Mambo matano magumu kwa Maresca
Muktasari:
- Hata hivyo, kuna mambo ambayo yanamsubiri anayopaswa kuhakikisha kwamba anakabiliana nayo ili kuanzisha utawala wake utakaokumbukwa huko Etihad mara tu mkataba wake utakapomalizika miaka mitatu ijayo, ikiwamo kuungwa mkono kutoka kwa uongozi kwa kujiondoa kwenye kivuli cha Pep Guardiola.
LONDON, ENGLAND: KOCHA mpya wa Manchester City, Enzo Maresca ameshaanza kazi, akiweka sawa mambo kabla ya kuanza na mechi ya ufunguzi wa msimu wa 2026/27 ambayo itakuwa Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 18, mwaka huu katika Uwanja wa Wembley jijini London.
Hata hivyo, kuna mambo ambayo yanamsubiri anayopaswa kuhakikisha kwamba anakabiliana nayo ili kuanzisha utawala wake utakaokumbukwa huko Etihad mara tu mkataba wake utakapomalizika miaka mitatu ijayo, ikiwamo kuungwa mkono kutoka kwa uongozi kwa kujiondoa kwenye kivuli cha Pep Guardiola.
KUJIONDOA KWENYE KIVULI CHA PEP
Jinsi Maresca anavyomfuata Guardiola ndiyo swali kali analopaswa kulijibu kutoka kwa mashabiki, wachambuzi, waandishi na muhimu zaidi pale inapohitajika, uwanjani. Katika kipindi cha miaka 10 kilichobadili historia, Guardiola alishinda mataji 20 (ikiwemo Ngao ya Jamii tatu).
Maresca alikuwa kando yake katika ushindi wa makombe matatu kwa mpigo msimu wa 2022/23 walipobeba Ligi Kuu England, FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hii ni kadi moja ya utambulisho kwa wachezaji ambao anapaswa kuwashawishi wamfuate. Nyingine ni msimu mmoja, 2020-21, akiwa kocha wa kikosi cha maendeleo cha Man City ambapo walishinda taji Ligi Kuu England.
Zingine ni kuongoza Leicester City kupanda Ligi Kuu 2024 na kushinda na Conference League 2025 akiwa na Chelsea pamoja na Kombe la Dunia la Klabu kwa mabao 3-0 dhidi ya PSG ya Luis Enrique katika fainali. Zamu yako, Enzo.
AMUINGIZE ANDERSON, AMTOE RODRI?
Rodri ni mtawala laini wa kiungo cha Man City, lakini je, atakuwa kwenye kikosi mwishoni mwa dirisha la usajili la majira ya joto? Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 anatoa ujumbe unaochanganya, akitumia fainali za Kombe la Dunia kuwa na msimamo usio wazi, angalau kuhusu kutaka kubaki hadi mkataba wake umalize 2027.
“Niko mtulivu sana, najua kabisa nilipo na nitakuambia kwamba labda kama kusingekuwa na Kombe la Dunia, mambo yangekuwa tofauti sasa,” amewahi kukaririwa akiwema Rodri. Mhispania huyo anajaribu kurejesha kiwango kilichompa Ballon d’Or 2024 baada ya jeraha kubwa la goti Septemba 2024, na matatizo mengine ya baadaye yanayohusiana nayo, hivyo kuuzwa kunaweza kuwa hatua sahihi kwa mchezaji na klabu, hasa fedha zinapoweza kugharamia mbadala wake, Elliot Anderson (23), wa Nottingham Forest.
AZIBE PENGO VS ARSENAL
Man City walimaliza wakiwa pointi saba nyuma ya mabingwa, Arsenal, katika nafasi ya pili msimu huu baada ya kupeleka changamoto ya ubingwa hadi mechi ya kabla ya mwisho, wakati sare ya 1-1 ugenini Bournemouth ilipowapa Arsenal ubingwa.
Pengo hilo ni kubwa, lakini siyo kwamba haliwezi kufikiwa, na jukumu la Maresca ni kupindua meza. Kama sivyo, lazima awe karibu kuhakikisha timu “bado ipo” (kwa kutumia kauli mbiu ya Guardiola) hadi hatua ya mwisho ya msimu, jambo ambalo litamlinda kazini.
Tatizo kubwa la Maresca ni dhahiri; kipindi hiki ni kigumu hasa mwanzoni mwa utawala wake na anaweza kuonekana kama ‘David Moyes’ wa Man City. Moyes aliyeyushwa mapema tu baada ya Sir Alex Ferguson kumuachia Manchester United, ambako alishindwa kufanya lolote kama mtu aliyemfuata.
KUUNGWA MKONO NA UONGOZI
Kauli ya mwenyekiti wa Man City, Khaldoon al-Mubarak, kwamba kocha hawezi kuwa muhimu kuliko klabu ndiyo msingi wa falsafa ya timu. Isipokuwa kwamba wakati Ferran Soriano na Txiki Begiristain walipoajiriwa na yeye kama ma-CEO na mkurugenzi wa michezo mtawalia 2012 alikuwa akijenga mfumo wa aina ya Barcelona huko Mashariki mwa Manchester uliokuwa tayari kwa ujio wa Guardiola.
Wawili hao walikuwa katika nyadhifa sawa Barcelona wakati (kwa Begiristain) au kabla kidogo (kwa Soriano) ya kipindi cha Guardiola 2008-12. Begiristain aliondoka majira ya joto yaliyopita akibadilishwa na Hugo Viana wakati mabadiliko kutoka Man City inayomzunguka Guardiola yakiendelea na sasa tutaona kama al-Mubarak na wengine wanaweza kuendesha falsafa hiyo baada ya Guardiola.
Kwa nafasi nzuri ya hilo, mambo matatu lazima yafanye kazi kwa pamoja. Kwanza, al-Mubarak, Soriano na Viana wanapaswa kuamini wamechagua mtu sahihi kwa Maresca. Pili, wachezaji lazima waaminiwe. Tatu, na muhimu zaidi, al-Mubarak, CEO wake na mkurugenzi wa michezo lazima waendelee kumuunga mkono hata pale kiwango cha timu kinaposhuka na ukosoaji unapoongezeka.
ATAFUTE NJIA NYINGI ZA MABAO
Tangu Erling Haaland alipowasili 2022, Man City imekuwa ni timu iliyojengwa kumzunguka mshambuliaji huyo namba tisa.
Makombe matatu waliyobeba kwa mpigo (treble), Super Cup na Kombe la Dunia la Klabu, taji la nne mfululizo na msimu uliopita Kombe la Carabao na FA mara mbili vinaonyesha hili lilikuwa jambo la busara.
Tatizo linakuja Haaland anapoumia au kushindwa kufunga kwa kipindi fulani, kwa sababu hilo limekuwa likiiathiri timu hiyo. Kwa kuwa kwake na miaka 25 ameshinda Kiatu cha Dhahabu Ligi Kuu England katika misimu mitatu kati ya minne, hilo ni jambo la nadra sana.
Hata hivyo, misimu miwili iliyopita alifunga “tu” mabao 22 katika Ligi Kuu akiwa wa tatu nyuma ya Mohamed Salah, na mabao mengine manane katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, FA na Carabao. Matokeo yake ni kwamba ukawa msimu pekee ambao Man City hawakushinda taji tangu Haaland ajiunge katika kikosi hicho.