Vita ya michuano ya Ulaya imekaa utamu England

Muktasari:
- Wakati mechi za raundi ya 38 kwa kila timu katika Ligi Kuu England zikipigwa Jumapili, vita iliyobaki ni ile ya kupatikana kwa klabu zitakazokamatia tiketi za kucheza michuano ya Ulaya.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England 2024/25 itafika ukomo Jumapili, lakini jambo kubwa lililobaki ni vita ya kuwania nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Wakati mechi za raundi ya 38 kwa kila timu katika Ligi Kuu England zikipigwa Jumapili, vita iliyobaki ni ile ya kupatikana kwa klabu zitakazokamatia tiketi za kucheza michuano ya Ulaya.
Wakati Liverpool ikifanikiwa kubeba ubingwa ikiwa bado na mechi nne mkononi na Southampton, Leicester City na Ipswich Town kushuka daraja wiki kadhaa zilizopita, kasheshe lililobaki ni kwenda kunasa nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya.
Tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao bado haijakamilika. Liverpool na Arsenal zimeshajihakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushika nafasi mbili za juu kwenye msimamo, lakini shughuli ipo kwenye tiketi tatu zilizobaki.
Vita ilivyo kwenye mbio za kufukuzia tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.

Man City (Namba 3, pointi 68)
Mechi: Fulham
Haukuwa msimu bora kwa Manchester City baada ya mwanzoni kuaminika kwamba timu hiyo ingenyakua taji la tano mfululizo la Ligi Kuu England. Lakini, mambo yalikuwa tofauti na sasa kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kinapambana kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Ushindi wa mabao 3-1 ilioupata dhidi ya Bournemouth uliifanya kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi. Hata hivyo, Man City itahitaji kupata ushindi dhidi ya Fulham kwenye mechi ya ugenini huko Craven Cottage ili kujihakikishia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Newcastle United (Namba 4, pointi 66)
Mechi: Everton
Chochote kinachotokea, huu umeshakuwa msimu bora kwa Newcastle United, ambayo ilishinda taji lake la kwanza baada ya miaka 56 iliponyakua Kombe la Ligi, Machi mwaka huu. Newcastle United itakuwa nyumbani kukipiga na Everton katika mechi ya mwisho ya msimu ambapo itahitaji kushinda ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Kwa kunyakua Kombe la Ligi, Newcastle ilijinyakulia tiketi ya kucheza michuano ya UEFA Conference League msimu ujao, lakini dhamira yao ni kumaliza msimu ikiwa ndani ya Top Five ili kupata tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Chelsea (Namba 5, pointi 66)
Mechi: Notttingham Forest
Kwa sehemu kubwa ya msimu, Chelsea ilikuwa inatazamwa kama timu itakayofanya ushindani kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Lakini, mambo yalibadilika baada ya mwaka huu kuanza, lakini tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao bado ipo kwenye mipango yao na kuonyesha mafanikio makubwa kwa kulinganisha na misimu miwili iliyopita ilipomaliza nafasi ya 12 na ya sita. Hata hivyo, kasheshe lililopo mbele yao ni kwamba mechi yao ya mwisho kwenye ligi itakipiga ugenini dhidi ya Nottingham Forest, ambayo pia ipo kwenye mbio za kusaka tiketi ya kucheza Ulaya msimu ujao.

Aston Villa (Namba 6, pointi 66)
Mechi: Man United
Baada ya kuonja utamu wa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, Aston Villa itahitaji kukamatia tena tiketi ya kucheza michuano hiyo msimu ujao. Aston Villa inayonolewa na kocha Unai Emery itasafiri kwenda Old Trafford kukipiga na Manchester United, ikisaka ushindi ili kukamatia tiketi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, kwa Aston Villa itahitaji kushinda mechi yake ya mwisho, huku ikiombea Chelsea na Newcastle United zisipate ushindi kwenye mechi zao za mwisho. Uzuri wa Aston Villa ni kwamba itakipiga na Man United, ambayo haina kitu chochote cha kushindania baada ya kushika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi.

Brighton (Namba 8, pointi 58)
Mechi: Tottenham
Brighton haipo kwenye mbio za kuwania tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini bado ina uwezo wa kucheza michuano ya Ulaya. Kuna njia mbili timu inayoshika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu England inaweza kufuzu kucheza Conference League. Lakini, kwenye njia hizo mbili, zote zitaitaka Chelsea kushinda fainali ya Conference League dhidi ya Real Betis, Jumatano ijayo. Chelsea kumaliza namba saba hilo linawezekana kama watapoteza dhidi ya Forest na kisha Aston Villa ikapata walau sare dhidi ya Man United.
Chelsea inaweza kumaliza namba sita na Newcastle namba saba.
Hii inatokea kama Chelsea itapoteza kwa Forest, Villa ikapata sare dhidi ya Man Utd na Newcastle ikapoteza kwa Everton kwa zaidi ya bao tatu na hapo Chelsea itakuwa chini kwa tofauti ya mabao.

Brentford (Namba 9, pointi 55)
Mechi: Wolves
Kutokana na kuwapo na uwezekano wa tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya kwa Ligi Kuu England kuwa hadi timu inayoshika namba nane kwenye msimamo, Brentford itapaswa kujilaumu yenyewe kama itashindwa kutumia fursa hiyo. Kikosi hicho cha kocha Thomas Frank kimekuwa na msimu mzuri, lakini ilitibua mambo na kuzidiwa na Brighton kwenye mechi iliyopita wakati ilipopoteza uongozi wa mabao 2-1 na kupoteza 3-2 dhidi ya Fulham. Mchezo wao wa mwisho utachezwa Molineux dhidi ya Wolves, ikijaribu kupambana kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao, lakini italazimika kuomba Brighton ipoteze mbele ya Spurs kwa sababu yenye ina tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.