Vita tatu zinazosubiriwa fainali ya Mabingwa Ulaya

Muktasari:
- Hayo ndiyo matarajio ya walio wengi katika kuelekea mchezo huo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mwaka huu wa 2025.
MUNICH, UJERUMANI: MATARAJIO ya mashabiki wengi wa soka ni kushuhudia fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yenye ufundi mwingi baada ya kukutanisha timu mbili zenye utitiri wa wachezaji wenye ujuzi mkubwa wa kuuchezea mpira na kuuamrisha ufanye kile ambacho wanapenda kifanyike.
Hayo ndiyo matarajio ya walio wengi katika kuelekea mchezo huo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mwaka huu wa 2025.
Paris Saint-Germain na Inter Milan, timu mbili zenye mafundi wa mpira wa kutosha, zenye nafasi sawa kwenye vita ya kunyakua taji hilo, zitakutana kuonyeshana ubabe huko Munich, usiku wa Jumamosi hii.
Sambamba na uhodari wao, timu hizo kila moja ina udhaifu wake ambao wapinzani wanaweza kuu-tumia na kupata matokeo hayo, kitu kinachofanya yawepo matarajio ya kushuhudia bato nyingi, hasa zile tatu matata kabisa zitakazonogesha usiku huo wa fainali ya kumsaka mfalme wa Ulaya.
Mwisho wa yote hayo, mshindi ni mmoja tu, ndiye atakayevikwa taji la kuwa bingwa wa soka la Ulaya.
Wakati mashabiki wakikuna vichwa kuona ni timu gani itakayoibuka na ubingwa kati ya PSG, ambao ni mabingwa wa Ligue 1 ya Ufaransa na Inter, ambao wamemaliza nafasi ya pili kwenye Serie A, wakizidiwa pointi moja tu na mabingwa Napoli kinachosubiriwa kwa hamu ni vita zitakazopiganwa kwenye fainali.

1.Nuno Mendes vs Denzel Dumfries
Kama kuna eneo ambalo litakuwa kwenye ushindani mkali katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni pembeni. Timu hizo zote mbili zimekuwa na mabeki wa pembeni na wing-back wenye uwezo mkubwa sana wa kulicheza soka, wabunifu na kila mmoja amekuwa na kiwango bora kabisa katika kutengeneza nafasi za mashambulizi kwa timu yake. Jambo hilo linafanya uwezekano wa kwenda kutokea vita kali katika eneo hilo.
Litakuwa ni suala la kushambulia na kukaba, ambapo upande wa kulia wa Inter Milan na upande wa kushoto wa PSG kutakuwa na vita kali itakayowakutanisha Denzel Dumfries na Nuno Mendes.
Dumfries yupo kwenye kiwango bora sana, akihusika kwenye mabao matano kati ya saba iliyofunga Inter kwenye mechi mbili ilizocheza na Barcelona katika nusu fainali. Anatarajia kwenda mbele kushambulia kwenye mechi hiyo ya fainali, ambako atakumbana na Mendes. Wachezaji wote hao wa pembeni wana uwezo wa kushambulia, basi ni eneo ambalo litakuwa na upinzani mkali.
Kwenye upande mwingine wa uwanja, kutakuwa na bato la Achraf Hakimi na Federico Dimarco. Kazi ipo.

2. Ousmane Dembele vs Yann Aurel Bisseck na Alessandro Bastoni
Ousmane Dembele, amekuwa na msimu mzuri, licha ya kwamba si aina ya mshambuliaji wa kati ambao atakuwa kwenye vita ya moja kwa moja na mabeki wa kati wa Inter Milan, kwa sababu hashambulii kwa kukaa kwenye eneo hilo kama mtu aina ya Erling Haaland. Kazi kubwa inayowakabili mabeki wa Inter ni kumzuia staa huyo wa Ufaransa kwenye mikimbio yake, kuzuia mpira usimfikie na kumnyima nafasi ya kupiga mashuti kitu ambacho kitawafanya Inter kuwa kwenye kasheshe kubwa. Shida ya kukabiliana na Dembele ni kwamba hachezi kwenye eneo moja kwa muda mrefu, anaweza ku-badilishana nafasi kwa kadri mechi inavyokwenda na washambuliaji wenzake kwenye kikosi cha PSG jambo litakaloifanya beki ya Inter kuwa kwenye matatizo makubwa ya kutambua mchezaji wa kumka-ba.
Haitakuwa kazi ya Francesco Acerbi, 37 katika kumkabili Dembele, bali itakuwa ya mmoja kati ya Yann Aurel Bisseck au Alessandro Bastoni ndiyo watakuwa na kasheshe hilo la kutembea na Dembele uwan-jani.

3. Gianluigi Donnarumma vs Inter
Itashangaza kama Gianluigi Donnarumma hatashinda tuzo ya Kipa Bora wa Mwaka wa Fifa msimu huu baada ya CIES Football Observatory kumtambua kama mmoja wa makipa bora kabisa duniani kwa sasa.
Muitaliano huyo ameonyesha kiwango bora kwenye kikosi cha PSG katika kufikia mafanikio makubwa katika safari yao ya michuano ya Ulaya, akiokoa hatari matata kabisa kwenye raundi zilizopita katika mtoano. Katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Arsenal, gazeti moja liliandika kwamba staa wa The Gun-ners, Bukayo Saka atakuwa anaweweseka na zile sevu za Donnarumma alizofanya kwenye mechi hiyo na kuisaidia timu yake kutinga fainali. Hivyo, hata kama Inter Milan ni wajuzi wa kutengeneza nafasi nyingi za kushambulia, itakuwa kwenye vita kali ya kuhakikisha inamvuka Donnarumma kama inataka kunyakua taji lao la nne la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kipa huyo anaweza kwenda kuwa kikwazo kikubwa kwa Inter Milan katika mchezo huo wa fainali na kuipa faida Paris Saint-Germain ili kunyakua taji lao la kwanza.