Tielemans aing'oa Senegal, Ubelgiji ikienda 16 bora
Muktasari:
- Senegal itajilaumu yenyewe kwani imefanikiwa kucheza kwa uwezo mkubwa mchezo huo kwa dakika 75 ikionyesha kiwango bora kwa kuibana Ubelgiji.
Ubelgiji imefanikiwa kutoka nyuma na kwenda kutengeneza ushindi mzuri ikiichapa Senegal kwa mabao 3-2, ikijikatia tiketi ya kucheza hatua ya 16 bora kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Senegal itajilaumu yenyewe kwani imefanikiwa kucheza kwa uwezo mkubwa mchezo huo kwa dakika 75 ikionyesha kiwango bora kwa kuibana Ubelgiji.
Dakika ya 25, Senegal ilifanikiwa kupata bao la kuongoza likifungwa na kiungo Habibu Diarra akiunasa mpira wa pili uliokuwa unaokolewa na beki wa Ubelgiji.
Senegal ikaendelea kucheza kwa ubora ikizima vizuri mashambulizi ya Ubelgiji, ikimaliza dakika 45 za kwanza ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili Senegal iliendelea kuonyesha ubora na kufanikiwa kupata bao la pili dakika ya 51 kupitia mshambuliaji Ismaila Sarr akifunga kiufundi kwa shuti kali akipokea krosi ndefu kutoka kwa beki wa kati, Moussa Niakhate.
Baada ya bao hilo, Senegal iliendelea kutawala mchezo lakini ikaanza kucheza kwa kupoteza umakini wa kuongeza mabao zaidi kupitia nafasi ambazo ilizitengeneza.
Ubelgiji ikafanikiwa kutoka nyuma kwa kupata bao la kwanza likifungwa na mshambuliaji mkongwe Lomelu Lukaku dakika ya 86 akipokea asisti ya beki Thomas Meunier wawili hao wakitokea benchi wakiingia kwa nyakati tofauti.
Nahodha wa Ubelgiji, Youri Tielemans akaonekana akizozana kwa maneno na mwenzake Leandro Trossard wakati wakienda kwenye mapumziko ya maji.
Hata hivyo wawili hao wakashirikiana kutengeneza bao la pili likifungwa na Tielemans kwa kichwa dakika ya 89 akipokea krosi ya Trossard na kuifanya mchezo huo kumalizika kwa dakika 90, timu hizo zikifungana mabao 2-2.
Ubelgiji katika dakika 30 za nyongeza, ilionyesha ukomavu ikitafuta bao la ushindi na kufanikiwa dakika ya 90+5 kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na Tielemans.
Penalti hiyo ilitokana na kiungo Lamine Camara aliyeingia kipindi cha pili kumchezea vibaya Tielemans na VAR kuonyesha kwamba kulikuwa na madhambi katika tukio hilo.
Matokeo hayo yameivusha Ubelgiji ikifuzu hatua ya 26 bora huku Senegal ikitupwa nje ya mashindano kwa kipigo cha mabao 3-2.