Waarabu kumlipa Vini Jr Pauni 800,000 kwa siku
Muktasari:
- Winga huyo wa Kibrazili anayekipiga kwenye kikosi cha Real Madrid alifunga mabao 24 na kuasisti mara 11 katika mechi 39 msimu uliopita, akiisaidia timu hiyo kubeba ubingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
MADRID, HISPANIA: MKWANJA aliowekewa mezani Vinicius Junior na miamba ya Saudi Arabia utamfanya aweke rekodi ya mkataba mtamu zaidi kuwahi kutokea.
Winga huyo wa Kibrazili anayekipiga kwenye kikosi cha Real Madrid alifunga mabao 24 na kuasisti mara 11 katika mechi 39 msimu uliopita, akiisaidia timu hiyo kubeba ubingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Anapewa nafasi kubwa ya kushinda Ballon d’Or sambamba na wakali wengine, Jude Bellingham na Kylian Mbappe, ambao anacheza nao kwenye kikosi cha miamba hiyo ya Santiago Bernabeu.
Kwa mujibu wa ESPN, Saudi Arabia inajiandaa kuweka pesa ndefu kwenye kichwa cha Vinicius, 24, wakiamini watamshawishi afungashe virago vyake na kuondoka Bernabeu. Kinachoelezwa ni kwamba ofa ambayo imewekwa mezani kwa Vini Jr ni karibu Pauni 300 milioni kwa mwaka, Pauni 25 milioni kwa mwezi, Pauni 800,000 kwa siku na karibu Pauni 10 kwa kila sekunde. Dili hilo litakuwa la miaka mitano litakalokoma 2029.
Vinicius, ambaye ana mkataba wa miaka mitatu Real Madrid, atakwenda kufanywa balozi wa Saudi Arabia kwenye kampeni yao ya Kombe la Dunia 2034 endapo kama atakubali dili hilo.
Public Investment Fund ya Saudi Arabia, inayomiliki asilimia 75 kwenye klabu za Al Ahli, Al Ittihad, Al Hilal na Al Nassr, zimefanya mazungumzo na Real Madrid, lakini miamba hiyo ya Hispania haipo tayari kumuuza Mbrazili huyo. Real Madrid itahitaji kivunjwe kipengele cha kulipa Pauni 850 milioni kilichowekwa kwenye mkataba wa supastaa huyo kutoka Amerika Kusini. Vini Jr alijiunga na Real Madrid akitokea Flamengo mwaka 2018 kwa ada ya uhamisho ya Pauni 40 milioni. Amecheza mechi 264 kwenye kikosi hicho na kufunga mabao 83 na asisti 75.