Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi zinavyoibeba Simba fainali ya Kombe la FA

PEMBA Pict


MACHO na masikio ya wapenzi wa soka kwa sasa hapa nchini ni fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kati ya Simba dhidi ya Azam FC, katika mechi kali itakayopigwa leo Julai 4, 2026, kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba saa 11:00 jioni.


Azam inayocheza fainali ya tano tangu msimu wa 2015-2016, ilifika hatua hii kibabe baada ya ushindi wa mabao 3-2, dhidi ya mabingwa watetezi Yanga iliyochukua mara nne mfululizo, huku kwa upande wa Simba ikiifunga Coastal Union mabao 4-0.


Ushindi huo kwa Azam FC wa mabao 3-2, Juni 21, 2026, ulivunja rasmi rekodi ya Yanga ya kucheza jumla ya mechi 28, za Kombe la CRDB bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipochapwa na Simba bao 1-0, Julai 25, 2021, msimu wa 2020-2021.

Mechi hiyo ya mwisho kwa Yanga kuchapwa bao 1-0, dhidi ya Simba, ilikuwa ya fainali ya Kombe la CRDB iliyopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, ambapo rekodi hiyo ilidumu kwa siku 1,792, ambapo ni miaka minne, miezi 10 na siku 27.

Sasa wakati miamba hiyo ya Simba na Azam FC ikikutana katika fainali hiyo inayosubiriwa kwa hamu ya kuhitimisha msimu wa 2025-2026, zipo rekodi za kuvutia ambazo mashabiki wa timu hizo wangependa kuzifahamu kabla ya pambano hilo halijapigwa.

FAIN 01

SIMBA TISHIO FAINALI

Moja ya jambo la kujivunia kwa mashabiki wa Simba, rekodi zinaonyesha tangu michuano hii iliporejea msimu wa 2015-2016, Simba imeingia fainali mara tatu na zote imetwaa taji hilo, jambo linalosubiriwa kuona na msimu wa 2025-2026, itakuwaje.

Simba iliingia fainali ya kwanza msimu wa 2016-2017 na kuifunga Mbao FC ya Mwanza mabao 2-1, iliyokuwa inafundishwa na Kocha Mrundi Etienne Ndayiragije anayefundisha TRA United, huku akizifundisha Azam FC, KMC na timu ya taifa ya Tanzania.

Fainali hii ilikuwa ya kwanza kwa Mbao baada ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2015-2016, huku ikionekana ni timu ambayo haina ushindani japo kilichotokea kwa mashabiki wa Simba hawakuamini kama wangetwaa ubingwa huu kwa kutumia nguvu zaidi.

Mechi hiyo ilipigwa Mei 28, 2017 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo mshindi wa pambano hilo ilibidi apatikane katika dakika 30, za nyongeza baada ya timu hizo kumaliza dakika 90, zikiwa suluhu na hapo ndio mtafaruku ulipojitokeza.

Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao katika muda huo wa nyongeza lililofungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Frederick Blagnon kabla ya Mbao FC kusawazisha kupitia kwa Robert Ndaki na baada ya hapo Simba ikapata penalti mwishoni iliyozua mzozo.

Penalti hiyo iliyofungwa na Shiza Kichuya ndiyo iliyowahakikishia ubingwa wa Simba japo viongozi na wachezaji wa Mbao FC walionyesha wazi kutoridhika na uamuzi uliofanywa na mwamuzi wa kati wa mechi hiyo, Ahmed Kikumbo kutokea jijini Dodoma.

Baada ya hapo, Simba ikaingia tena fainali msimu wa 2019-2020 na kutwaa tena taji hilo kwa kuichapa Namungo FC mabao 2-1, katika mechi kali na ya kuvutia pia iliyopigwa Agosti 2, 2020, kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini, Sumbawanga.

Mabao ya Simba yalifungwa na Luis Miquissone dakika ya 27 huku John Bocco akipachika la pili dakika ya 39 wakati lile la kufutia machozi kwa ‘Wauaji wa Kusini’, Namungo lilifungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Edward Manyama dakika ya 56.

Fainali ya tatu kwa Simba ni ya msimu wa 2020-2021, ilipoichapa Yanga kwa bao 1-0, lililofungwa na Mganda Taddeo Lwanga dakika ya 80, ikiwa ndio iliyokuwa fainali ya mwisho kwa Simba kucheza, kabla ya kurejea tena msimu huu wa 2025-2026.

Mechi hiyo iliyopigwa Julai 25, 2021, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, ilishuhudiwa aliyekuwa kiungo wa Yanga, Mkongomani Mukoko Tonombe akionyeshwa kadi nyekundu pia baada ya kumchezea madhambi nahodha wa Simba, John Bocco.

Kwa maana hiyo, hii ni fainali ya nne kwa Simba kuicheza ya michuano ya Kombe la CRDB, ambapo kati ya tatu zilizopita zote imetwaa taji hilo, jambo ambalo linasubiriwa kuona msimu huu ikiwa itaendeleza rekodi au Azam FC itaivunja rasmi.

FAIN 02

FAINALI YA TANO KWA AZAM FC

Fainali ya msimu huu wa 2025-2026, itakuwa ni ya tano kwa Azam FC kucheza, huku kikosi hicho kikiwa na rekodi mbovu ya kutwaa taji hilo, kwani hadi sasa imetwaa mara moja kati ya nne, ililolichukuwa kwa mara ya kwanza msimu wa 2018-2019.

Azam ilichukua taji hilo baada ya kuifunga Lipuli FC ya Iringa bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Mzambia Obrey Chirwa dakika ya 64, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi, Juni Mosi, 2019.

Katika fainali tatu ambazo Azam FC ilikosa ubingwa wa Kombe la CRDB, zote ilipoteza dhidi ya Yanga, ikianza na ya msimu wa 2015-2016, ilipochapwa mabao 3-1, Mei 25, 2016, kisha na msimu wa 2022-2023, ilipofungwa tena bao 1-0, Juni 12, 2023.

Yanga ikaendeleza nuksi kwa Azam FC ya kutotwaa ubingwa wa CRDB, baada ya kuifunga tena kwa penalti 6-5, msimu wa 2023-2024, kufuatia suluhu (0-0) ya dakika 120, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Juni 2, 2024.

FAIN 03

REKODI ZAIBEBA SIMBA

Ukiachana na Simba kutwaa taji hilo mara tatu zote ilizoingia fainali, ila rekodi zinaibeba pia kwani imekutana na Azam FC mara nne katika michuano ya CRDB kabla ya mechi ya leo Julai 4, 2026, ambapo imeshinda mara tatu na kupoteza moja tu.

Timu hizo zilikutana mara ya kwanza katika nusu fainali ya Kombe la FA iliyopigwa Aprili 29, 2017, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Simba kushinda bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Mohamed Ibrahim ‘MO’ dakika ya 48.

Baada ya hapo timu hizo zikakutana tena katika hatua ya robo fainali iliyopigwa Julai 1, 2020, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Simba ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na John Bocco dakika ya 39 na Clatous Chota Chama dakika ya 56.

Mechi ya tatu kwa timu hizo kukutana ni ya nusu fainali ya Kombe la CRDB, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Ruvuma na Simba kushinda bao 1-0, Juni 26, 2021, lililofungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Luis Miquissone dakika ya 89.

Baada ya hapo Azam FC ikakataa unyonge na kuifunga Simba mabao 2-1, katika mechi kali ya nusu fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, ikiwa ni ushindi wa kwanza wa kikosi hicho, baada ya kuchapwa mara tatu zilizopita.

Mechi hiyo ya nusu fainali iliyopigwa Mei 7, 2023, mabao ya Azam yalifungwa na Lusajo Mwaikenda dakika ya 22 na Prince Dube aliyepo Yanga kwa sasa dakika ya 75, huku la Simba likifungwa na Sadio Kanoute anayeichezea Azam FC dakika ya 28.

FAIN 04

ILIVYOKUWA

Katika michuano ya CRDB msimu huu wa 2025-2026, timu zote mbili zilianzia hatua ya 64 bora kama ilivyokuwa utaratibu wa misimu yote, ambapo Azam FC iliifunga Endument FC ya Kilimanjaro bao 1-0, kisha raundi ya 32, ikaifunga Mbeya Kwanza 1-0. Hatua ya 16 bora Azam FC ilicheza na Fountain Gate na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0, huku hatua ya robo fainali, ikaichapa maafande wa Mashujaa bao 1-0, kisha nusu fainali ikaitoa bingwa mtetezi wa michuano hiyo Yanga kwa mabao 3-2.

Kwa upande wa Simba, ilianza kampeni zake pia hatua ya 64, bora kwa kuichapa Greenland FC ya Kagera mabao 3-0, kisha 32 bora, ikaichapa B19 FC mabao 2-0 na 16 bora ikaifunga Dodoma Jiji 3-1, huku robo fainali ikaifunga TRA United mabao 4-0.

Katika hatua ya nusu fainali iliyopigwa Juni 20, 2026, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Simba ilifuzu kibabe fainali ya Kombe la CRDB, baada ya kuifunga Coastal Union mabao 4-0, ikisaka ubingwa wa kwanza tangu msimu wa 2020-2021.


DONDOO MUHIMU

1967-Mwaka ambao michuano hiyo iliasisiwa ikifahamika Kombe la FAT.

2002-Ilikuwa ni mara ya mwisho kuchezwa kwa Kombe la FAT kwa sababu ilisimama kwa miaka 13 mfululizo.

2015-Mwaka ambao michuano ya FA ilirejeshwa upya na kubadilishwa jina na kuitwa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), kabla ya sasa kuitwa Kombe la CRDB.

01-Ni timu moja tu kutoka daraja la chini ya Tanzania Stars ndio iliyowahi kutwaa ubingwa wa michuano hii.

09-Idadi ya mataji iliyobeba Yanga katika michuano hii ikiwa ndio vinara tangu ilipoanzishwa rasmi mwaka 1967.

04-Mataji iliyotwaa Simba katika michuano hiyo tangu enzi za Kombe la FAT ikishika nafasi ya pili, nyuma ya Yanga.

06-Idadi ya timu nje ya Simba na Yanga zilizotwaa taji la michuano hii tangu enzi za Kombe la FAT.

*-Abdul Suleiman ‘Sopu’ ndiye mchezaji pekee aliyewahi kufunga mabao matatu ‘Hat-Trick’ katika mechi ya fainali dhidi ya Yanga msimu wa (2021-2022), wakati huo alikuwa akikichezea kikosi cha ‘Wagosi wa Kaya’, Coastal Union ya jijini Tanga.