Kiungo Senegal abwaga manyanga akiweka sharti moja
Muktasari:
- Pape Gueye amecheza mechi za Senegal katika Kombe la Dunia 2026, akifunga mabao mawili na kupiga pasi moja ya mwisho.
Saa chache baada ya Senegal kutupwa nje kwenye Fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa kufungwa mabao 3-2 na Ubelgiji, kiungo Pape Gueye ametangaza kujiweka kando kuichezea timu hiyo.
Gueye anayechezea Villarreal ya Hispania, amesema hatoichezea Senegal kama benchi la ufundi la sasa chini ya Pape Thiaw litaendelea kuwepo.
"Nitapumzika kuchezea timu ya taifa kwa muda wote ambao benchi hili la ufundi litaendelea kuisimamia timu,” amesema Gueye.
Gueye ameshindwa kuanika hadharani nini hasa kimetokea baina yake na benchi hilo la ufundi la Senegal hadi akachukua uamuzi huo.
Kiungo huyo amesema anajiandaa kuujulisha umma sababu zilizoikwamisha Senegal katika mashindano hayo siku kadhaa zijazo.
“Nitakuja baadaye kuzungumzia sababu za kutolewa mashindanoni. Lakini leo natangaza kwamba kwa vile benchi hili la ufundi linaendelea kuwepo, nitasimama kuichezea timu ya taifa ya Senegal,” amesema Gueye.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2026, Gueye amecheza mechi nne, akifunga mabao mawili na kupiga pasi moja ya mwisho.
Senegal imeondolewa kwa namna ya kushangaza na Ubelgiji katika mechi ya hatua ya 32 bora iliyochezwa alfajiri ya kuamkia leo, Alhamisi, Julai 2, 2026 kwa muda wa Afrika Mashariki.
Iliongoza kwa mabao 2-0 hadi katika dakika ya 84 ya mechi lakini Ubelgiji ilifunga mabao mawili katika dakika tano za mwisho na kufanya mechi hiyo iende katika dakika 30 za nyongeza.
Wakati wengi wakiamini kwamba mechi hiyo ingemalizika kwa mikwaju ya penalti, Ubelgiji ilifunga bao la tatu katika dakika ya 120, hivyo kuzika rasmi ndoto ya Senegal kusonga mbele.