Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

England inaporejea Azteca ikikumbuka ‘bao la mkono wa Mungu’

ENGLAND Pict

Muktasari:

  • Jumapili, Julai 5, Mexico City. Kama kila kitu kingekwenda sawa na kikosi cha England chini ya kocha Thomas Tuchel kingemaliza kileleni mwa Kundi L na kushinda mchezo wa hatua ya 32 Bora, kingecheza hatua ya 16 Bora katika Uwanja wa Azteca uliopo Mexico.

ATLANTA, MAREKANI: MARA tu droo ya Kombe la Dunia ilipokamilika mjini Washington, Marekani, Desemba mwaka jana, tarehe iliandikwa kwenye kalenda na kuwekewa alama nzito na mashabiki wote wa England waliotarajia kusafiri kwenda Mexico, pamoja na mamilioni ya wengine waliokuwa wakijua kuwa wangeshuhudia mechi kutokea nyumbani.

Jumapili, Julai 5, Mexico City. Kama kila kitu kingekwenda sawa na kikosi cha England chini ya kocha Thomas Tuchel kingemaliza kileleni mwa Kundi L na kushinda mchezo wa hatua ya 32 Bora, kingecheza hatua ya 16 Bora katika Uwanja wa Azteca uliopo Mexico.

Kulikuwa pia na uwezekano mwingine. Ikiwa Mexico wangeongoza kundi lao na kusonga mbele wangekuwa wapinzani wa England. Fikiria hali hiyo; England kucheza mechi muhimu ya mtoano dhidi ya mmoja wa wenyeji wa mashindano kwenye uwanja wake mwenyewe.

Azteca ni ngome ambayo Mexico wana rekodi ya kutisha. Ni uwanja wanaouamini sana kutokana na kuchezwa katika mwinuko wa takribani mita 2,240 kutoka usawa wa bahari. Hali hiyo huwafanya wachezaji wa timu pinzani kuchoka haraka na kushindwa kupumua kwa urahisi, lakini siyo kwa Mexico waliozoea mazingira hayo.

Mbali na hilo, zaidi ya mashabiki 80,000 huujaza uwanja huo na kutengeneza mazingira ya kipekee. Kwa wengi, huwezi kusema umeona au umesikia mazingira ya kusisimua ya soka duniani hadi ushuhudie mechi ya Kombe la Dunia inayowahusisha Mexico katika Uwanja wa Azteca.

ENG 01

Kwa England, ndoto hiyo sasa imekuwa kweli baada ya kuifunga DR Congo kwa mabao 2-1 mjini Atlanta, Marekani. Siku moja kabla, Mexico waliifunga Ecuador mbele ya mashabiki wao katika usiku wa shangwe uliodumu hadi alfajiri.

Lakini, kwa mashabiki wa England, Azteca una maana nyingine kubwa zaidi. Ni uwanja unaowakumbusha tukio ambalo halijasahaulika na ambalo limeacha maumivu yasiyofutika katika historia ya soka lao. Ni tukio la “Mkono wa Mungu” wa Diego Maradona.

Katika robo fainali ya Kombe la Dunia 1986 kati ya England na Argentina, Maradona alifunga bao la kwanza kwa kutumia mkono, jambo ambalo waamuzi hawakuliona.

Dakika chache baadaye akaongeza bao la pili baada ya kuwapita karibu wachezaji wote wa England, bao ambalo hadi leo linatajwa kuwa miongoni mwa mabao bora kabisa kuwahi kufungwa katika historia ya mchezo.

ENG 02

Wakati huo, kocha wa England, Tuchel, alikuwa na miaka 12 akifuatilia mechi hiyo akiwa nchini kwao Ujerumani na hakosi simulizi anapozungumzia mchezo huo wa aina yake.

“Halikuwa jambo lililowaumiza Waingereza pekee,” anasema Tuchel na kuongeza:

“Hata mimi nakumbuka tukio hilo. Wakati huo sikuwa na uhusiano wowote na soka la England, lakini nililikumbuka vizuri. Nakumbuka Kombe la Dunia la Maradona, mabao yake mawili dhidi ya England; lile la kupiga chenga na lile lingine... ambalo kwa teknolojia ya sasa ya VAR lisingekubaliwa.”

Je, ni sahihi kusema kwamba Tuchel na kikosi chake wanakwenda Azteca kulipiza kisasi kwa yaliyotokea 1986? Kocha huyo anaonekana kuamini hivyo kwa namna fulani.

“Tutalipwa. Bahati itarudi upande wetu. Karma itafanya kazi yake. Tutabadilisha historia,” anasema huku akitabasamu

Kama ilivyo kwa mashabiki wengi wa soka, Tuchel bado ana kumbukumbu nyingi za Kombe la Dunia 1986, akiikumbuka timu imara ya zamani ya Urusi iliyofungwa mabao 4-3 na Ubelgiji baada ya muda wa nyongeza katika hatua ya 16 Bora.

“Nawakumbuka Vasyl Rats na Jan Ceulemans (mastaa wa zamani wa Urusi). Pia nakumbuka kivuli kilichokuwa katikati ya Uwanja wa Azteca.

Kutokana na jua kali, kivuli hicho hakikuonekana kusogea kabisa wakati wote wa mchezo. Nakumbuka pia kitabu kikubwa cha picha za Kombe la Dunia kilichoonyesha uzuri wa uwanja huu na bendera nyingi zilizokuwa zimepambwa,” anasema.

ENG 03

“Ni uwanja wa kihistoria. Ujerumani ilicheza fainali hapa. Nina hamu kubwa ya kucheza mechi hii. Ni mechi ya kipekee kucheza dhidi ya Mexico nchini Mexico. Tutakuwa tunacheza dhidi ya taifa zima na nguvu za mashabiki wao.”

Tuchel anasema pia picha za Kombe la Dunia 1986 zimewekwa katika hoteli ambayo kikosi cha England kinaishi katika Kituo cha Taifa cha Soka cha St George’s Park.

“Kuna picha kubwa za Gary Lineker (straika wa zamani wa England) akifunga mabao, Peter Shilton (kipa wa zamani wa England) na makocha wa wakati huo. Ni sehemu ya historia kubwa. Huu ni wakati mzuri wa kucheza kwa amani ndani ya Uwanja wa Azteca na kubadili historia,” anasema.

Kwa upande wa Mexico, hamasa imefikia kiwango cha juu ambapo mashabiki wao wengi walitamani kukutana na England badala ya DR Congo.

Katika migahawa mbalimbali ya Mexico City walifurahi Harry Kane alipofunga mabao ya kuchelewa na kuipa England ushindi wa 2-1 dhidi ya Wakongomani. Sababu siyo kwamba wanaiona England kuwa timu dhaifu zaidi, bali wanaamini nguvu yao kubwa wanapocheza Azteca.

Wanataka kuifunga timu kubwa, na kwao England ni mwathirika anayefaa. Takwimu zinaonyesha Mexico wamecheza karibu mechi 150 katika Uwanja wa Azteca na wamepoteza nane pekee. Kipigo chao cha mwisho kilikuwa Septemba 2013.

Tangu wakati huo hawajapoteza mechi 26 mfululizo katika uwanja huo, ukiwemo ushindi mara tatu walioupata kwenye Kombe la Dunia mwaka huu.

Katika historia ya Kombe la Dunia, Mexico wamecheza mechi 10 Azteca (1970, 1986 na 2026), wakishinda nane, sare mbili na hawajapoteza hata mmoja. Pia wameweka rekodi ya kutoruhusu bao katika mechi nane, ikiwemo kila mchezo waliocheza kwenye mashindano ya mwaka huu.

England, kwa upande wao, wamecheza mechi sita Azteca. Mbili zilikuwa dhidi ya Mexico; walitoka sare 1969 na kupoteza 1985.

Katika Kombe la Dunia 1986 waliifunga Paraguay mabao 3-0 katika hatua ya 16 Bora kwenye uwanja huo. Lakini, siyo ushindi huo unaokumbukwa. Kinachokumbukwa zaidi, hasa sasa England wanaporejea Azteca ni tukio la “Mkono wa Mungu” la Diego Maradona ambalo limebaki kuwa moja ya simulizi kubwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia.