Marekani yatinga 16 bora Kombe la Dunia, ikiifuata Ubelgiji
Muktasari:
- Katika mechi hiyo ya hatua ya 32 bora iliyopigwa kwenye Uwanja wa San Francisco Bay Area, Santa Clara, California, Marekani, wenyeji walipata bao la kwanza kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Folarin Balogun dakika ya 45.
CALIFORNIA, MAREKANI: WENYEJI wenza wa michuano ya Kombe la Dunia 2026, timu ya taifa ya Marekani, imefuzu hatua ya 16 bora baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Bosnia and Herzegovina.
Katika mechi hiyo ya hatua ya 32 bora iliyopigwa kwenye Uwanja wa San Francisco Bay Area, Santa Clara, California, Marekani, wenyeji walipata bao la kwanza kupitia kwa nyota wa kikosi hicho, Folarin Balogun dakika ya 45.
Nyota huyo ambaye hilo ni bao lake la tatu katika michuano hii, ameendelea kuonyesha kiwango bora akiwa ni muhimili mkubwa kwa timu hiyo inayofundishwa na Kocha, Mauricio Pochettino.
Baada ya kufunga bao hilo, nyota huyo alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 64, kutokana na kumchezea vibaya nyota wa Bosnia, Tarik Muharemovic na kuiweka timu hiyo katika presha ya kucheza pungufu kwa zaidi ya dakika 26.
Licha ya kadi hiyo nyekundu, Bosnia ilishindwa kutumia faida ya kusawazisha bao na kujikuta dakika ya 82, ikifungwa la pili na Malik Tillman.
Ushindi huo kwa Marekani unaifanya kufuzu hatua ya 16 bora ambapo sasa itacheza dhidi ya timu ya taifa ya Ubelgiji iliyofuzu baada ya kuifunga Senegal mabao 3-2, ambapo mechi hiyo itachezwa Jumanne ya Julai 7.
Matokeo hayo yanaifanya Marekani iungane na timu za Mexico na Canada ambazo zote ni waandaaji wa Kombe la Dunia 2026, kufuzu hatua ya 16 bora na kuendelea kuonyesha kiwango cha kuvutia kutokana na ushiriki wao.
Canada ilikuwa ya kwanza kufuzu hatua ya 16 bora baada ya kuichapa Afrika Kusini bao 1-0, Juni 28, ikafuatiwa na Mexico iliyoichapa Ecuador mabao 2-0, Julai Mosi, 2026.
Marekani ambao ni wenyeji wenza wa michuano ya Kombe la Dunia kwa kushirikiana na Mexico na Canada, inashiriki kwa mara ya 12, tangu ilipoanza mwaka 1930, 1934, 1950, 1990, 1994, 1998, 2002, 2006, 2010, 2014, 2022 na sasa 2026.
Miongoni mwa rekodi bora kwa Marekani ni kumaliza nafasi ya tatu katika fainali za mwaka 1930, zilizofanyika Uruguay, pia kufika hatua ya robo fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 2002, lililofanyika kwenye nchi mbili za Japan na Korea Kusini.
Kwa upande wa historia ya Bosnia and Herzegovina katika Kombe la Dunia ni fupi ikilinganishwa na mataifa mengi ya Ulaya, ambapo tangu ilipopata uhuru wake baada ya kuvunjika kwa Yugoslavia mwanzoni mwa miaka ya 1990, inashiriki mwaka huu mara ya pili.
Tangu liwe taifa huru, Bosnia and Herzegovina ilifuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2014, fainali za Brazil, ambapo kikosi hicho kiliishia hatua ya makundi katika kundi F, lililokuwa na timu za Argentina, Nigeria na Iran.
Katika kundi hilo la F, liliongozwa na Argentina iliyokuwa vinara na pointi tisa, Nigeria ilimaliza nafasi ya pili na pointi nne, wakati Bosnia and Herzegovina ilikuwa ya tatu na pointi tatu, huku Iran ikiwa mkiani na pointi moja.
Nyota anayeshikilia rekodi ya kufunga bao la kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kwa timu ya Bosnia and Herzegovina ni Vedad Ibisevic aliyefunga kwenye kichapo cha kikosi hicho cha mabao 2-1, dhidi ya Argentina, mechi ikipigwa Juni 15, 2014.