakuwa mara yangu ya kwanza kukutana nao, hivyo ni mechi yenye maana kubwa.”
Nyota huyo ameongeza kuwa timu yake itajiandaa kikamilifu kuhakikisha inafuzu fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo.