Viktor Gyokeres apewa maua yake
Muktasari:
- Straika huyo wa kimataifa wa Sweden, Gyokeres alifunga zaidi ya mabao 50 kwenye kikosi hicho cha Sporting msimu uliopita, amekuwa akisifiwa na Ronaldo kama mchezaji mwenye kipaji spesho.
LONDON, ENGLAND: STAA wa zamani wa Sporting CP, Cristiano Ronaldo anauhakika straika mwingine wa zamani wa Sporting, Viktor Gyokeres atafanya balaa kwa sababu hana shaka juu ya kiwango chake.
Straika huyo wa kimataifa wa Sweden, Gyokeres alifunga zaidi ya mabao 50 kwenye kikosi hicho cha Sporting msimu uliopita, amekuwa akisifiwa na Ronaldo kama mchezaji mwenye kipaji spesho.
Gyokeres alicheza chini ya kocha wa sasa wa Manchester United, Ruben Amorim wakati alipokuwa Ureno na kulikuwa na matarajio kwamba angefuata nyayo za Ronaldo kwa kuondoka kwenye klabu hiyo ya Lisbon na kutua Old Trafford.
Badala yake, Gyokeres amechagua kujiunga na Arsenal, ambayo itakipiga na Man United kwenye mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England, Jumapili.
Ronaldo alicheza na Rio Ave na kufunga hat-trick wakati Al Nassr iliposhinda 4-0 katika mechi ya pre-season na baada ya mechi hiyo, supastaa huyo aliulizwa kuhusu kiwango cha straika Gyokeres na huko anakoenda Ligi Kuu England.
“Anakwenda kwenye ligi ya ushindani mkali. Kuhusu Sporting naitakiwa kila la heri, naamini itakuwa bingwa tena,” alisema Ronaldo na kuongeza. “Gyokeres? Mchezaji anayekumbukwa ni yule aliyepo tu kwenye timu. Naamini Sporting itaendelea kuwa timu shindani.
“Gyokeres alikuwa mchezaji spesho, lakini timu lazima iendane na mazingira mapya. Ninaamini (Luis) Suarez, aliyesajiliwa kutoka Almeria ni mshambuliaji mzuri. (Conrad) Harder naye ni mchezaji mzuri, kijana na anahitaji muda.”
Gyokeres alicheza mechi ya kwanza kwenye timu yake mpya wakati Arsenal ilipochapwa 1-0 na Tottenham Hotspur. Alitoka kapa pia kwenye kipigo cha 3-2 kutoka kwa Villarreal, lakini alifunga bao lake la kwanza wakati timu yake ilipoichapa Athletic Bilbao 3-0 kwenye mechi yao ya mwisho ya kirafiki.